Mbeya. Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Uchumi nchini (Tiseza) imesema licha ya mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kuwekeza zaidi katika kilimo, imeanza kutoa elimu na kutangaza fursa nyingine kwa wawekezaji huku ikitangaza maeneo matano ya kipaumbele kwa ajili ya uwekezaji.
Akizungumza leo Septemba 21, 2025 katika kilele cha Tamasha la Maonesho ya Biashara Kusini yaliyofanyika mkoani Mbeya, Ofisa Uwekezaji wa mamlaka hiyo Nyanda za Juu Kusini, Privata Simon amesema wametumia tamasha hilo kutoa elimu na kuhamasisha wananchi na kusogeza fursa za uwekezaji.
Amesema Tiseza ina majukumu matatu ikiwa ni kutangaza fursa za uwekezaji ndani na nje ya nchi, kuwawezesha wawekezaji na kuishauri Serikali kuhusu uwekezaji akieleza kuwa Nyanda za Juu Kusini ina fursa nyingi ambazo wawekezaji watanufaika nazo.
“Mbali na kilimo ambacho ndio wengi wameelekeza nguvu, kuna sekta ya uvuvi ambapo kwa sasa kuna samaki aina ya mbasa ambaye yuko Matema pekee, utalii tunazo mbuga za wanyama, milima na mito ambazo mwekezaji atanufaika nazo,” amesema Privata.
Ameongeza kuwa hadi sasa Tiseza imetenga maeneo matano maalumu kwa ajili ya uwekezaji ikiwa ni Bagamoyo na Kwala (Pwani), Nala (Dodoma), Buzwagi (Shinyanga) na Ubungo jijini Dar es Salaam, kwamba maeneo hayo yana fursa mbalimbali kama ardhi.
Amewaomba wananchi hususani wazawa kuchangamkia fursa hiyo ili kujiinua kiuchumi na kuongeza pato la nchi akiitaka mikoa ya Katavi, Rukwa, Songwe na Mbeya kuwa sehemu ya kuwekeza nje ya kilimo.
Kwa upande wake, Ofisa Uhamasishaji Uwekezaji wa mamlaka hiyo, Cuthbert Kangila amesema Tiseza inalenga kuimarisha uchumi wa nchi akieleza kuwa mataifa mengi yaliyoendelea yamewekeza zaidi kwenye viwanda.
Amesema Rais Samia Suluhu Hassan alianzisha taasisi hiyo akilenga kupanua wigo kiuchumi kwa wananchi kupitia uwekezaji, akiwaomba wananchi kutumia fursa hiyo kuongeza pato lao na Taifa kwa ujumla.
“Hii Taasisi inalenga kuimarisha uchumi, mataifa mengi yaliyoendelea yametumia viwanda kama sehemu ya kichocheo kiuchumi, niwaombe wananchi kutumia nafasi hii kuwekeza zaidi ili kufikia malengo,” amesema Sangila.
Mmoja wa wananchi na mwekezaji wa kampuni ya Livy Afrika mkoani Mbeya, Christopher Mwasambili amesema Tiseza imefanya mambo makubwa akieleza kuwa katika mpango wa Dira ya Taifa 2050 inaweza kusaidia.
“Tuna mazao ya kimkakati ambayo Tiseza inaweza kusaidia kuongeza mnyororo wa thamani hasa katika hii Dira ya Taifa ya 2050, tutaendelea kushirikiana na taasisi hii kufungua fursa nyingi za uchumi kupitia uwekezaji,” amesema Mwasambili.