Unguja. Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha ACT – Wazalendo, Othman Masoud Othman ameahidi kuirejesha ardhi yote iliyokwapuliwa kwa wananchi wa Wazanziba kinyume cha utaratibu.
Amesisitiza kuirejesha ardhi hiyo akilenga itumike katika masuala mbalimbali yakiwemo ya maendeleo, akisema tangu ashike wadhifa wa Umakamu wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, amekuwa akipokea malalamiko kuhusu ardhi.
Othman ameyasema hayo leo Jumapili Septemba 21, 2025 akizungumza katika mkutano wa hadhara wa kampeni uliofanyika katika Jimbo la Kijini Mkoa wa Kaskazini Unguja, katika mwendelezo wa kusaka kura.

“Niwaahidi, nachukua ahadi mbele yenu, nachukua ahadi hapa niliposimama mbele ya Mungu ambaye anashuhudia dhamira yangu kwamba hili naweza kulifanya kwa sababu ni haki yenu.”
“Kama ni uwekezaji, tunataka tuwekeze kila mahali, hatutaki kuishi? Nchi iwe ya uwekezaji tu? ACT – Wazalendo inasema Serikali itakayoiunda ndio itatengea maeneo ya uwekezaji,” amesema Othman.
Amedai kuwa Oktoba 29, 2025 CCM wanamaliza msimu na Wazanzibari wataanza msimu mpya chini ya uongozi wa ACT – Wazalendo itakayoboresha maisha yao.
Mbali na hilo, Othman amesema kama mwananchi ana ardhi yake Serikali haitamny’ang’anya ili kukodishwa bali itaweka mazingira mazuri ya kuwakutanisha wananchi na wawekezaji kwa ajili ya mchakato huo.
“Serikali itachukua asilimia fulani baada ya mwananchi kukodisha ardhi yake. Mfano umekodisha kwa Dola za Marekani 100,000, Serikali itachukua Dola 30,000 kama sehemu ya kodi ya ardhi,” amesema Othman.
Amefafanua kuwa Serikali ya ACT – Wazalendo itahakikisha ardhi ni mali ya mwananchi ili wanufaishe na Serikali itapata kodi kutokana na kipato chako.
“Changamoto ya ardhi Oktoba ndio mwisho, labda muwe hamtaki,” ameeleza.
Makamu Mwenyekiti wa ACT – Wazalendo (Zanzibar), Ismail Jussa amesema kila mkutano wa hadhara wa kampeni watakaoufanya wataeleza kasoro mbalimbali zilizojitokeza katika Serikali ili Wazanzibari kufanya uamuzi sahihi.
Awali, Mwenyekiti mstaafu wa ACT – Wazalendo, Juma Duni Haji maarufu ‘Babu Duni’ amedai kuwa wananchi wa Kijini na Matemwe wana madai ya kulalamikia kuhusu kunyang’anywa ardhi yao wanaoitumia kwa ajili ya kilimo.
“Watu wamekusudiwa kunyanga’anywa ardhi, dunia kote ardhi ndio uhai, sasa mnapokwenda kupiga kura, mjue mnakwenda kupigia hatima ya kizazi kijacho kinachotutegemea sisi. Mkifanya masihara hatutoboi, tutamalizwa safari hii,” amesema Babu Duni nakuongeza;
“Sasa mnapokwenda kupiga kura ukipata karatasi ya kura jiulize mara mbili kuhusu masuala yanayohusu maisha yako kufanya uamuzi,” amesema Babu Duni.
Babu Duni ambaye ni mjumbe wa kamati kuu ya ACT – Wazalendo, amewataka wananchi wa mkoa wa Kaskazini wanapoenda kupiga kura Oktoba 29, kuzingatia matatizo yanayowakabili kabla ya kufanya uamuzi wa kuchagua viongozi.
Katibu wa Habari, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma wa ACT – Wazalendo, Salim Biman amesema wana kila sababu ya kushinda jimbo hilo, kwa sababu wagombea wa chama hicho wa uwakilishi na ubunge wanakubalika.