……………
📌 Wajadili ushirikiano katika kuzalisha umeme wa nyuklia nchini
📌 Watanzania kujengewa uwezo katika masuala ya nyuklia
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mha. Felchesmi Mramba ameongoza ujumbe wa Serikali ya Tanzania katika kikao na Shirika la Taifa la Nyuklia la China (China National Nuclear Corporation – CNNC), kujadili fursa za ushirikiano katika kuanzisha na kuendeleza mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia teknolojia ya nyuklia.
Katika kikao kilichofanyika jijini Vienna, Austria pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa 69 Wa Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomi (IAEA), Wawakilishi wa CNNC waliieleza Tanzania kuwa kampuni hiyo ina uzoefu mkubwa katika kujenga na kuendesha mitambo ya kuzalisha umeme wa nyuklia, na wako tayari kushirikiana na Tanzania katika hatua mbalimbali za utekelezaji wa miradi ya aina hiyo.
“Tanzania imeanza maandalizi ya kuzalisha umeme kwa kutumia nyuklia ikiwa ni utekelezaji wa dhamira na nia njema ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuona nchi inakuwa na vyanzo endelevu, salama na vya uhakika vya nishati, hivyo tupo tayari kushirikiana na CNNC katika safari hii ya kuzalisha umeme wa nyuklia.” Amesema Mramba
Ametoa shukrani kwa CNNC kwa kuonesha nia ya kushirikiana na Tanzania, akibainisha kuwa Serikali ya Tanzania imeamua kuwekeza katika mradi wa kuzalisha umeme wa nyuklia kama sehemu ya mkakati wa kuongeza upatikanaji wa nishati endelevu na ya uhakika.
 Katika kikao hicho, CNNC imeahidi kushirikiana na Tanzania katika kujenga uwezo wa kitaalamu kwa Watanzania kupitia mafunzo ya kiufundi, ziara za mafunzo, pamoja na kutoa ufadhili kwa masomo ya uzamili katika fani ya nyuklia. Hatua inayolenga kuhakikisha Tanzania inakuwa na wataalamu wa kutosha kusimamia na kuendeleza miradi ya nishati ya nyuklia nchini.
Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Bw. Jing Zhang, Mkuu wa Idara ya Ufundi wa IAEA, Mha. Joseph Kirangi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Maji na Madini kutoka Zanzibar, Prof. Najat Mohamed, Mkurugenzi Mkuu wa Kamisheni ya Nguvu za Atomi Tanzania (TAEC), Mha Innocent Luoga, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu na Wataalam wa masuala ya Nyuklia.
Â