Chaumma kuja na viwanda vya nyama, kurasimisha ufugaji

Arusha. Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), kimeahidi kurasimisha sekta ya ufugaji, kuanzisha viwanda vya kuchakata nyama sambamba na kuwapatia wafugaji na wakulima ardhi mkoani Arusha.

Katika hilo, chama hicho kimewatahadharisha wale wote wanaohodhi ardhi kikisema kikiingia madarakani kitawapatia ardhi hiyo wenye uhitaji.

Kauli hiyo imetolewa leo Septemba 21, 2025na mgombea mwenza wa urais, Devota Minja wakati akihutubia wananchi wa jimbo la Arumeru Magharibi na Kisongo, mkoani Arusha.

Akiwa ameambatana na mgombea ubunge wa jimbo la Arumeru Magharibi katika Kata ya Olturumet, Minja amesema haiwezekani wafugaji na wakulima wateseka wakati ardhi bado ipo kubwa mkoani humo.

“Sekta ya mifugo tutairasimisha rasmi, tutahakikisha wafugaji wote wanapata ardhi, tuwe na malisho ya kutosha wafugaji walishe kuanzia Januari hadi Desemba.

“Tujenge viwanda mfugaji asiende mnadani akakutane na walanguzi, Chaumma hatutaki muendelee kunyonywa,” ameahidi Minja.

Uanzishwaji wa viwanda hivyo umetajwa kutachochea ajira kwa watu wa eneo hilo, kuchochea biashara ya ndani na nje ya nchi hali itakayoongeza mapato ya mtu mmoja mmoja na Serikali kwa ujumla.

Aidha, Chama hicho kimesema kitaimarisha shughuli za kifugaji sambamba na kuongeza upatikanaji wa maziwa.

Chaumma kinaahidi hayo wakati kampeni za uraisi, wabunge na madiwani zinaendelea kuchanja mbuga kote nchini kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatano Oktoba 29, mwaka huu.

“Nyama hizo zitakazochakatwa zitasafirishwa hadi nje ya nchi. Kwa wakulima nao tutakuwa na viwanda vya kuzalisha mbolea ili waipate kwa urahisi,” amesema.

Akizungumzia kuhusu fursa zilizopo mkoani  Arusha, mgombea mwenza huyo amesema utalii unaingiza fedha nyingi, hivyo hakuna sababu ya wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo kutozwa ushuru.

Akitolea mfano, amesema soko la Ngaramtoni ni vigumu kuwa na vumbi akishangaa fedha zinazokusanywa zinakwenda wapi.

Amesema eneo hilo linapaswa kuwa lenye ubora ili kuchochea baishara.

Maneno hayo yanaungwa mkono na Mgombea Ubunge wa Jimbo hilo la Arumeru Magharibi, Nasinyari Mollel aliyesema soko hilo linapaswa kuboreshwa kakuwa ni tegemeo kwa watu wengi.

Nasinyari amedai kuchoshwa na shida za wakazi wa jimbo hilo, hivyo yuko tayari kuwatumikia huku akisema kwamba hilo litategemea kama watakiweka madarakani chama chao nay eye kupatiwa ridhaa ya kongoza jimbo hilo.

“Maji, vumbi, magari ya wagonjwa yote tutahakikisha vinapatikana endapo mkituchagua Chaumma chama chenye nia ya kumkomboa Mtanzania,” amesema.

Chama hicho kimesema changamoto zinazokabali Arusha kwa ujumla ikiwemo barabara, maji, kitazitatua mara baada ya kuingia madarakani.