Unguja. Ahadi za kujenga mshikamano, amani na utulivu, maendeleo ya watu na kukuza uchumi, ndizo zinazoonekana kuyatawala majukwaa ya kampeni za urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM).
Tayari kampeni hizo zilizozinduliwa katika Uwanja wa Mnazimmoja Unguja, zimeshatimiza siku ya saba tangu zilipoanza, zikibakiza mwezi mmoja kabla ya upigaji kura, utakaofanyika Oktoba 28 na 29, mwaka huu.
Kampeni hizo, zinamhusisha mgombea urais wa chama hicho, Dk Hussein Ali Mwinyi anayewania kuiongoza Zanzibar kwa kipindi cha pili, anachuana na wagombea wa vyama takriban 10, huku mpinzani mkuu akiwa, Othman Masoud Othamn wa Chama cha ACT- Wazalendo.
Kwa nyakati tofauti, Dk Mwinyi amesema ni CCM pekee ndiyo chama chenye sera za kuwakomboa wananchi na dhamira ya kweli katika kuleta mabadiliko.
Mara nyingi, anaijenga hoja hiyo akirejea kazi iliyofanywa na Serikali yake katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, hivyo atakapopewa ridhaa kwa mara nyingine, atafanya zaidi.
Katika moja ya ahadi zake, Dk Mwinyi amesema katika kipindi cha uongozi wa awamu ijayo, atahakikisha kila eneo la nchi hiyo anaacha alama isiyofutika.
Ametaja msingi wake mkuu katika awamu ijayo ya uongozi wake ni kuendelea kuleta amani na mshikamano, kukuza uchumi na kuimarisha huduma za kijamii.
“Tutaondoa masuala ya ubaguzi wa kila aina, ukabila, dini, rangi, ukanda wa Pemba na Unguja, Ukaskazini na Ukusini, katika awamu ijayo tutaendelea amani na kudumisha umoja wetu kama nilivyoahidi mwaka 2020,” amesema.
Ikiwa ni mwanzo wa utekelezwaji wa hilo, Dk Mwinyi amesema wanafanya kampeni za kistaarabu, bila kumtukana mtu kwa kueleza wanayotarajia kuwafanyia Wazanzibari ili kuondoa changamoto zao.
Ukiacha amani, Dk Mwinyi amesema suala la ajira ni eneo lingine atakalolishughulikia kuhakikisha vijana wanapata fursa kama ilivyoainishwa katika Ilani ya chama chake au zaidi.
“Nataka niwaahidi vijana, Serikali itafanya kila namna kukuza viwanda na kuimarisha kilimo na kuwawezesha, kwa hiyo ajira zitazalishwa nyingi,” amesema.
Dk Mwinyi amesema ni imani yake uchumi utakuwa kutoka asilimia 7.4 ya sasa hadi kufika asilimia 10 kabla hajaondoka madarakani.
“Ndugu zangu tumefaya mengi na tutahakikisha tunaendeleza yale ambayo tuliyafanya, naomba mtuchague tena ili tukayamalizie haya,” amesema.
Hata hivyo, amesema msingi wa yote hayo ni wananchi kuhakikisha wanajitokeza kupiga kura katika uchaguzi mkuu ili upatikane ushindi mkubwa utakaoondoa malalamiko ya wizi wa kura kutoka kwa wapinzani.
“Ndugu zangu ushindi unapokuwa mdogo unaibua manung’uniko, sasa kwa wingi wetu huu namba tujitokeze tushinde kwa kishindo tusiwape nafasi ya kudai hayo,” amesema
Dk Mwinyi wakati akizungumza na waendesha bodaboda, wajasiriamali na wakulima eneo la Mndo, amesema wanakusudia kuimarisha biashara za wajasiriamali na kuwatengenezea ushirika bodaboda ili wamiliki pikipiki zao wenyewe.
Katika kulifamnikisha hilo, alisema wataongeza mikopo isiyokuwa na riba kutoka Sh96 bilioni zilitolewa katika kipindi kinachomalizika na kuwa mara mbili zaidi.
