Dar es Salaam. Hatua ya Serikali kuvunja kituo cha daladala cha Kwamama Kibonge, kilichopo eneo la Buza jijini Dar es Salaam imeendelea kuzua mvutano mkubwa kati ya wananchi na mamlaka husika.
Wananchi, madereva na wafanyabiashara wadogo waliozungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti wanasema, uamuzi huo umewaongezea gharama na usumbufu, huku Serikali ikisisitiza kuwa, lengo ni kuimarisha usalama na kurahisisha usafiri kupitia stendi mpya iliyojengwa umbali wa takribani mita 500 kutoka ilipokuwapo ya awali.
Tangu Julai mwaka huu Serikali ilipoanza kutekeleza uamuzi huo, abiria wameendelea kufurika eneo hilo wakisubiri usafiri licha ya marufuku ya askari wa usalama barabarani. Askari hao wameimarisha doria, wakitawanya abiria wanaosubiri usafiri eneo hilo huku wakizuia daladala zote zinazopakia na kushusha abiria katika eneo hilo.
Hata hivyo, madereva wa magari ya abiria, bajaji na bodaboda wameendelea kushusha na kupakia huku wakiwakwepa askari hao.

Lakini pia wafanyabiashara wadogo wakiwamo wa vyakula, matunda na mbogamboga nao wanaendelea na biashara kando ya kituo hicho.
Mwananchi lilishuhudia hali hiyo leo Jumapili, Septemba 21, 2025, msongamano wa abiria na magari ulikuwa mkubwa huku askari wakielekeza magari na abiria kutotumia eneo hilo kwa kuwa si kituo rasmi.
Wananchi wameendelea kupinga agizo la kufungwa kwa kituo hicho wakisema kipo katikati ya makazi yao na kimekuwa msaada mkubwa wa safari zao za kila siku.
Asha Balozi ameiambia Mwananchi kuwa stendi mpya imejengwa mbali na makazi yao, hivyo wanalazimika kupanda pikipiki au kutembea umbali mrefu.
“Ukitoka Mashine ya Maji, kushushwa kule stendi mpya inalazimu ulipie pikipiki kurudi tena huku nyumbani. Hiyo ni gharama isiyo ya lazima ambayo wengi hatuimudu,” amesema mmoja wa abiria aliyeomba hifadhi ya jina lake.
Akiwazungumzia wagonjwa, wazee na wanafunzi amesema; “Mfano nikiwa na mgonjwa au mzee, akishushwa kule stendi mpya anawezaje kutembea umbali huu mrefu kurudi huku Kwamama Kibonge?.
Aidha, wafanyabiashara wadogo waliokuwa wakitegemea kituo hicho wamesema maisha yao yameathirika kutokana na kupungua kwa wateja.
“Daladala zikishusha abiria hapa wateja walikuwa wengi. Lakini sasa hivi watu wachache wanafika kwa sababu kushuka hapa kunahitaji kuviziana na askari,” amesema mfanyabiashara wa samaki wa kukaanga, Yusuph Kashindye.
Madereva wa daladala na bajaji pia wameungana na wananchi kulalamikia hali hiyo, wakieleza kuwa abiria wengi wanakataa kushushwa katika stendi mpya kwa sababu inawalazimu wapite maeneo ya makazi yao na baadaye kutafuta usafiri mwingine au kutembea kwa miguu kurudi nyumbani.

