Nasser bingwa Africa, Patel Mkwawa Rally

DEREVA Mtanzania, Yassin Nasser na msoma ramani Mganda, Ally Katumba ndio mabingwa wa Afrika kwa mwaka 2025 licha ya kumaliza nafasi ya tatu katika raundi ya tano ya ubingwa wa mbio za magari wa Afrika zilizomalizika jana Jumapili.

Dereva huyo aliyekuwa akiendesha gari aina ya Ford Fiesta R5 alimaliza nafasi ya tatu kwa upande wa ubingwa wa Afrika akitumia saa 7:45:1.

Wakienda kwa jina la Moil Team, Nasser na Katumba walimaliza msimu na pointi 133 na kuwaacha wapinzani wao wa karibu, Samman Vohra nad Drew Sturrock kwa pointi 3 baada ya wao kumaliza na 130.

Raundi hii ya tano na ya mwisho iliyokwenda kwa jina la Mkwawa Rally of Tanzania, pia ilimtawaza Prince Charles Nyerere kama bingwa wa Afrika kitengo cha ARC 2.

Mshindi wa jumla wa mbio hizo alikuwa ni bingwa mtetezi Karan Patel kutoka Kenya aliyetumia saa 7:13:7 na kumshinda Samman Vohra pia kutoka Kenya akiendesha gari aina ya Skoda Fabia alitumia saa 7:21:9.

Ahmed Huwel wa Iringa aliyemaliza wa tatu kwa jumla, ndiye aliyeongoza katika kinyang’anyiro cha ubingwa Tanzania akiingiza gari mpya ya daraja la ubingwa wa dunia, Toyota GS Yarris.

Huwel alikuwa wa tatu kwa kasi baada ya kutumia saa 7:31 akimaliza mbele ya Nasser na Naveen Puligilla, aliyeshika nafasi ya tano akitumia saa 8:11:1.

Nafasi ya sita ilishikwa na dereva mkongwe Samir Shanto wa Morogoro aliyeongozwa na msoma ramani mkongwe, Maisam Fazal ndani ya Ford Fiesta Proto.

Nafasi ya saba ilishikwa na Prince aliyekuwa akiendesha gari aina ya Mitsubishi EvoX, huku dereva  kutoka Burundi Mohamed Roshanali alimaliza nafasi ya saba mbele ya Waleed Nahdi  na Shehzad Munge kutoka Dar es Salaam.