Bao la kwanza lampa mzuka Haaland

MSHAMBULIAJI wa Namungo, Abdulaziz Shahame ‘Haaland’ amesema licha ya timu hiyo kuanza Ligi Kuu Bara kwa sare nyumbani, lakini amefurahia kufunga bao lake la kwanza akiwa na kikosi hicho, kwani litamuongezea morali ya kuzidi kupambania nafasi.

Nyota huyo aliifungia bao Namungo dakika ya 90+4, katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Pamba Jiji iliyomalizika kwa sare ya 1-1, kwenye Uwanja wa Majaliwa uliopo Lindi, Septemba 18 mwaka huu, baada ya wageni kutangulia kupitia kwa Mkenya, Saphan Siwa dakika ya 19.

“Malengo yetu yalikuwa kupata pointi tatu kwa sababu tulikuwa nyumbani, lakini kama ulivyoona mechi haikuwa rahisi na hadi mwisho tukapata chochote kitu, nimefurahia kuanza vizuri japo bado nina kazi kubwa ya kufanya kikosini,” alisema Shahame.

Nyota huyo alisema eneo la ushambuliaji analocheza kuna wachezaji bora zaidi na wenye uwezo wa kutimiza majukumu vizuri, isipokuwa jambo kubwa analofanya ili kumtofautisha na wengine ni kuhakikisha kila anapopata nafasi anaitumia ipasavyo.

Shahame anayefananishwa na mshambuliaji wa Manchester City ya England, Erling Braut Haaland, amejiunga na timu hiyo msimu huu wa 2025-2026 akitokea TMA ya Arusha inayoshiriki Ligi ya Championship.

Akiwa na TMA msimu uliopita wa 2024-2025, Haaland aliibuka mfungaji bora wa Ligi ya Championship, baada ya kumaliza na mabao 18, ikiwa ni idadi sawa na nyota wa Mtibwa Sugar, Raizin Hafidh na Andrew Simchimba aliyekuwa Geita Gold.

Shahame aliyejiunga na TMA msimu wa 2022-2023 akitokea Pan Africans baada ya kuachana na Mbeya Kwanza, akiwa na Namungo alimaliza mfungaji bora katika mashindano ya Tanzanite Pre-Season International yaliyohitimishwa Septemba 7, 2025 akipachika mabao manne.