Mbongo afichua mambo mawili Marekani

KINDA la Kitanzania anayekipiga SCCC FC Ligi ya Vijana Marekani, Lohanga Malenga amesema ni fursa kwake kupata mafunzo ya kitaaluma huku akiendelea kupata ujuzi wa soka.

Kiungo huyo ambaye ni mchezaji wa timu ya taifa chini ya miaka 19, alijiunga na timu hiyo akitokea akademi ya Villareal na alitwaa ubingwa wa Tri-State Cup mara mbili mfululizo.

Akizungumza na Mwanaspoti, Malenga alisema ingawa wanacheza kwa levo ya vijana lakini ni ligi ngumu Marekani na anazidi kupambania nafasi yake ili atimize malengo ya kuitwa timu ya taifa, Taifa Stars.

“Tofauti ni kiwango cha chuo ni kigumu zaidi na kinaweza kuleta changamoto mpya pamoja na fursa za kitaaluma. Akademi inalenga zaidi katika kukuza ujuzi wa mchezaji na uelewa wa kimbinu naamini nikiwa hapa nitaongeza kitu,” alisema Malenga na kuongeza

“Ndiyo maana nimechagua kuendelea na masomo yangu huku nikiendelea kucheza soka katika kiwango cha juu na hiyo ndiyo sababu iliyonifanya nijiunge na timu hiyo kwa sababu nafaidika na mambo yote.”

Asili ya kiungo huyo anatokea DRC Congo lakini alizaliwa Tanzania ambako alicheza soka tangu akiwa na miaka mitano lakini baadae alipata nafasi ya kujiunga na Villareal.

Katika ligi ya vijana anayoitumikia nyota huyo, kuna timu 219 za Division I katika National Junior College Athletic Association (NJCAA) zinazoshiriki kwenye kanda 24 tofauti.

Timu hizo zinatoa ufadhili wa michezo, unaojumuisha kiwango cha juu cha ada ya masomo, ada nyinginezo, malazi na chakula, vitabu vinavyohusu masomo hadi Dola 250 kwa vifaa vinavyohitajika kwenye masomo pamoja na gharama za usafiri mara moja kwa mwaka wa masomo kwenda na kutoka chuoni.