Bado Watatu – 35 | Mwanaspoti

Raisa alifanya kazi ya ziada kunibembeleza ninyamaze na akanipa moyo kwamba yaliyonitokea ni mitihani tu na kwamba Mungu ataniepushia balaa.

Muda wa kulala ulipowadia, Raisa alinikaribisha chumbani mwake. Raisa hakuwa na mume, lakini nilipoingia chumbani mwake niliona suruali ya kiume aina ya jeans imetundikwa kwenye mlango.

“Mbona kuna suruali ya kiume humu ndani?” nikamuuliza.

“Nina bwana wangu; huwa anakuja kulala hapa siku moja moja,” akajibu.

“Lakini kwa leo hatakuja?”

“Nimeshampigia simu, nimemwambia asije mpaka utakapoondoka.”

“Anaonekana ni mvulana mtanashati.”

“Hao ndio wanaopenda kuvaa ma-jeans. Mume wangu pia anapenda kuvaa ma-jeans sana. Ana jeans zake mbili kama hii; alizinunua Kenya. Siku moja alizipeleka kwa dobi; alipokwenda kuzichukua dobi, akamuibia jeans moja.”

“Alimwambia eti alikuja mwizi usiku akaiba nguo ikiwemo ile jeans. Mume wangu akaamua kumsamehe.”

“Kwani wewe humfulii mume wako?”

“Ninamfulia ila majinzi ninamwambia apeleke kwa dobi.”

“Basi wewe humpendi mume wako. Mbona mimi ninamfulia bwana wangu.”

“Mwenzangu mimi nguo zote namfulia lakini majinzi yamenishinda, ni magumu japokuwa mume nampenda.”

Nilipomwambia hivyo Raisa alicheka.

“Ni magumu kweli shoga yangu. Mimi pia hupeleka kwa dobi lakini namdanganya huyo bwana kuwa nimefua mimi.”

Maneno yake yakanifanya nijaribu kucheka lakini kicheko changu kilikuwa huzuni tupu. Nilikuwa na furaha gani ya kucheka wakati pingu za polisi zilikuwa zinanisaka!

Tukalala. Saa kumi na moja na nusu asubuhi nikamuamsha Raisa aliyekuwa akikoroma kama chura.

“Kumekucha shoga, nataka nijitayarishe kwa safari,” nikamwambia baada ya kuamka.

Tukashuka kitandani, tukaingia bafuni pamoja na tukaoga pamoja. Tulipotoka kuoga, nilifungua begi langu nikatoa nguo nyingine na kuvaa.

Baada ya nusu saa tukawa kwenye bajaj. Raisa aliamua kunisindikiza stendi.

Tulipofika nilikata tikiti ya mabasi ya kampuni moja. Hilo basi lilikuwa linaondoka saa moja.

Nilikaa na Raisa mpaka basi hilo lilipotaka kuondoka ndipo nikaagana naye. Raisa akaenda zake na basi likaondoka kuelekea Dar.

Huko Dar nilikuwa na ndugu zangu wengi tu. Ilikuwa ni mimi nichague nifikie kwa nani ambako nitakuwa salama zaidi. Kuhusu kula na kupata mahitaji mengine, halikuwa tatizo kwani ndugu zangu karibu wote walikuwa na uwezo wa kutosha.

Kilichotakiwa ni mimi kuwaeleza ukweli ndugu zangu na kuwataka wawasiliane na wazazi wangu ili kupata ukweli zaidi.

Mpaka muda ule basi linaondoka, nilikuwa nimepata amani ndani ya moyo wangu kwamba nimeweza kuutoka mji wa Tanga bila matatizo.

Tulipofika wilaya ya Muheza, basi lilisimama. Pale huwa kuna abiria wengine wanaopakiwa ambao walikata tikiti za basi hilo. Lakini kabla ya abiria yeyote kuingia ndani ya basi hilo, niliona polisi wawili, mmoja mwanamke, wakiwa wamefuatana na mtu mmoja aliyevaa kiraia. Waliingia ndani ya basi hilo na kuuliza kama ndani ya basi hilo kulikuwa na abiria anayeitwa Rukia.

