Dar/Mikoani. Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), kimeamua mambo 10 ya kutekelezwa na wanachama wake, ikiwamo kutokupokea kesi za msaada wa kisheria kutoka mahakamani hadi hatua za kisheria zitakapochukuliwa dhidi ya waliohusika na shambulio dhidi ya Wakili Deo Mahinyila.
Vilevile, TLS kupitia Baraza la Uongozi imetakiwa kupanga na kutangaza siku ya maandamano ya amani ya mawakili nchi nzima, kama ishara ya kulaani kitendo alichofanyiwa wakili huyo na wengine waliowahi kupitia udhalilishwaji au uonevu wakitekeleza majukumu yao.
Inadaiwa Septemba 15, 2025 asubuhi wakili Mahilinya akiwa ndani ya eneo la Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, alishambuliwa hadharani kwa vibao, mateke, ngumi na virungu, vitendo vilivyorekodiwa na vyombo vya habari na kushuhudiwa na umma.
Mbali na tukio hilo, siku hiyo vyombo vya habari viliripoti tukio la askari polisi walioonekana wakiwapiga baadhi ya wanachama wa Chadema waliokwenda mahakamani kufuatilia kesi ya uhaini, inayomkabili Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu.
Akizungumzia tukio hilo bila kugusia suala la Wakili Mahilinya, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaa, Jumanne Muliro alisema: “Asubuhi ya Septemba 15, kundi la wanachama wa Chadema lilianzisha fujo pale mahakamani baada ya ukumbi kujaa, kwa kujaribu kuwashambulia askari polisi.
“Katika hali hiyo, askari walilazimika kujihami na kudhibiti fujo hizo. Ni muhimu kuelewa kuwa kitendo chochote cha kujaribu kuwashambulia askari polisi walioko kazini wakitekeleza majukumu yao ya kisheria hakitavumiliwa, na askari watachukua hatua za kujihami na kurejesha hali ya usalama kadri itakavyohitajika.”
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Baraza la Uongozi wa TLS kwenda kwa wanachama wote Septemba 18, 2025, Chama hicho kimekwishachukua hatua za dharura, ikiwamo kikao kwa njia ya mtandao na kuazimia miongoni mwa mambo mengine, kufanyika maandamano ya amani nchi nzima.
Mwananchi bila mafanikio imeutafuta uongozi wa juu wa Jeshi la Polisi kuzungumzia uamuzi huo wa TLS.
Hata hivyo, katika barua ya Septemba 19, 2025 kwenda kwa TLS Kanda ya Kagera, kuhusu taarifa ya maandamano ya amani, Mkuu wa Polisi, Wilaya ya Bukoba, Marwa Mwita amesema kibali cha maandamano hakijatolewa.
Kwa mujibu wa barua hiyo ambayo Mwananchi imeiona, TLS iliomba kibali cha kufanya maandamano ya amani kuanzia maeneo ya ofisi zake za Bukoba, maeneo ya Bohari GPSA yaliyopo Mtaa/Kata Miembeni Manispaa ya Bukoba kwa kutumia barabara iendayo Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba na kuhitimishwa Mahakama Kuu, Masjala ya Bukoba Septemba 22, 2025 kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 8:00 mchana.
Akieleza sababu za kibali kutokutolewa, mkuu huyo wa Polisi wa wilaya amesema kutakuwa na shughuli za kampeni zinazoendelea kufanyika na askari watakuwa kwenye ulinzi wa kampeni.
Vilevile, amesema barua ya TLS haijaambatishwa kibali kutoka kwa Jaji wa Mahakama Kuu cha kuruhusu maandamano kufanyika hapo kwa siku hiyo na muda huo, jambo ambalo alisema linaweza kuathiri shughuli za mahakama kwa siku hiyo.
Sababu nyingine amesema: “Kesi inayozungumziwa kwenye barua yako ipo Mkoa wa Dar es Salaam na wala si Mkoa wa Kagera.”
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Blasius Chatanda alipotafutwa na Mwananchi leo Septemba 20, 2025 amethibitisha kuitambua barua hiyo.
Ameonya kuwa “watakaothubutu kuanza maandamano ambayo hayajaruhusiwa na Jeshi la Polisi watakutana na mkono mzito wa kisheria.”
Kamanda Chatanda amesema hawajajua maandamano wanayotaka kuyaanzisha siku hiyo, ambayo ni siku ya mahakama, Jaji Mkuu kama hatakuwa na kazi nyingine zaidi ya kuwapokea.
“Kama walitaka barua ya kuanzisha maandamano basi wangeiomba Dar es Salaam kule walipoanzia na si Kagera. Jeshi la Polisi halipo tayari kuwaruhusu kuendelea na maandamano ambayo hawajui ndani yake kuna nini… mtu anaweza kupitia maandamano hayo kupenyeza mambo yake kwa sababu ni kipindi cha kampeni,” amesema.
Taarifa iliyosainiwa na Rais wa TLS, Boniface Mwabukusi, imesema uamuzi wa Baraza la Uongozi baada ya kuzingatia maoni ya wanachama ni pamoja na:
Moja, TLS itoe Tamko kulaani kitendo cha udhalilishaji alichofanyiwa Mahinyila na askari Polisi Septemba 15 akiwa mahakamani. Pili, mawakili wasipokee kesi zozote za msaada wa kisheria kutoka mahakamani hadi pale hatua za kisheria zitakapochukuliwa dhidi ya wote waliohusika na shambulio la aibu na kupata taarifa juu ya hatua hizo zilizochukuliwa.
Tatu, barua rasmi zipelekwe kwa wahusika akiwamo Jaji Mkuu na Waziri wa Katiba na Sheria kuhusu kutokushiriki kwenye shughuli zozote au kutoa msaada wa kisheria.
Nne kuwe na mkutano kati ya TLS, IGP, DPP na AG kuona ni namna gani wanaweza kutatua chanagamoto iliyojitokeza ya kushambuliwa kwa wakili huyo.
Tano, TLS kupitia Baraza la Uongozi na kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi wa Chapters liombe kukutana na Jaji Mkuu ili kumfikishia kilio cha mawakili kupitia tukio la Mahinyila, pia kumpatia maazimio ya TLS.
Sita, TLS kupitia kwa rais wake, ifanye mkutano na waandishi wa habari kulaani na kukemea kilichofanywa dhidi ya wakili huyo.
Saba, TLS kupitia Baraza la Uongozi, ipange na kutangaza siku rasmi ya maandamano ya amani ya mawakili wote nchi nzima kama ishara ya kulaani kitendo hicho.
Nane, itakapotangazwa siku ya maandamano mawakili wote kwa kila Chapter watakutana kwa siku mbili mfululizo kupokea majibu kutoka Mahakama Kuu.
Tisa, TLS kuielekeza kamati yake ya masuala ya katiba na sheria kuchukua hatua za haraka za kisheria dhidi ya ukiukwaji uliofanywa na askari polisi, ikiwa ni pamoja na kufungua mashauri ya kikatiba na kuwasilisha malalamiko rasmi mbele ya Tume ya Utumishi wa Mahakama na vyombo husika vya usimamizi wa Polisi nchini.
Azimio la 10, Mahinyila afungue shauri mahususi mahakamani dhidi ya waliomshambulia kwa majina yao.