Kocha Yanga ana dakika 270 ngumu

YANGA tayari ipo jijini Dar es Salaam na kesho Jumatatu inaanza rasmi mazoezi kwa ajili ya mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Pamba Jiji itakayopigwa keshokutwa, Jumatano, huku benchi na ufundi na mastaa wa timu hiyo wakiwa na dakika 270 ngumu ili kufunga hesabu za mwezi huu.

Wababe hao wa soka nchini, walikuwa Luanda, Angola kucheza mechi ya mkondo wa kwanza ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wiliete Benguela Ijumaa iliyopita na kupata ushindi wa mabao 3-0 na kurejea juzi na leo itaanza maandalizi ya Ligi Kuu.

Mechi hiyo ya kwanza kwa watetezi hao itapigwa jijini Dar es Salaam, huku ikiwa na rekodi tamu msimu uliopita baada ya kupata ushindi mechi zote mbili ikianza na ushindi wa 4-0 nyumbani na kushinda 3-0 ugenini na kuvuna jumla ya mabao saba na pointi sita.

Pambano hilo itakuwa ni mtihani wa kwanza kwa Kocha Romain Folz katika ligi kuu dhidi ya timu inayoonekana kuimarika ikiwa chini ya Kocha Mkenya, Francis Baraza aliyeanza na sare ya 1-1 ugenini dhidi ya Namungo katikati ya wiki iliyopita.

Yanga ambayo haijaruhusu bao lolote katika mechi za mashindano chini ya Folz ikiwamo kushinda 1-0 Ngao ya Jamii dhidi ya Simba na kisha kuitambia Wiliete mabao 3-0 mara baada ya mechi hiyo ya Ligi Kuu, itakuwa na saa 72 tu kujipanga kabla ya kurudiana na timu hiyo ya Angola.

Ndiyo, mechi hiyo ya marudiano ya CAF imepangwa kupigwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na Yanga itakuwa na kazi ya kulinda ushindi iliyopata ugenini ili kujiweka pazuri kutinga raundi ya pili na kusubiri mshindi kati ya Elgeco Plus ya Madagascar au Silver Striker ya Malawi.

Kutoka mechi ya keshokutwa ya ligi dhidi ya Pamba Jiji, wawakilishi hao wa Tanzania watakuwa na siku mbili za Alhamisi na Ijumaa kabla ya kushuka uwanjani tena kupambana na Wiliete ambayo katika mechi ya Ijumaa ikiwa kwao, ilicheza vizuri kuliko Yanga, licha ya kupoteza 3-0.

Hii ikiwa na maana Kocha Folz na mastaa wa Yanga watamaliza na Pamba kisha kuanza haraka hesabu za kuing’oa Wiliete katika mechi hiyo ya marudiano, licha ya ushindi mnono wa mabao 3-0 yaliyofungwa na Aziz Andabwile, Edmund John na Prince Dube.

Msimu uliopita Yanga iliishia makundi ya michuano hiyo baada ya kuvuna pointi nane ikiwamo ile ya sare ya 1-1 dhidi ya MC Alger ya Algeria iliyoizuia kwenda robo fainali kwa mara ya pili mfululizo kwa tofauti ya alama moja tu na wababe hao wa Algeria iliyomaliza na pointi tisa ikiwa nafasi ya pili nyuma ya Al Hilal iliyokuwa chini ya Florent Ibenge iliyoongoza Kundi A.

Mara baada ya mechi hiyo ya marudiano ya CAF, Yanga itasafiri hadi Mbeya kukabiliana na Mbeya City, mechi iliyopangwa kupigwa siku tatu baadae, yaani Septemba 30 kumalizia kibarua kigumu alichokuwa nacho Folz mwezi huu. Hizo zitakuwa dakika nyingine 90 ngumu kwa Yanga.

Kocha huyo aliyetua hivi karibuni kutoka Afrika Kusini, ameshamaliza mechi tatu ngumu alizokuwa nazo kati ya sita za Septemba, ikiwamo ile ya Tamasha la Wiki ya Mwananchi dhidi ya Bandari Kenya na Ngao ya Jamii ambazo zote ilishinda kwa bao 1-0 mtawalia kisha kuizamisha Wiliete.

Hivyo Folz ana kibarua kwa dakika 90 za kwanza dhidi ya Pamba Jiji, kisha kuzikabilia dakika 90 nyingine mbele ya Wiliete na kuufunga Septemba na dakika 90 za ugenini jijini Mbeya na kama atatoboa kote salama, atazima kelele na lawama za mashabiki juu ya timu kutocheza vyema.

Kocha huyo alinukuliwa mara baada ya pambano la ugenini la CAF, timu imeshinda lakini haikucheza vyema alivyotarajia na wanarudi uwanja wa mazoezi ili kujiweka fiti kwa ratiba inayomkabili akiamini kila kitu kitakaa sawa na kuwapa furaha Wanayanga.

Folz ambaye ni raia wa Ufaransa anajua wazi mashabiki wa Yanga wanataka kuiona timu hiyo ikifika mbali katika Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya misimu miwili iliyopita kucheza robo fainali ikiwa chini ya Miguel Gamondi aliyeiingiza makundi pia msimu uliopita kabla ya kutimuliwa.

Gamondi kwa sasa yupo Singida Black Stars inayoshiriki Kombe la Shirikisho Afrika iliyoanza na ushindi wa 1-0 ugenini dhidi ya Rayon Sport ya Rwanda iliyochezea 3-1 katika mechi ya kirafiki ya kimataifa mbele ya Yanga hivi karibuni. Gamondi tayari ameshaipa Singida Kombe la Kagame.

Katika mechi nane za kwanza za Ligi Kuu Bara msimu uliopita, Yanga ikiwa na Gamondi ilishinda zote bila kuruhusu bao kabla ya Azam kuwatibulia kwa kuichapa 1-0 na kufuiatiwa na Tabora United (sasa TRA United) iliyoshinda 3-1 na kumng’oa kocha huyo Jangwani.