“Kama dereva nikisema niwashushe abiria stendi mpya, wananisusia. Wanataka kushuka hapa na wengi wanaishi maeneo haya ya karibu. Mimi naona Serikali iwasikilize, kituo hiki kiendelee kutoa huduma,” amesema dereva mmoja alipokuwa akishusha abiria eneo hilo.
Kwa upande wao, waendesha bajaji wamesema idadi ya wateja imepungua kwa kiasi kikubwa. “Tulikuwa tunapata wateja wengi kutoka kituo hiki, lakini sasa hivi tunabaki kupaki tu. Unaona bajaji zimejaa hapa, lakini abiria hakuna,” amesema Ramadhan Ally, dereva bajaji anayesafirisha abiria kati ya Buza na Chamazi.
Kauli za viongozi wa mtaa
“Kituo hiki kipo katikati ya makazi ya watu, ni msaada mkubwa wa usafiri. Wananchi wetu wanaomba kisiondolewe, na sisi Serikali ya mtaa huu tunaungana nao tunashauri kituo kisivunjwe, kiendelee kuwepo,” amesema Mwenyekiti wa Mtaa wa Buza, Mohammed Mbagalo.
Ameongeza kuwa; “Wananchi hawatakiwi kufuata kituo, kituo ndicho kinachotakiwa kuwafuata wananchi ili wapate huduma.”
Hivyo, amependekeza suluhu ipatikane kwa kupanga upya eneo hilo, ikiwamo kuweka sehemu ya kushushia abiria upande mmoja na kupandia mwingine badala ya kuondoa kituo kizima.
Akizungumzia sakata hilo, Meneja wa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura), Mkoa wa Dar es Salaam, Geoffrey Mkinga amesema suala hilo lipo chini ya Serikali ya Manispaa ya Temeke na tayari hatua zimeshachukuliwa.
“Suala linafanyiwa kazi na kamati maalumu iliyoundwa na DC wa Temeke. Wasiliana na ofisi ya Mkurugenzi,” amesema meneja huyo.
Akilizungumzia hilo Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke, Jomaary Satura amesisitiza msimamo wa Serikali ni kuvunja kituo hicho na kuwataka madereva daladala na abiria kuacha kukaidi maagizo ya Serikali ili kuepuka kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Kwamama Kibonge hakuna kituo. Ni kosa kushusha au kupakia watu hapo kwa kuwa siyo kituo,” amesema Satura.
Kuhusu stendi mpya, Satura amesema: “Serikali imetumia pesa nyingi za wananchi kujenga kituo hicho. Magari yote yaendelee kutumia stendi hiyo badala ya kuendekeza mvutano,” amesema.
Akitambua mvutano unaoendelea, Satura amesema Serikali imekuwa ikipokea malalamiko ya wananchi na kuyashughulikia kupitia vikao vinavyoitishwa na Mkuu wa Wilaya ya Temeke, lakini msimamo rasmi unabaki kuwa kituo cha Kwamama Kibonge kimefungwa.

Wafanyabiashara wadogo wakiendelea na biashara zao Kwamama Kibonge, usiku na mchana.
“Malalamiko yamekuwepo na yamekuwa yakishughulikiwa na Mheshimiwa DC. Vikao vingi vimefanyika kwa kuwasikiliza wote wanaolalamika na Serikali kuchukua hatua. Hadi sasa maamuzi yaliyopo ndiyo hayo, sidhani kama kuna mengine zaidi ya hayo,” amesema.
Mvutano kuhusu kituo cha Kwamama Kibonge unaibua kumbukumbu ya migogoro ya vituo vya magari katika Wilaya ya Temeke, ambayo imekuwa ikijirudia mara kwa mara.
Mfano ni stendi ya Kijichi iliyozinduliwa Oktoba 17, 2022, baada ya kugharimu Sh3.4 bilioni chini ya mradi wa DMDP.
Malengo yake yalikuwa kuhudumia mabasi ya mikoa ya Kusini, lakini ndani ya siku mbili tu baada ya kuzinduliwa, malalamiko yalizuka.
Madereva na abiria walilalamika kuwa eneo hilo liko mbali na halikuwa rahisi kufikika, hali iliyosababisha mabasi yote kurejea katika kituo cha zamani cha Mbagala Rangi Tatu, na hivyo Kijichi kubaki bila basi hata moja.
Mvutano huo ulimlazimu Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuingilia kati na kuagiza ujenzi wa stendi mpya ya Temeke Sudan uharakishwe, baada ya kushindikana kwa mradi wa Kijichi.
Wamiliki wa mabasi kupitia Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa) walilalamika wakati huo kuwa hawakushirikishwa katika mchakato wa kuhamishwa, wakisema mara nyingi ushauri wao kuhusu maeneo bora ya kujenga stendi hupuuziwa.
Wito wa ushirikishwaji wadau
Mchambuzi wa masuala ya uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Abel Kinyondo amesema mamlaka hazina budi kushirikisha wananchi moja kwa moja katika miradi inayogusa maisha yao ili kuhakikisha inakuwa na tija.
Amesema kukosekana kwa ushirikishwaji kunasababisha serikali kutumia nguvu kuwalazimisha wananchi kutumia huduma ambazo mara nyingi walengwa wenyewe hawajamiliki.
“Tuna miradi mingi nchini, ikiwemo masoko na vituo vya daladala, ambayo imejengwa lakini imebaki wazi kutokana na kukosekana kwa ushirikishwaji. Watumiaji wanaposhirikishwa mapema, wanamiliki mradi huo na hutumia huduma kwa hiari. Bila hivyo, tunaendelea kujenga miradi mikubwa isiyo na matumizi ambayo inagharimu maendeleo ya sekta nyingine na kupoteza fedha za Serikali,” amesema Profesa Kinyondo.