UONGOZI wa KMC umesema kwa sasa kila kitu kimekamilika kwa kocha mkuu wa timu hiyo raia wa Brazil, Marcio Maximo, baada ya kushindwa kukaa benchi katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara msimu wa 2025-2026, dhidi ya Dodoma Jiji.
Katika mechi hiyo iliyopigwa Septemba 17, 2025 kwenye Uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge jijini Dar es Salaam, Maximo alikaa jukwaani na kikosi hicho kiliibuka na ushinda wa bao 1-0, lililofungwa na Daruweshi Saliboko dakika ya 56.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Mtendaji Mkuu wa KMC, Daniel Mwakasungula alisema kilichosababisha hali hiyo kutokea ni kutokana na kuchelewa kwa leseni yake ya ukocha, kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
“Ni kweli wengi wetu walikuwa na maswali kwa sababu ya kumuona jukwaani ila suala la leseni yake ndio ilikuwa changamoto kidogo, tumekamilisha kila kitu na mechi yetu ya Septemba 23 dhidi ya Singida Black Stars ataonekana,” alisema Mwakasungula.
Mwakasungula alisema baada ya ushindi wa mechi ya kwanza, mashabiki wa timu hiyo watarajie mambo mazuri, kwani wachezaji wote waliosajiliwa kwa msimu wa 2025-2026 ni bora na wao kama uongozi umezingatia zaidi ripoti ya benchi lao la ufundi.
Hii ni mara ya tatu kwa Maximo kuja tena Tanzania kufundisha soka, baada ya awali kuifundisha Taifa Stars kuanzia mwaka 2006 hadi 2010, kisha akaifundisha Yanga mwaka 2014, akiwa ni miongoni mwa makocha waliojizoelea umaarufu hapa nchini.
Maximo amerejea nchini akiwa na kumbukumbu nzuri, kwani ndiye kocha wa kwanza pia kuiongoza timu ya taifa ya Taifa Stars kufuzu Michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza Ligi za ndani (CHAN), iliyofanyika Ivory Coast mwaka 2009.