Biashara ya maziwa inavyowainua kiuchumi wanawake wa Mwika

Moshi. Wakati changamoto ya ajira ikiendelea kuwa kikwazo nchini, baadhi ya wanawake wa Kata ya Mwika Kaskazini, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro wameeleza namna shughuli ya uuzaji wa maziwa ya ng’ombe inavyowainua kiuchumi na kuboresha maisha ya familia zao.

Wanawake hao ambao wamejikita katika ufugaji wa ng’ombe wa maziwa na kuuza maziwa  katika kiwanda cha kuchakata maziwa cha Kondiki kilichopo kwenye kata hiyo, wamesema wanapata zaidi ya Sh1 milioni kila mwezi kutoka kiwandani hapo, jambo ambalo huwasaidia kukidhi mahitaji yao ya kila mwezi pamoja na kusomesha watoto wao.

Wanawake hao wamesema hayo Septemba 20, 2025 wakati mabalozi 12 kutoka Umoja wa Ulaya (EU) walipotembelea kiwanda hicho na kujionea shughuli za uzalishaji zinazoendelea katika kiwanda hicho ambacho kila siku hukusanya zaidi ya lita 7,000 za maziwa kutoka kwa wafugaji.

Akizungumza mmoja wa wafugaji hao  katika Kijiji cha Lyasongoro, Joyce Mnyenye amesema kiwanda hicho kimekuwa mkombozi wao mkubwa kwa kuwa, awali walikuwa hawana mahali pa kuuzia maziwa, hivyo walikuwa wakigawa bure mtaani.

Amesema uwepo wa kiwanda hicho umewafanya wanawake kujishughulisha kwa hali na mali, hivyo kuondokana na changamoto ya ajira kwa kuwa kila mwezi wanapokea fedha zaidi ya Sh1 milioni kulingana na uzalishaji wao.

Amesema mtu anapokuwa na bidii zaidi kwenye ufugaji, ndipo anapopata fedha nyingi zaidi kwa kuwa lita moja ya maziwa huuza kwa Sh1,000 kiwandani hapo.

“Kiwanda hiki cha kondiki kimetunufaisha sisi wafugaji, mwanzoni tulikuwa tukikamua maziwa na tulikuwa hatujui pa kuyapeleka, baada ya kufunguliwa kiwanda hiki sasa hivi tunauza maziwa yetu hapa, tunapata fedha na tumeweza kusomesha watoto na matumizi mengine,” amesema Joyce.

“Hivi sasa tuna ajira ya uhakika maana mwisho wa mwezi tunakwenda kiwandani kupokea fedha kulingana na maziwa uliyouza, fedha zile tunafanya nazo matumizi ya familia pamoja na mambo mengine ya kimaendeleo.”

 “Kwa siku nakamua lita 35 za maziwa ya ng’ombe, nauza Sh1,000 kwa lita moja na mwisho wa mwezi napokea Sh700,000 kutokana na kuuza maziwa, wanawake wa hapa kijijini tuna ajira ya uhakika ndiyo maana tunapambana usiku na mchana,”amesema Joyce.

Mfugaji mwingine, Lucy Moshi amesema tangu aanze shughuli ya ufugaji amepata manufaa makubwa kwa kujipatia kipato cha uhakika na kuweza kufungua biashara nje ya ufugaji huo pamoja na kujenga nyumba ya kisasa.

“Tangu nianze kuuza maziwa kwenye kiwanda hiki, maisha yangu yamebadilika, nimeweza kumudu gharama za familia yangu bila kutegemea msaada yoyote,” amesema Lucy.

Meneja wa kiwanda hicho, Adrian Kimario amesema kwa sasa wanahudumia wafugaji zaidi ya 1,500 kutoka maeneo mbalimbali ya wilaya za Moshi na Rombo, hali ambayo imesababisha kuongezeka kwa uzalishaji wa maziwa.

Amesema kwa siku kiwanda hicho hukusanya maziwa lita 7,000 kutoka kwa wafugaji.

“Sasa hivi tunahudumia wafugaji 1,500; kiwango kikubwa cha maziwa kimeongezeka kutokana na sisi kushirikiana kwa karibu sana na wafugaji pamoja na kuwafundisha mbinu za kisasa za kuzalisha,” amesema Kimario.

“Mwaka 2018 tulipoanza, tulikuwa tunakusanya lita 1,500 za maziwa kwa siku lakini sasa hivi tunakusanya lita 7,000 kwa siku. Tunaendelea kuwafundisha wafugaji wetu namna bora ya ufugaji, kuwatafutia wataalamu wa kuwaelekeza, tuna imani ndani ya miaka kadhaa ijayo kiwango kinaweza kuongezeka mara dufu na kuleta tija kwa wafugaji.”

Kimario amesema kiwanda hicho kwa sasa kimetoa soko la uhakika la maziwa ambayo yanazalishwa na wafugaji pamoja na ajira rasmi 50 kwa wananchi wanaozunguka eneo hilo.

 Kiongozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Christine Grau amepongeza jitihada zinazofanywa na kiwanda hicho katika uzalishaji na kuwainua wafugaji wakiwamo wanawake na vijana, akisema wataendelea kushirikiana na Tanzania katika kuboresha mazingira ya kazi.