Askari Magereza ajiua akidaiwa kushiriki mauaji ya askari mwenziye

Njombe. Askari wa Jeshi la Magereza mkoani Njombe, Erasto Mlelwa (26) amejiua kwa kujirusha kutoka kwenye gari la polisi baada ya kubainika kushiriki mauaji ya askari mwenzake, Dickraka Mwamakula (24) huko Lilondo, halmashauri ya Madaba mkoani Ruvuma.

Hayo yamebainishwa leo Septemba 21, 2025 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga wakati akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya Jeshi la Polisi mkoani Njombe.

Amesema jeshi hilo lilikuwa linaendelea na uchunguzi kufuatia taarifa za kupotea kwa askari Mwamakula ambaye aliripotiwa kupotea tangu Septemba 7, 2025 ambapo mara ya mwisho alikuwa na askari mwenzake, Mlelwa.

Amesema askari hao walielekea eneo moja lililofahamika kwa jina la Lilondo huko Madaba kwa ajili ya kuangalia mashamba lakini baada ya hapo, Mwamakula hakuonekana mpaka Jeshi la Polisi lilipoanzisha uchunguzi wa kina.

Erasto Mlelwa anaedaiwa kujiua baada ya kubainika kushiriki mauaji ya askari mwenzeo huko Madaba mkoani Ruvuma.

“Jeshi la Polisi lilianzisha uchunguzi wa kina chini ya makachero waliobobea na kumpata huyu askari Erasto Mlelwa ambaye alikuwa naye,” amesema Banga.

Ameongeza kuwa katika mahojiano na askari huyo pamoja na kufika eneo ambalo walikwenda kuangalia shamba, alipatikana mtu mwingine, Braison Mtalika (15) ambaye ni mkulima, mkazi wa huko Ruvuma.

Amesema watuhumiwa hao wote wawili baada ya mahojiano walionyesha mwili wa Mwamakula mahali ulipo ukiwa na majeraha makubwa eneo la kisogoni lakini mwili wake ukiwa umechomwa moto na kufukiwa katika eneo la mashamba.

Amesema Jeshi la Polisi wakati linaenda Hospitali ya Lilondo kwa ajili ya kumpata daktari ili kufanya uchunguzi wa mwili huo (postmortem) mtuhumiwa Mlelwa aliamua kujiondoa uhai wake kwa kuruka kutoka kwenye gari na kuangukia kichwa.

“Askari huyo alipofikishwa katika hospitali ya Lilondo, tayari alikuwa amepoteza maisha lakini chanzo cha tukio hili la kusikitisha ni wivu wa kazini, kwamba marehemu Mwamakula alionekana kupendwa kazini kutokana na utendaji wake mwema wa kazi na tulitarajia atalitumikia Taifa hili kwa weledi   alionao.

“…lakini huyu mwenzake amemuonea wivu na kumtuhumu alikuwa anapendwa na viongozi kwa sababu anawaroga baadhi ya watumishi,” amesema Kamanda Banga.

Amesema mwili wa marehemu Mwamakula umehifadhiwa katika Hospitali ya Kibena kwa ajili ya taratibu zingine za mazishi lakini mwili wa Mlelwa ambaye amejiua upo huko Madaba kwa ajili ya kusubiri uchunguzi wa daktari.

Ametoa wito kwa watumishi wa Serikali kuwa weledi wa mtu ndiyo unaomfanya kupata vyeo au madaraka na siyo kutegemea imani za kishirikina.

Kamanda wa polisi mkoa wa Njombe akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa. Picha Seif Jumanne

Ametumia nafasi hiyo kulipa pole Jeshi la Magereza mkoani Njombe kwa kupoteza askari wawili na Mungu aendelee kuwatia moyo na watakuwa pamoja katika mazishi ya askari hao.

Mkazi wa Njombe, Abdallah Liku amewataka watumishi kuzingatia weledi wanapokuwa katika majukumu yao ya kazi na kuacha imani za kishirikina kwa kuamini wenzao wanafanikiwa kwa kufuata njia hizo.

“Ni matukio ya ajabu sana mtu kuamini mwenzio anafanikiwa kutokana na ushirikina na siyo kufanya kazi kwa weledi,” amesema Liku.