Mfaransa aukubali mziki wa Doumbia, Andabwile

BAADA ya kupoteza mbele ya Yanga katika mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya awali, Kocha wa Wiliete Benguela ya Angola, Bruno Ferry, amekubali ubora wa mastaa wa wapinzani hao, huku Mohamed Doumbia akimshtua.

Bruno raia wa Ufaransa ambaye aliwahi kuifundisha Azam akiwa kocha msaidizi, sasa ni kocha mkuu wa kikosi cha Wiliete ambacho juzi kilikutana na Yanga na kuchezea kipigo cha mabao 3-0 nyumbani kwao Angola.

Akizungumza na Mwanaspoti, Bruno alisema, ubora wa kikosi cha Yanga umemshangaza kwani ni timu ambayo sio rahisi kuwasoma mastaa wote kwa haraka.

Alisema Yanga ilifanikiwa kuwazaidi kila eneo ndio maana ikawa rahisi kwao kuamua matokeo, licha ya timu hiyo kupambana sana kuzuia na kushambulia, lakini wapinzani walishawaweza.

“Kama kocha lazima ni kubali kwamba ubora wa wachezaji ndio ulioamua mechi dhidi ya Yanga, wapinzani walikuwa bora maeneo yote na walifanikiwa kuamua matokeo.

“Bado timu yangu ina mlima mrefu wa kupanda kwa sababu tanatafuta uzoefu kwenye mashindano ya Afrika, ukilinganisha na wapinzani wetu mastaa wao wana uzoefu wa muda mrefu,” alisema kocha huyo.

Bruno alisema Yanga ina wachezaji bora sana kwa jumla, lakini yupo mmoja aliyemshtua, kwani mwanzoni alimuhofia Aziz KI japo alipopata taarifa hatakuwepo kwani ameuzwa, akaona kazi itakuwa nyepesi kidogo, kumbe haikuwa hivyo.

“Nilijua Yanga hawatakuwa na Aziz KI, lakini kumwona Doumbia ilikuwa ni kama sapraizi kubwa kwangu, ni mchezaji mwenye viwango vya hali ya juu.

“Pia kuna Aziz Andambwile, ni kiungo mzuri anacheza kwa nidhamu kubwa kuwapunguzia presha mabeki wake, kiufupi tulikutana na kipimo kigumu, lakini hatujakata tamaa, tutajipanga vizuri kwa ajili ya mchezo wa marudiano kwa kuwa sasa wameshaiona Yanga vizuri,” alisema.

Ushindi huo wa Yanga ulipatikana kwa mastaa watatu ambao walifunga mabao hayo na la kwanza likifungwa na Andabwile dakika ya 32, Edmund John dakika ya 72 na Prince Dube dakika ya 81.

Yanga imerejea Dar leo alfajiri ikitokea Angola, ambapo baada ya safari hiyo itakuwa na maandalizi ya mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Pamba Jiji utakaochezwa Septemba 24 mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, kisha Septemba 27 itashuka tena uwanjani hapo kurudiana na Wiliete.