MSHAMBULIAJI wa Kitanzania, Yusuph Athuman hivi karibuni alitambulishwa kikosi cha Napsa Stars inayoshiriki Ligi Kuu Zambia na meneja wa mchezaji huyo akafichua jambo kuhusu usajili huo.
Kabla ya kutimkia Zambia msimu uliopita alisajiliwa na Yangon United inayoshiriki Ligi Kuu Myanmar kabla ya kurejea Tanzania na kumaliza mkataba wake na Fountain Gate ambako huko kote hakucheza.
Akizungumza na Mwanaspoti, Meneja wa mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga, Hon Simbeye alisema kulikuwa na ofa kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania lakini waliangalia uwezekano wa kucheza ndipo wakafanya maamuzi ya Zambia.
Simbeye ambaye pia anamsimamia beki wa Simba Alon Okechi aliyejiunga na Zanaco ya Zambia alisema kwa uwezo wa Athuman anaamini atapata nafasi ya kucheza na kuonyesha makali yake.
“Ninafanya kazi na wachezaji wengi hapo Bongo mmojawapo ni Athuman, tulikuwa na ofa nyingi lakini tulikaa na kuangalia wapi anaweza kucheza na kuonyesha kiwango chake ndipo akasaini Napsa Stars,” alisema Simbeye na kuongeza
“Ligi ya Zambia naifahamu vizuri kocha alihitaji mshambuliaji wa kati mwenye nguvu naamini kwa uwezo wa Athuman ataweza kucheza kwa sababu ana uzoefu kashacheza Yanga kwa kiwango kizuri.”
Ligi ya Zambia tayari imeshaanza zikipigwa raundi nne na chama la mshambuliaji huyo liko nafasi ya 16 kati ya 18 kwenye msimamo wa ligi, ikitoa sare mbili na kupoteza mbili.