Akiwa kisiwani Pemba, Dk Mwinyi amesema wanakwenda kuifungua kupitia katika sekta mbili, ujenzi wa bandari na uwanja wa ndege wa kimataifa na mkandarasi anatarajiwa kukabidhiwa kazi hiyo, Septemba 25 mwaka huu.
Kwa upande wa bandari, amesema tayari wameanza kujenga na manufaa yameanza kuoneakana kwa kuboresha Bandari ya Mkoani huku nyingine za Shumba zikiendelea na mchakato wa ujenzi.
Kwa upande wa karafuu, amesema watawapa hatimiliki wakulima wa zao hilo ili wayamiliki mazao hayo ili kuona tija, badala ya kuwakatisha tamaa wakulima.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Mohamed Said Dimwa amesema chama hicho kimekuja na upepo mpya wa siasa za mshikamano na demokrasia ya kweli.
“Tunaamini umoja wetu, sera zetu zinatupeleka katika kupata ushindi wa kishindo katika kipindi hiki cha pili,” amesema.
Dk Dimwa ametaja maeneo 10 mahususi ya vipaumbele vya CCM ambavyo vimeanishwa katika ilani ya chama hicho ya mwaka 2025/30.
Mambo hayo ni kuendeleza na kuwaunganisha wananchi wa Zanzibar ili kuleta maendeleo na mafanikio, kuleta uchumi imara na ajira 350,000 kwa vijana.
Kipaumbele kingine, amesema ni kujenga maghala makubwa ya chakula, kuendeleza wananchi kiuchumi, kuanzisha makazi bora, kukuza teknolojia na kudhibiti taka ili kuweka miji katika hali ya usafi.
Dk Dimwa ametaja jambo jingine ni kuanzisha hifadhi ya mafuta ya petroli na dizeli ili kuondoa changamoto ya bidhaa hiyo kupanda bei kila mara.
Katika kampeni hizo marais wastaafu awamu ya sita, Amani Karume na awamu ya saba, Dk Mohamed Shein wamepata fursa kuzungumza na kumnadi mgombea wao.
Amani Karume amewasihi wanachama hao na wananchi kuweka sawa kadi zao za kupigia kura ili siku ikifika kila mmoja ajitokeze kupiga kura nyingi kwa chama hicho.
“Tutunze kadi zetu za mpiga kura vizuri siku ikifika tukapige kura, halafu turudi nyumbani tuendelee kuomba tukisubiri ushindi wetu,” amesema Karume.
Dk Shein alimpamba Dk Mwinyi akisema ana uwezo mkubwa kuijenga Zanzibar, hivyo anastahili kuungwa mkono na kumchagua katika kipindi cha pili.
Dk Shein amesema katika kipindi cha miaka mitano Dk Mwinyi ameiongoza Zanzibar kwa mafanikio makubwa na wala hakubahatisha, bali amepitia kwenye misingi ya ilani ya chama hicho.
“Dk Mwinyi anastahiki kupewa nafasi nyingine akafanye makubwa, maana uwezo wake ni mkubwa aliyoyafanya, kwa miaka mitano anathibitisha uwezo wake wa kufanya kazi,” amesema.
Amesema hapana shaka Dk Mwinyi kasimama kidete kujitolea kusimamia umoja, mshikamano wa nchi na amekuwa akihubiri amani na kumtanguliza Mungu wakati wote.
Amesema katika awamu yake ya kwanza amejenga miradi mikubwa itakayozalisha ajira zaidi ya 25,000 yenye thamani ya Dola 6.2 bilioni za Marekani.
Amesema amewakomboa wanyonge, wenye kipato cha chini, maisha duni na kuwainua kiuchumi kwa kutoa mikopo 5,369 yenye thamani ya Sh39 bilioni.
“Haya sio mambo ya kubeza tunatakiwa kuunga mkono na kumpa nguvu aifikishe Zanzibar mbali,” amesema.
Amesema ameanzisha harakati za uchumi wa buluu licha ya wengi awali kubeza jambo hilo, lakini ameonesha mafanikio makubwa katika sekta hiyo.