NMB yatoa fursa ya mkopo hadi Sh500 bilioni kwa mteja mmoja

Dar es Salaam. Benki ya NMB imesema ina uwezo wa kumkopesha mteja mmoja zaidi ya Sh500 bilioni kwa ajili ya kuendeleza shughuli za biashara na uzalishaji ikiwamo kilimo, mifugo, viwanda na madini, kutokana na ukuaji wa mtaji wake.

Mikopo hiyo inalenga kuwasaidia wateja kuongeza uzalishaji na hutolewa kupitia suluhu mbalimbali za kifedha kulingana na mahitaji ya kila mmoja.

Kauli hiyo imetolewa jijini Mbeya jana Jumamosi Septemba 20, 2025 na Mkuu wa Idara ya Biashara wa benki hiyo, Alex Mgeni katika hafla ya chakula cha jioni na wafanyabiashara wakubwa kutoka mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu.

“Tunahitaji kuona wateja wetu wakikua kibiashara na kiuchumi. Hata hivyo, tunawahimiza kuendelea kutumia huduma za kidijitali ikiwamo NMB Mkononi na Internet Bankingambazo hupunguza gharama na muda wa kufika matawini,” amesema Mgeni.

Pia, amesema benki hiyo imeanzisha mkopo maalumu wa nishati safi ya kupikia kwa wafanyabiashara wenye riba nafuu ya asilimia moja kwa mwezi na asilimia 12 kwa mwaka.

Mkuu wa Kitengo cha Kilimo wa NMB, Nsolo Mlozi amesema wateja wa Kanda ya Nyanda za Juu wamekuwa wakijihusisha zaidi na shughuli za kilimo ikiwamo mikopo ya mitambo, magari ya kusafirisha mazao, ununuzi wa mazao na pembejeo.

“Ongezeko la uzalishaji limefanya baadhi ya mazao ya chakula kama viazi na mpunga kubadilika na kuwa ya kibiashara. Hivyo, benki yetu inakusudia kuanza kutoa mikopo ya mitambo ya umwagiliaji ili kuongeza tija na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi,” amesema Mlozi.

Meneja wa NMB Kanda ya Nyanda za Juu, Wogofya Mfalamagoha amesema benki hiyo kwa sasa ndiyo kubwa zaidi nchini, ikiwa na matawi kila wilaya na mawakala hadi vijijini.

Amebainisha kuwa, miaka miwili iliyopita NMB ilikuwa na mawakala 20,000 pekee, lakini kwa sasa imefikia 60,000 nchi nzima, hatua inayoonyesha kuimarika kwa huduma zake.

Mteja wa benki hiyo, Ralph Makundi amesema mikopo ya NMB imemsaidia kukuza kampuni yake ya ujenzi kutoka daraja la sita hadi kufikia daraja la kwanza, jambo lililomuwezesha kushiriki kwenye kandarasi kubwa za ujenzi wa miundombinu.

“NMB imenisaidia kutanua mtaji na kujenga uwezo wa kufanya kazi kubwa kitaifa,” amesema Makundi.