Nikashituka lakini nikanyamza kimya. Baada ya kuuliza mara tatu na mimi kuwa kimya, polisi hao pamoja na yule mtu aliyevaa kiraia walikuja moja kwa moja hadi kwenye siti niliyokuwa nimekaa. Yule polisi mwanamke akaniambia:

“Hebu tuone tikiti yako.”

Nikatoa tikiti yangu na kumpa. Akaisoma jina kisha akawambia wenzake:

Ilibaki kidogo tu nipigwe kibao na yule mtu aliyevaa kiraia ambaye nilihisi alikuwa askari wa upelelezi.

“Si tumeuliza hapa Rukia ni nani, ukanyamza kimya!” akaniambia kwa ukali.

Nikaendelea kunyamza huku mwili wangu ukitetemeka.

“Sasa safari yako inaishia hapa. Tunarudi Tanga ulikokimbia. Ulidhani kuwa hatutakupata!”

Niliwaacha waseme wanavyotaka. Sikuwajibu chochote. Maneno waliyoniambia licha ya kuwa ya kashfa hayakushughulisha akili yangu. Akili yangu ilikuwa imeshughulishwa na kesi ambayo ilikuwa mbele yangu baada ya kukamatwa.

Nilishajua kwamba ule ulikuwa ndio mwisho wangu. Nitakwenda sota mahabusi hadi nife. Na hata kama nitanusurika kufa bado hukumu ya kifo itakuwa inaningoja.

Kwa hiyo wale polisi hata kama wangenitukana nisingewajali. Maisha yangu yaliyokuwa mikononi mwao ndio niliyajali zaidi.

Wakati nasimama kutoka kwenye siti, nilitiwa pingu za mikono kama muuaji. Sikushituka kwani ni kweli nilikuwa natuhumiwa kwa mauaji. Nilishushwa kwenye basi kama anavyoshushwa mfungwa kutoka katika gari la mahabusi.

“Baba yangu na mama yangu nawambia kuwa nimeshakamatwa,” nikajisemea kimoyo moyo kutokana na taharuki lililonipata.

Gari la polisi lilikuwa kwenye mlango wa basi. Vile nashushwa kwenye basi tu nikaingizwa kwenye gari la polisi. Nilikuta polisi wengine wawili, mmoja mwanamke na mwingine mwanamme.

Safari ya kurudi Tanga ikaanza. Safari yangu ya kwenda Dar ilikuwa kama mbio za sakafuni zilizoishia ukingoni!

Sikuweza kujua wale polisi walijuaje kuwa nilikuwa katika basi hilo. Nilichokigundua ni kuwa walilifukuza lile basi kutoka Tanga na kulipata pale Muheza.

Sikutaka kumtilia shaka rafiki yangu Raisa. Sikudhani kwamba ndiye aliyewaambia polisi hao kuwa nimo kwenye basi hilo ninaenda Dar. Kama Raisa angetaka kunisaliti angenisaliti pale pale nyumbani kwake. Asingeniacha nilale hadi asubuhi nijipakie kwenye basi kisha ndio awambie polisi. Alikuwa na uwezo wa kuwapigia simu usiku ule ule bila mimi kujua.

Nikiwa nimewekwa katikati ya polisi wawili wanawake, niliendelea kusimangwa na polisi hao karibu safari nzima. Kila polisi alisema lake.

Waliniambia kuwa sikuwa na akili kumuua hawara yangu nyumbani kwangu na kisha kwenda kuitupa maiti yake makaburini.

“Halafu ni aibu. Mwanamme mwenyewe ni rafiki wa mume wako?” Polisi mmoja akaniambia.

“Sasa ulimuulia nini, ukampiga rungu mwenzako? Alikunyima pesa?” polisi mwingine akadakia.

