Geita. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kesho Septemba 22, 2025 anatarajiwa kufungua maonyesho ya nane ya teknolojia ya madini mkoani Geita, yanayokutanisha washiriki zaidi ya 1,300 kutoka ndani na nje ya nchi zikiwamo China, Korea, Namibia, Kenya na Uganda.
Maonyesho hayo yalianza Septemba 18, 2025 yanatarajiwa kufungwa Septemba 28, huku idadi ya washiriki ikiwa zaidi ya 500 walioshiriki mwaka jana.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumapili Septemba 21, 2025 Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigela amesema maonyesho hayo ni fursa muhimu kwa wananchi kushuhudia teknolojia mpya katika utafiti, uchimbaji, uchenjuaji na uongezaji thamani ya madini.
“Tofauti na mwaka jana, mwaka huu tumeboresha miundombinu kwa kujenga mabanda tisa ya kudumu na kuweka taa, ili shughuli za kiuchumi ziendelee hata baada ya maonyesho kufungwa,” amesema Shigela.
Amesema Mkoa wa Geita unaongoza kwa uzalishaji wa dhahabu nchini, ukizalisha zaidi ya tani 12 kwa mwaka na zaidi ya tani 50 katika kipindi cha miaka minne iliyopita.
Pia, amebainisha ongezeko la wafanyabiashara wadogo kutoka ndani na nje ya nchi na kuwataka wananchi kutumia fursa hiyo kujikwamua kiuchumi.
Ofisa Madini Mkazi Mkoa wa kimadini Geita, Samuel Shoo amesema maonyesho hayo yamekuwa msaada mkubwa kwa wachimbaji wadogo ambao sasa wanazalisha zaidi ya kilo 4,000 za dhahabu kwa mwaka, ikilinganishwa na kilo 2,000 kabla ya kuanza kutumia mitambo badala ya zebaki.
“Maonyesho haya yamewaunganisha wachimbaji na wawekezaji wanaowaletea teknolojia mbalimbali za uchimbaji na uchenjuaji, jambo lililowasaidia kuachana na zebaki na kutumia mitambo ya CIP inayoongeza uzalishaji,” amesema Shoo.
Shoo ameongeza kuwa teknolojia hizo zimewawezesha wachimbaji kuachana na mbinu hatarishi kwa afya na mazingira, huku wengine wakihamia kwenye uchimbaji salama kwa kutumia chuma badala ya miti.
Mchimbaji mdogo wa dhahabu mjini Geita, Leonard Bugomola amesema kupitia kliniki zilizotolewa kwenye maonyesho hayo, wachimbaji wameongeza tija.
“Tulikua tunatumia karasha zinazotumia dizeli lakini sasa tumehamia kwenye CIP zinazotumia umeme na mitambo ya kisasa, Tumeachana na zebaki na sasa tunatumia cyanide,” amesema Bugomola.
Bugomola ameongeza kuwa maonyesho hayo yamechochea fursa za kiuchumi kwa Manispaa ya Geita.
Maonyesho ya mwaka huu yanaongozwa na kauli mbiu isemayo: “Ukuaji wa sekta ya madini ni matokeo ya matumizi ya teknolojia sahihi na uongozi bora, shiriki uchaguzi mkuu.”
Mbali na teknolojia za madini na shughuli za ujasiriamali, mwaka huu kumeongezwa ubunifu wa kuvutia watalii, ikiwemo hifadhi ndogo ya wanyama kama simba na chui.