BAADA ya kusoka kwa siku 481 katika Ligi ya Championship, Mtibwa Sugar imeanza vibaya Ligi Kuu Bara msimu huu, kufuatia kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Mashujaa katika mechi iliyopigwa jioni hii kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, mkoani Kigoma.
Mabingwa hao wa zamani wa mwaka 1999 na 2000 ilishuka daraja msimu wa 2023-2024, baada ya kuburuza mkia na pointi 21 na imerejea msimu huu, lakini imeshindwa kutamba katika mechi hiyo ya kwanza kutokana na bao la dakika ya 32, lililofungwa na nyota wa Mashujaa, Idrisa Stambuli.
Stambuli ambaye hilo ni bao la kwanza kwake kwa Ligi Kuu msimu huu akiwa na maafande hao wa Mashujaa, alilifunga kwa ustadi mzuri baada ya kupokea pasi safi iliyopigwa na Mudathir Said na kumshinda kipa wa Mtibwa, Costantine Malimi.
Kabla ya pambano la leo, mara ya mwisho kwa Mtibwa kucheza Ligi Kuu Bara ilichezea kichapo cha mabao 5-1, kutoka kwa Ihefu ambayo kwa sasa ni Singida Black Stars, katika mechi kali iliyopigwa kwenye Uwanja wa Liti Singida, Mei 28, 2024.
Katika mechi hiyo, Ismail Mgunda anayeichezea Mashujaa kwa sasa aliifungia Ihefu mabao matatu ‘Hat-Trick’, huku mengine yakifungwa na Emmanuel Bola na Morice Chukwu, wakati bao la kufutia machozi la Mtibwa Sugar lilifungwa na Seif Karihe.
Ushindi huo ni wa kwanza kwa Mashujaa katika Ligi Kuu msimu huu, baada ya awali kuanza msimu kwa sare ya kufungana bao 1-1, dhidi ya maafande wenzao wa JKT Tanzania, katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika Septemba 18, 2025.
Mabingwa hao wa Ligi ya Championship msimu wa 2024-2025, ikivuna pointi 71, baada ya kushinda mechi 22, sare mitano na kupoteza mitatu, ikiungana kupanda Ligi Kuu Bara na Mbeya City iliyomaliza ikiwa nafasi ya pili na pointi 68.
Mara ya mwisho kwa Mashujaa na Mtibwa kukutana katika Ligi Kuu Bara kabla ya pambano la leo, ilikuwa pia kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, ambapo kikosi hicho cha maafande kiliibuka na ushindi wa mabao 3-2, mechi iliyopigwa, Mei 25, 2024.
Katika pambano hilo, mabao ya Mashujaa yalifungwa na aliyekuwa nyota wa kikosi hicho, Reliants Lusajo aliyefunga mawili na lingine lilifungwa na Mundhir Vuai, wakati ya Mtibwa yalifungwa na Seif Karihe huku, Samson Madeleke akijifunga pia.
Kichapo hicho ni cha kisasi baada ya pambano la kwanza la msimu wa 2023-2024, Mtibwa kushinda mabao 2-1, yaliyofungwa na Seif Karihe na Matheo Anthony, huku lile la Mashujaa likifungwa na Adam Adam, katika mechi iliyopigwa Desemba 19, 2023.
Ligi hiyo itaendelea tena usiku huu kwa Namungo kuvaana na Tanzania Prisons iliyotoka kupigika mbele ya Coastal Union katikati ya wiki hii. Wenyeji Namungo ilitoka sare ya 1-1 na Pamba Jiji katika mechi iliyopita.