KOCHA wa AS Port, Seninga Innocent, amesema kuchagua kuutumia Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Zanzibar kwa mchezo wao wa nyumbani dhidi ya KMKM kutoka visiwani hapa, sio sababu ya kushindwa kirahisi, bali watapambana kupata ushindi.
Innocent ameyasema hayo jana Jumamosi Septemba 20, 2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea mchezo wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya awali dhidi ya KMKM utakaochezwa leo Jumapili saa 10:15 jioni kwenye Uwanja wa New Amaan Complex.
Wakati Innocent akiyasema hayo, Kocha wa KMKM, Hababuu Ali amesema wameshajiandaa kimwili na kiakili kucheza mechi hiyo, ingawa wanatambua michuano hiyo ni migumu lakini wanahitaji kuimaliza mechi hiyo ambayo watakuwa wageni.
Mechi hizo zote mbili za hatua ya awali katika Kombe la Shirikisho Afrika, zitachezwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Zanzibar baada ya AS Port kuuchagua kwa mechi yake hiyo ya nyumbani.
“Kuchagua uwanja kwa mpinzani haitujengei hofu ya kuwa wenyeji kutumia fursa, tumejipanga vyema ndio maana tumefanya uamuzi huo,” amesema Innocent.
Amesema wamechagua mchezo wao wa nyumbani upigwe Zanzibar kwa sababu ya hali ya hewa yake kwani hawataki kuwa na safari zaidi ndio maana ya kufanya hivyo.
Hatahivyo, amesema amefurahishwa na mapokezi mazuri ya KMKM kwani wameifanya safari yao kuwa nyepesi zaidi.
Kwa upande wa Hababuu, ameeleza kuwa, anaamini kikosi chake kitafanya vizuri katika mechi hiyo kutokana na kujipanga kwao.
“Tutatumia silaha zetu kumuangusha mpinzani na lengo letu ni kushinda mechi hiyo tukiwa ugenini”, amesema Hababuu.
Nahodha wa KMKM, Juma Khalfan Khatib, amesema watapambana ipasavyo kuitetea nembo ya timu hiyo kutokana na mafunzo waliyoyapata kwa mwalimu wao.