SIKU 443 sawa na miezi 14 au wiki 63 tangu kocha Fadlu Davids aanze kuinoa Simba iliyomuajiri Julai 5, 2024 imedaiwa amegoma kusalia kikosini na kuamua kutimkia Raja Casablanca ya Morocco.
Mwanaspoti iliyokuwa ya kwanza kueleza kwamba huenda Fadlu asingerudi na timu hiyo nchini, hali imethibitika kwa kutoambatana na msafara wa kikosi hicho kilichokuwa Botswana.
Kukosekana kwa Fadlu sambamba na wasaidizi wake alioingia nao Msimbazi, imeongeza nguvu tetesi kwamba ameamua kurejea Raja baada ya kuchomoa maombi ya mabosi wa Simba kuendelea kusalia kikosini.
Kocha huyo ambaye aliongeza mkataba wa mwaka mmoja mwanzoni mwa msimu huu ili kuendelea kuinoa timu hiyo inaelezwa ameunganisha kwenda Morocco baada ya awali kuomba kuondoka mara baada ya Dabi ya Kariakoo Septemba 16, lakini aliombwa aiongoze Simba dhidi ya Gaborone United katika mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo ilishinda 1-0.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba kimeliambia Mwanaspoti, Fadlu hatakuwa sehemu ya kikosi hicho ndio maana timu imewasili jijini Dar es Salaam bila ya kocha huyo raia wa Afrika Kusini.
“Ni kweli kocha hatujarudi naye na huenda asiwe sehemu ya benchi letu la ufundi na muda wowote uongozi utatoa taarifa kwani yeye kaelekea Afrika Kusini.”
Fadlu sasa anatarajiwa kuchukua mikoba ya kuinoa Raja Club Athletic ambayo hivi karibuni imetoka kuachana na aliyekuwa kocha wao Lassaad Chabbi kwa makubaliano ya pande zote mbili.
Inaelezwa makubaliano ya pande zote mbili Simba na Fadlu yamekamilika na kocha huyo anarejea katika klabu aliyowahi kuitumikia kama kocha msaidizi, ambapo walitwaa Botola Pro bila kupoteza mchezo wowote msimu mzima.
Wakubwa hao wa Morocco wamepania kurejea kileleni, hususani katika mashindano ya CAF, na wamemhakikishia Fadlu pamoja na benchi lake la ufundi.
Chabbi akiwa na Raja katika mechi mbili msimu huu mpya wa Botola Pro, kovha huyo alikusanya pointi 4 na kukaa nafasi ya 3 katika msimamo wa Ligi.