Samia atajwa mwelekeo Dira 2050 na ubia sekta binafsi

Dar es Salaam. Rais, Samia Suluhu Hassan amepongezwa kwa Dira ya 2050, ikielezwa kuwa ni ya kitaifa huku wito ukitolewa wa kuhakikisha uhusiano baina ya serikali na sekta binafsi unaimarishwa zaidi ili kujenga uchumi jumuishi.

Pongezi na wito huo umetolewa kama sehemu ya maazimio ya Kongamano la Uchumi Jumuishi lililoandaliwa na Kigoda cha Mwalimu Nyerere na kufanyika katika Chuo Kikuu cha Mzumbe jijini Mbeya.

Mwenyekiti wa Kongamano hilo, Profesa Alexander Makulilo ambaye pia ni Mgoda wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere cha Masuala ya Umajumui wa Afrika, amewaambia washiriki kuwa Dira 2025 imehusisha maoni mengi ya Watanzania na imeakisi mahitaji na matarajio yao.

“Dira 2025 ina sifa zote za kuitwa Dira ya Taifa na si ya chama au serikali. Hii ni kwa sababu imeandaliwa baada ya kupata maoni ya Watanzania na ukiitazama inaakisi mahitaji na ndoto zetu kama taifa. Hili ni jambo zuri ambalo serikali ya Rais Samia imewafanyia Watanzania,” amesema Makulilo.

Mojawapo ya masuala yaliyoibuliwa katika azimio la washiriki ni suala zima la serikali kuweka nguvu zaidi katika uchumi jumuishi ili kunufaisha sehemu kubwa ya Watanzania.

Akitoa mada kuhusu hilo, mmoja wa wasomi maarufu wa masuala ya uchumi nchini, Profesa Humphrey Moshi ambaye pia alishiriki kwenye kuandaa Dira ya 2025 iliyomaliza muda wake, amesema jambo la muhimu ambalo serikali inatakiwa kufanya sasa ni kuhakikisha kilimo kinapewa nafasi kubwa katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania.

“Tunapozungumzia uchumi jumuishi maana yake ni ule uchumi ambao unagusa watu wengi zaidi katika taifa. Kwa sasa, kilimo kinategemewa na asilimia 64 ya Watanzania, hivyo uchumi jumuishi maana yake ni lazima uguse hawa walio wengi,” amesema.

Akizungumza katika kongamano hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi (PPPC), David Kafulila amesema ushirikiano imara baina ya serikali na sekta binafsi ni mojawapo ya nguzo muhimu za Dira 2025.

Akizungumza kwa kutoa mifano na takwimu, Kafulila amesema ubia baina ya serikali na sekta binafsi unaisaidia serikali kuwekeza kwenye masuala muhimu kama afya, elimu na miundombinu kwa vile sekta binafsi itatumia fedha zake kuwekeza kwenye miradi yenye faida kibiashara.

“Dhana nzima ya PPP kwa maana ya ushirikiano baina ya serikali na sekta binafsi ni kwamba sote tunakuwa wabia katika maendeleo ya nchi yetu. Lakini kubwa zaidi serikali haitalazimika kuwekeza kila mahali kwa sababu sekta binafsi itaweza kufanya hivyo,’’ amesema Kafulila.

Akitoa maelezo zaidi, Kafulila amesema ili uchumi uwe wa watu wengi, lazima ufuate sekta ambazo zimebeba watu wengi.

“Ripoti ya siku nyingi kidogo kutoka miaka ya 2008 inasema kwamba ukikuza uchumi kati ya asilimia nane mpaka kumi kwa miaka mitatu mfululizo, utapunguza umasikini kwa asilimia 50,” amesema Kafulila.

Kongamano hilo lilihudhuriwa na watu wa kada tofauti na mojawapo ya maazimio ilikuwa ni kumpongeza Rais Samia kwa kulinda amani na utulivu nchini kwa sababu nao ni sehemu ya kigezo cha kufanikiwa kutimiza ndoto.