Kifungo chawang’ang’ania waliopora Sh117 milioni mali ya Leopard Tours

Arusha.  Matumaini ya kurudi uraiani kwa wafungwa watatu waliokuwa wakipambana kujinasua na kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la uporaji wa Sh117 milioni kwa mtutu wa bunduki, yametoweka baada ya rufaa yao kutupwa.

Mwaka 2019 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Salim Msamila, Shaban Kambongo na Issa Mohamed, walihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kupora Sh117.4 milioni mali ya Kampuni ya Leopard Tours ya jijini Arusha.

Washtakiwa hao wakakata rufaa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Arusha na kusiklilizwa na Jaji Joachim Tiganga ambaye aliitupa, hawakukata tamaa wakakata rufaa Mahakama ya Rufani Tanzania, ambayo nayo imeitupilia mbali rufaa yao.

Katika hukumu yao waliyoitoa Septemba 19,2025 ambayo ipo katika Mfumo wa Taarifa za Maamuzi, Sheria na Kanuni za Tanzania (TanzLII), jopo la majaji watatu, Rehema Mkuye, Lucia Kairo na Abdul Issa, walizitupa sababu 17 za rufaa hiyo.

Kwa hukumu hiyo, wafungwa hao wamefika mwisho katika ngazi ya rufaa na wanabakia na njia mbili tu, ama kufungua maombi ya kurejewa kwa hukumu hiyo kwa dosari za kisheria tu au wapate msamaha wa Rais kwa mujibu wa Katiba.

Tukio la uporaji lilivyokuwa

Ushahidi uliowafunga unaeleza kuwa, Septemba 5, 2017 katika mzunguko wa magari wa Impala jijini Arusha, watu hao wakiwa na silaha aina ya bastola na nyundo walipora Sh117.4 milioni mali ya Kampuni ya Leopard Tours.

Siku hiyo, shahidi wa kwanza wa Jamhuri, Imran Ismail ambaye ni mhasibu wa kampuni hiyo, akiwa na gari aina ya Toyota Alteza, alikwenda Benki ya M iliyopo kijenge kwa lengo la kuchukua fedha kwa hundi mbili zenye thamani hiyo.

Baada ya kufika benki, aliegesha gari lake nje, akachukua begi la rangi nyeusi lililokuwa na hundi hizo na kwenda kuzikabidhi kwa ‘cashier’ aitwaye Ibrahim na akarudi nyumbani kwa ajili ya chakula cha mchana na kuswali.

Alirudi benki baadaye saa 9:00 alasiri na kuchukua fedha Sh117.4 milioni na kuziweka kwenye begi na kuanza safari ya kurejea ofisini, lakini alipofika mzunguko wa magari wa Impala, alibaini uwepo wa gari jeupe mbele yake.

Wakati huo ilikuwa saa 10:15 alasiri, gari hilo lilimzuia kwa mbele na alijaribu kupiga honi ili gari hilo limpishe, lakini ghafla akavamiwa na mtu mmoja aliyevunja kioo cha gari na kuanza kuchukua begi lenye hela kwa nguvu.

Kwa kutumia mkono wake wa kushoto, shahidi huyo alijaribu kupambana kuzuia kuchukulia kwa begi hilo na mtu huyo, alipoona anashindwa kuchukua begi hilo, alizunguka upande wa kulia wa dereva na kuvunja kioo cha gari hilo.

Ni katika purukushani hizo, ghafla alijitokeza mtu mwingine aliyemnyooshea bastola kichwani na kumuamuru aachie begi hilo vinginevyo angemuua, aliachia begi hilo ambalo majambazi hao walizima gari yake na kuondoka na funguo.

Wakati huohuo, alibaini kumuona mtu wa tatu akiwa amesimama mbele yake na kulikuwa na pikipiki upande wa kulia wa gari lake, majambazi hao walipora kwa kutumia pikipiki.

Kwa mujibu wa shahidi huyo, tukio hilo lilidumu kwa dakika tano tu na lilifanyika mchana hali iliyowezesha kuwaona majambazi hao.

Baadaye aliweza kuwatambua katika gwaride la utambulisho lililoandaliwa na polisi.

Alieleza kuwa,  alimtambua mrufani wa kwanza, Salim Msamila ndiye aliyemtisha kwa bastola na mrufani wa pili, Shaban Kambongo ndiye aliyesimama pembeni ya gari na wa tatu, Issa Mohamed ndiye alivunja vioo vya gari kwa kutumia nyundo.

Ushahidi wa Jamhuri ulimhusisha pia shahidi wa tatu, Koplo Abdallah mwenye namba F.2596 aliyefanya upekuzi nyumbani kwa mrufani wa pili na kufanikiwa kupata Sh7, 514,000 ambazo ni sehemu ya fedha zilizoporwa.

Katika utetezi wao uliokataliwa na Mahakama, warufani wote watatu walijiweka kando na tuhuma hizo na kukana kufahamiana huku mrufani wa kwanza, Salim Msamila akidai alilazimishwa kutia saini maelezo yake ya onyo.

Katika rufaa yao wakipinga uamuzi wa jaji Tiganga aliyebariki kifungo cha miaka 30 jela walichohukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, waliwasilisha sababu za rufaa 17, wakitaka kutiwa kwao hatiani kubatilishwe na wachiwe huru.

Miongoni mwa sababu hizo ni kwamba, jaji alikosea kisheria na kimantiki kwa kubariki kifungo hicho wakidai  ziliegemea utambuzi ambao ni dhaifu na haukuweza kuwatambulisha, hivyo ilikuwa ni makosa kisheria kuegemea ushahidi huo.

Pia walieleza, wapo mashahidi muhimu wa jamhuri waliopaswa kuitwa lakini hawakuitwa kutoa ushahidi.

Mbali na sababu hiyo, walidai jaji alikosea kisheria na kimantiki kwa kuegemea ushahidi wa kielelezo namba 2 cha upande wa mashitaka ambacho ni Sh7,514,000 zilizopatikana kutokana na upekuzi ulifanyika kinyume cha sheria.

Ukiacha sababu hizo, pia walilalamika kuwa jaji alikosea kisheria na kimantiki kwa kujielekeza vibaya kuwa gari lenye namba za usajili T327 CJY  la mrufani wa kwanza na pikipiki iliyokuwa ikiendeshwa na Issa zilitumika katika tukio hilo.

Pia, walieleza jaji alikosema kisheria na kimantiki kuegemea kwenye kidhibiti ambacho ni Sh7,514,000 zinazodaiwa ni sehemu ya zile zilizoporwa wakati fedha hizo hazikuwa na alama yoyote kutoka Benki ya M iliyotoa fedha hizo.

Hata hivyo, baada ya jaji kusikiliza sababu hizo za rufaa na hoja za upande wa jamhuri kutoka kwa mawakili wa Serikali waandamizi, Janeth Sekule, Blandina Msawa na Tusaje Kapange, Mahakama ilizikataa hoja  zote.

Majaji pamoja na maelezo mengine, walisema kiasi kilichoporwa kilithibitishwa na Operesheni Meneja wa Benki ya M, hivyo kulikuwa hakuna haja ya kumwita mkurugenzi wa Kampuni ya Leopard Tours kutoa ushahidi wake.

Kulingana na majaji hao, ushahidi uliotolewa na mashahidi wa jamhuri ulitosha kuthibitisha shitaka dhidi yao, hivyo hoja yao kuwa jaji alikosema kisheria na kimantiki wakati kuna mashahidi muhimu hawakuitwa, haina mashiko.