Bilionea Mtanzania akumbana na kikwazo ununuzi wa kampuni Kenya

Nairobi. Bunge la Kenya wiki iliyopita limeelekeza kampuni ya East African Portland Cement (EAPC), kufuata mpango wa kununua tena hisa za asilimia 29.2 zinazomilikiwa na kampuni ya Uswisi, hatua ambayo inaonekana inaweza kuathiri mauzo ya hisa hizo kwa bilionea wa Tanzania.

Mpango wa kuuza hisa za EAPC kwa mwekezaji wa Tanzania, Edhah Abdallah Munif, umeibua wasiwasi kwenye bunge la Kenya kuhusu bei ya punguzo, ambayo ni nusu ya thamani ya hisa za kampuni ya saruji.

Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Biashara, Viwanda na Ushirika sasa wanataka EAPC inunue hisa hizo kwa thamani ya soko kisha ziuzwe kwa faida baadaye.

Iwapo EAPC itakubali mpango huo, itakuwa kampuni ya tatu kwenye Soko la Hisa la Nairobi (NSE) kufuata mpango wa kununua tena hisa, baada ya Nation Media Group mwaka 2021 na Centum mwaka 2023.

Hii inafuata mabadiliko ya sheria ya kampuni ya 2015 yaliyoruhusu kampuni kununua hisa zao wenyewe.

Upinzani wa Bunge juu ya hisa za EAPC unaweza pia kuathiri mpango ambapo wawekezaji wa Tanzania wamekubaliana na kampuni ya Uswisi, Holcim, kununua hisa hizo.

Wabunge wamehoji kwa nini hisa za kampuni yenye mali nyingi zinauzwa kwa bei isiyoakisi thamani ya kitabu ya Ksh20.4 bilioni (sawa na Sh390 bilioni) na thamani ya soko.

Munif ananunua hisa milioni 26.32   kutoka Holcim kupitia kampuni ya uwekezaji ya Kalahari Cement kwa Ksh27.30 kila moja (sawa na Sh523.06), ikikadiria mpango huo kufikia Ksh718.7 milioni (sawa na Sh13.7 bilioni).

Hisa za Portland Cement ziliisha biashara jana kwa Ksh56 kila moja, zikikadiria thamani ya soko ya kampuni hiyo ya Ksh5 bilioni (sawa na Sh95.7 bilioni).

Wajumbe wa kamati ya bunge wanashuku kuwa kampuni inayopata hisa hizo inalenga mali za EAPC, hususan ardhi yenye thamani ya zaidi ya Ksh20 bilioni ambayo ni sawa na Sh383.1 bilioni.

EAPC itahitaji Ksh1.4 bilioni (Sh26.8 bilioni) kwa bei ya sasa ya hisa kufanikisha mpango wa kununua tena.

“Kwa nini mnangojea hisa ziuzwe? Kwa nini msinunue sasa?” alihoji Mbunge wa Kajiado Kusini, Samuel Parashina.

Portland Cement inapaswa kupata idhini kutoka Mamlaka ya Masoko ya Mitaji nchini Kenya (CMA) kwa mpango wa kununua tena, ambao mara nyingi unafadhiliwa na faida zinazogawika.

Bei ya juu ya kununua tena hisa ni asilimia 10 ya wastani wa bei mwezi mmoja, na chini ni bei ya sasa kwenye NSE.

Mkurugenzi Mtendaji wa EAPC, Mohammed Osman, amesema kampuni itafuata mpango wa kununua tena hisa ikiwa Bunge litaidhinisha. “Holcim inatoka katika eneo la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara na tunazingatia kununua tena hisa. Tuna uwezo wa kulipa na kuondoa wanahisa wadogo.”

Sheria zinahitaji hisa zilizopatikana kwa kununua tena zifutwe, ziuzwe baadaye, au ziwe chini ya mpango wa umiliki wa hisa kwa wafanyakazi.

Kwa mwaka uliopita, bei ya hisa za EAPC imeongezeka kwa asilimia 359 kutoka Ksh7.2 kila moja, ikifanya iwe moja ya hisa zinazofanya vizuri soko.

Kwa bei ya sasa, thamani ya soko ya kampuni ni Ksh5.55 bilioni (Sh106.3 bilioni), huku bei ya kununua ya Kalahari Cement ikikadiria Ksh2.46 bilioni (Sh471.3 bilioni).

Hii inaonyesha kuwa Kalahari Cement inapata hisa hizo kwa bei nafuu, huku kampuni bado ikipungukiwa thamani kwenye NSE.

Kiasi kikubwa cha mali za kampuni Ksh21.23 bilioni (Sh406.7 bilioni) ni mali za uwekezaji, hasa ardhi ya umiliki wa kudumu (ekari 4,626) chini ya mikataba ya muda mrefu ya upangaji. Kupungukiwa kwa thamani sokoni pia kunaashiria kuwa wawekezaji wamelizingatia uhai usio rahisi wa ardhi nyingi za kampuni.

Kampuni ilipanga kuuza sehemu ya ardhi zake kubwa kupata Ksh10 bilioni kwa ajili ya mtaji wa biashara, baada ya kushinda kesi mahakamani mwaka 2023 dhidi ya wakazi waliokuwa wamekalia ardhi hiyo kwa takribani miaka 10.

Wajumbe wa kamati ya bunge waliwasiliana na Mamlaka ya Ushindani Kenya (CAK) na CMA kupinga bei ya ofa, wakidai kuwa mpango huo unaweza usiwe katika masilahi ya umma kwa muda mrefu.

Serikali na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) wana hisa ya jumla ya asilimia 52 katika EAPC.

Mkurugenzi Mtendaji wa CMA, Wyckliffe Shamiah, alisema kuwa mamlaka haikuwa na nguvu ya kuamua bei ya ofa, akibainisha kuwa inakidhi makubaliano kati ya mnunuzi na muuzaji.

Mpango huu unajiri miezi michache baada ya kampuni ya Munif, Amsons Group, kukamilisha ununuzi wa Bamburi Cement Desemba mwaka jana kwa Ksh23.6 bilioni (Sh452.1 bilioni), kuimarisha nafasi yake katika soko la saruji la Kenya.

Kwa kuwa Bamburi Cement tayari inamiliki asilimia 12.5 ya EAPC, Munif atakuwa mnunuzi mkubwa zaidi akiwa na hisa asilimia 41.75. (Chanzo cha habari hii ni gazeti la Business Daily)