CCM Mjini Magharibi yaahidi kuandika historia

Unguja. Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mjini Magharibi, Talib Ali Talib amesema mwaka huu utakuwa wa kihistoria kwa sababu utashuhudia kumalizika kwa upinzani Zanzibar, hatua itakayosaidia kuharakisha maendeleo ya nchi.

Akizungumza leo Jumapili Septemba 21, 2025, wakati wa uzinduzi wa kampeni za Jimbo la Kwahani, Talib amesema jimbo hilo litakuwa kitovu cha historia hiyo kwa kuwa ndilo ngome ya chama hicho na chuo cha waasisi na viongozi waliothibitisha maadili na weledi wao wa kiuongozi.

Akimtolea mfano Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ambaye ametokea jimbo hilo, Talib amesema ameacha alama kubwa ya uongozi kutokana na msingi na mafunzo aliyoyapata katika ngome hiyo.

“Hakuna haja ya kumchagua kiongozi mwingine zaidi yake. Wanachama wa CCM watalipa fadhila kwa kumpa kura za ndiyo ili aendelee kufanya vizuri zaidi,” amesema Talib.

Amesisitiza kuwa wanachama wa Kwahani hawataombwa kura bali watatoa kwa hiari kwa wagombea wote wa CCM, kwa sababu amesea; “sisi ndio watoto wa mapinduzi na tutaendeleza misingi hiyo.”

Aidha, amewahimiza wanachama na wapenzi wa chama hicho kumchagua pia mgombea ubunge na uwakilishi wa CCM ili kuongeza nguvu za mapinduzi na kumpa Dk Mwinyi nafasi ya kutekeleza vyema dira ya maendeleo.

Kwa upande wake, Mgombea Ubunge wa Kwahani, Mohamed Laki amesema CCM kinasimama kama familia moja na alama moja ya mshikamano, hivyo hakuna sababu ya vurugu.

Ameahidi kulitumikia jimbo hilo iwapo atapewa ridhaa Oktoba 29, 2025, kwa kushirikiana na mgombea mwenza wa uwakilishi.

Naye, Mgombea Uwakilishi, Mohammed Sijamini amesema atahakikisha ahadi zote za chama zinatekelezwa, ikiwamo ya ajira, mikopo na michezo.

Amewataka wafuasi wa CCM kumpigia kura za ndiyo ili kushinda kwa kishindo ifikapo Jumatano Oktoba 29, 2025.

Mgombea udiwani jimboni humo, Lutfia Juma Chaku ameahidi kuwa atahakikisha wadi yake inadumisha usafi na huduma bora endapo atapewa ridhaa.