“Kwa vyovyote vile sababu za kumpiga zitakuwa ni za kipuuzi tu na sidhani kwamba alijua kama mwenzake atakufa.” Polisi hao waliendelea kunichambua.

“Halafu polisi wanafika nyumbani kwako unajidai kukimbia. Wewe huwezi kutukimbia sisi.”

“Sasa mwache akakutane na mkono wa sheria.”

“Hapa anajifanya goigoi hasemi, utadhani siye aliyempiga rungu mwenzake. Au pia unataka ukatae kwamba hujampiga rungu na kumuua…?”

Hakukuwa na yeyote niliyemjibu. Niliwambia kimoyomoyo: “Semeni hadi mchoke, sitawajibu chochote. Roho yangu nimeshamwachia Mwenyezi Mungu.”

Kwa vile gari hilo lilikuwa likienda mwendo kasi kidogo, baada ya saa moja kasorobo tukaingia jijini Tanga. Safari ikaishia kituo cha polisi cha Chumbageni. Pale nikashushwa na kuingizwa ndani ya kituo hicho.

Kwanza niliwekwa kwenye benchi ili nisubiri kuhojiwa. Baada ya robo saa hivi nikaingizwa katika ofisi ya idara ya upelelezi ambako kulikuwa na inspekta mmoja wa polisi upande wa upelelezi ambaye alinitambulisha jina lake. Aliniambia anaitwa Inspekta Amour na yeye akataka kujua jina langu.

Nilipomtajia jina langu aliliandika kwenye karatasi kisha akaniuliza umri wangu.

“Nina miaka ishirini na saba,” nilimjibu.

“Ni mkazi wa hapa Tanga?”

“Unakijua unachotuhumiwa?” akaniuliza huku akitabasamu.

Alipotabasamu alinipunguzia uoga kidogo. Vile alivyokuwa kijana pamoja na suti ya kijivu aliyovaa bila tai, alionekana kuwa mcheshi na mwenye utu, kinyume na tabia za polisi wengi ambao huonekana kuwa wakali wakati wote.

“Sikijui,” nikamjibu.

“Hujui umefanya kosa gani?” akaniuliza tena huku akiendelea kutabasamu lakini tabasamu la sasa lilikuwa la kutoamini maelezo yangu.

“Sawa. Unatuhumiwa kwa mauaji ya Shefa Bamkuu. Nadhani unafahamu hilo na ndiyo maana ulikimbia wakati polisi walipokufuata nyumbani kwako. Lakini baadaye tulipata taarifa kuwa umeondoka kwenda Dar. Si umekamatwa wilaya ya Muheza ukielekea Dar?”

“Ndiyo nilikamatwa Muheza.”

“Sawa. Sasa ninataka kuchukua maelezo yako. Lakini nataka nikupe onyo kwamba maelezo hayo yanaweza kutumika kama ushahidi dhidi yako. Kwa hiyo nieleze kile kitu cha kweli ambacho kilitendeka kwa hiyari yako mwenyewe.”

Inspekta huyo akanitajia tarehe ya siku ambayo Shefa aliuawa, akaniuliza nilikuwa wapi usiku huo.

“Nilikuwa nyumbani kwangu,” nikamjibu.

Inspekta alinitolea simu ya Shefa akaingia katika eneo la kupiga na kunionesha namba yangu ambayo ilibaki hapo baada ya Shefa kunipigia usiku ule.

“Hii ni namba ya nani?” akaniuliza.

“Mlikuwa na mawasiliano na marehemu Shefa katika tarehe hii?”

Nisingeweza kukataa kwa sababu tayari polisi walikuwa na mkanda wa mazungumzo yangu na Shefa.

“Ndio nilikuwa na mazungumzo naye.”

Inspekta huyo alitoa simu nyingine na kuingia katika eneo la WhatsApp.

“Sikiliza, uniambie kama umezitambua hizo sauti,” akaniambia.

Mara kidogo nikaanza kuzisikia sauti za maongezi yetu mimi na Shefa.

“Utakubaliana na mimi kwamba hizi sauti ni za wewe na Shefa?”