Arusha. Mgombea urais wa Chama cha The United People’s Democratic Party (UPDP), Twalib Kadege amesema wakishinda uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, jembe la mkono litakuwa mwisho kutumika kwa kuwa, watanunua matrekta milioni 400 yatakayosambazwa kote nchini kwa ajili ya kilimo cha kisasa.
Aidha, ameahidi kutafuta suluhu ya kudumu ya kuondoa migogoro ya wakulima na wafugaji kwa kutenga maeneo maalumu ambayo hayatakuwa na mwingiliano; kutakuwa na kanda maalumu kwa ajili ya wafugaji ambao watatengenezewa miundombinu muhimu ikiwemo majosho.
Kadege amebainisha hayo kwenye mkutano wake wa kampeni leo Jumapili Septemba 21, 2025 uliofanyika eneo la kituo kikuu cha mabasi Arusha.
Amesema ilani ya chama hicho imelenga kuwainua Watanzania kiuchumi ikiwamo wakulima kuondokana na kilimo cha jembe la mkono.
Amesema chama hicho kikishinda uchaguzi huo watahakikisha Watanzania wanaondokana na jembe la mkono na kununua trekta hizo zitakazosambazwa nchi nzima na kuwatafutia wakulima masoko ndani na nje ya nchi.
“Jembe la mkono mwisho,kupinda mgongo mwisho, tutaleta matrekta milioni 400 yalimie wananchi mashamba,” amesema mgombea huyo.
Kuhusu migogoro kati ya wakulima na wafugaji, amesema ilani ya chama hicho imekuja na suluhu ambapo wataweka kanda maalumu ya wafugaji mbali kabisa na wakulima na wa watawatengenezea mazingira mazuri.
“Tutawajengea mabwawa maeneo ya majosho, madaktari na kanda hiyo haitaingiliwa na mkulima kusumbua mfugaji hata kuwe na rutuba ya aina gani hilo litakuwa eneo la wafugaji tu na hakuna atakayeingia ili mfugaji aweze kuwa huru na mifugo yake.
“Wakulima nao watakuwa wanakaa mbali na wafugaji, suluhu hii itakuwa na sheria na watapeleka muswada bungeni ili mfugaji akiingiza mifugo kwenye shamba la mkulima, Serikali italipa, hatalipa yeye ila atapelekwa mahakamani na sheria itatungwa afilisiwe na jela aende kwa kuharibu mazao ya mkulima naamini itakomesha na mkulima vilevile akifanya, hivyo adhabu itachukuliwa dhidi yake,” amesema.
Kuhusu makundi mengine, mgombea huyo ameahidi kuwajengea wazee wote ambao hawana nyumba kuwajengea na kuwapa fedha za kujikimu Sh500,000 kila mwezi.
“Tunataka kutengeneza Serikali itakayokuwa kimbilio la wananchi. Kwa wazee tutatoa Sh500,000 kila mwezi, ilani yetu ndiyo inasema hivyo na wazee wasio na nyumba tutawajengea nyumba ili waishi vizuri kama Watanzania wengine, wasikae barabarani kuombaomba,” amesema.
Kwa upande wake, mgombea urais wa UPDP Zanzibar, Hamad Mohamed Ibrahim amewataka Watanzania kulinda amani iliyopo huku akisisitiza umuhimu wa Muungano.
Amesema chama hicho kitahakikisha Mkoa wa Arusha unazidi kukua kutokana na sekta ya utalii pamoja na uboreshaji wa miundombinu.
“Tunatakiwa tuwe waaminifu, wazalendo kwa Taifa letu, tuipende amani na tusisahau Muungano unakuza uzalendo. Asitokee mtu yeyote au mgombea kutoka chama chochote kunadi shari mbele yenu au anayetoa maelekezo yanayoweza kusababisha vurugu.
“Huyo si mwenzetu, niwaombe sana wanaokuja kwenu kuleta maneno ya shari hao hawana masilahi na Taifa, msiwaamini, kuwapokea au kuwakubali, kura yako ina thamani usipopiga kura umekosa haki yako ya msingi,” amesisitiza.
Kuhusu vijana, amesema chama hicho kitajenga viwanda kwa ajili ya kuwawezesha vijana kupata ajira pamoja na kulipia mahari vijana wote.
“Kijana yoyote ambaye hajaoa Tanzania, UPDP itamlipia mahari kwa kijana yeyote ambaye atasikia tangazo UPDP imeingia Ikulu, aje tutamlipia mahari. Hatutaishia hapo, wake zao waliowachumbia nao watapewa mitaji ya Sh5 milioni kwa ajili ya kulinda… vijana upweke haupo tena,” amesema.