SAMIA SUHULU HASSAN: Anapambania miaka mitano akijivunia minne aliyoongoza

Machi 17, 2021, usiku, aliyekuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, alitangaza kifo cha Rais John Pombe Magufuli. Kizunguzungu kilijiri kutoka kichwa hadi kichwa, wasiwasi mkubwa ukiwa kwenye swali, “nchi itavukaje?”

Rais kufikwa na mauti akiwa madarakani, lilikuwa tukio la kwanza kwa Tanzania. Katiba ya Tanzania, ibara ya 37 (5), inaeleza wazi kuwa, kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kikiwa wazi kutokana na kufariki dunia, kujiuzulu, kupoteza sifa za uchaguzi au kutomudu kazi zake kwa maradhi, Makamu wa Rais ataapishwa na atakuwa Rais kwa muda uliosalia.

Halafu Makamu wa Rais baada ya kuwa Rais, atateua Makamu wa Rais baada ya kushauriana na chama chake, kisha uteuzi huo utathibitishwa na Bunge.

Magufuli alifariki dunia. Makamu wa Rais alikuwepo, Samia. Kikatiba hakukuwa na kizungumkuti hata kidogo. Hata hivyo, kizunguzungu kilizaliwa kwa kutazama sifa za kimaumbile alizonazo Samia.

Ni mwanamke, halafu, Tanzania haikuwa imepata kuwa na Rais mwanamke. Hata Makamu wa Rais mwanamke, Samia ndiye wa kwanza.

Magufuli, kiongozi mwenye uthubutu mkubwa. Alianzisha miradi mikubwa na alifariki dunia ikiwa haijafika hata asilimia 50.

Ujenzi wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere (JNHPP) na Reli ya Standard Gauge (SGR), Daraja la Busisi. viulizo vyenye kuambatana na mashaka, vilielekezwa kwa Samia. Je, angeweza?

Machi 19, 2021, Samia alipokula kiapo kuongoza dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nchi ilikuwa ikisulubiwa kiuchumi.

Hali ya kisiasa ilikuwa mbaya. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Bara, Tundu Lissu aliyekuwa mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema na mbunge wa zamani, Jimbo la Nyamagana, Mwanza, Ezekia Wenje, walishahama nchi kabisa.

Kutoka Machi 19, 2021 hadi Mei 23, 2022, ni mwaka mmoja, miezi miwili na siku nne, jarida la Time la Marekani, lilimtaja Samia kuwa miongoni mwa watu 100 wenye ushawishi zaidi ulimwenguni.

Time iliandika: “Uongozi wake umekuwa ni chachandu (tonic).”

Januari 2, 2024, aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Alphayo Kidata, alitoa ripoti ya mapato yaliyokusanywa na mamlaka hiyo kwa nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2023-2024. Alisema Desemba 2023, TRA ilikusanya Sh2.77 trilioni, hizo ni fedha zilizoweka rekodi tangu kuanzishwa mamlaka hiyo mwaka 1995.

Bwawa la JNHPP, Samia alilikuta lipo asilimia 37. Hivi sasa limekamilika kwa asilimia 100. Reli ya Standard Gauge, imejengwa kwa kasi zaidi tangu alipoingia madarakani, sasa reli hiyo inajengwa kuelekea Kigoma.

Daraja la Busisi ni moja ya miradi iliyoutafsiri urais wa Magufuli. Alifariki dunia daraja likiwa chini ya asilimia 50. Sasa limekamilika kwa asilimia 100.

Benki ya Dunia (WB), Shirika la Fedha la Kimataifa (IFM) na Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB), kwa nyakati tofauti mwishoni mwa mwaka 2021 na mwanzoni mwa mwaka 2022, walimpongeza Samia kwa hatua zake za kuivusha nchi katika janga la Uviko -19.

Uamuzi wake wa kuruhusu chanjo, jumlisha hatua za kiuchumi alizozichukua, ziliwezesha kuirejesha nchi kwenye ukuaji chanya wa kiuchumi kutoka chini ya asilimia 4 mwaka 2021 hadi asilimia 4.6 mwaka 2022, kisha asilimia 5.5 mwaka 2025.

Ruhusa ya mikutano ya hadhara ya kisiasa, ambayo aliitoa Januari 3, 2023, ikiwa ni takriban miaka saba tangu ilipopigwa marufuku, ilimuonesha nia kiongozi wa aina gani.

Kuanzisha tume ya Haki Jinai, utambulisho wa 4R za demokrasia, ni mambo yanayotambulisha uongozi wa Samia.

Nyongeza ya posho za kujikimu kwa wanafunzi wa elimu ya juu, kufanya elimu kuwa bure mpaka kidato cha sita, ujenzi wa madarasa na shule mpya za msingi na sekondari kwa wingi zaidi ndani ya muda mfupi kupata kutokea. Kupandisha mishahara ya wafanyakazi na madaraja, baada ya kusimama kwa miaka saba, ujenzi wa barabara za mabasi ya mwendokasi kilometa nyingi zaidi kuliko alizozikuta, zilizojengwa na Rais wa Nne, Jakaya Kikwete.

Jumatano Januari 24, 2024, Chadema, kilifanya maandamano jijini Dar es Salaam. Chadema walifanikiwa kushawishi umati mkubwa kuingia barabarani kuandamana. IIlikuwa mara ya kwanza kwa chama cha upinzani Tanzania kukiri kufanya mazungumzo na Jeshi la Polisi, kisha kukubaliana kushirikiana kufanikisha maandamano ya amani.

Machi 8, 2023, Samia alikuwa mgeni rasmi kwenye kongamano la Siku ya Wanawake Duniani, lililoandaliwa na Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), ukumbi wa Kuringe, Moshi, Kilimanjaro.

Mei 31, 2022, Samia alikuwa mgeni rasmi kwenye sherehe za maadhimisho ya miaka 30 ya muziki ya mwana-Hip Hop, Sugu, zilizofanyika Serena Hotel, Dar es Salaam. Sugu ni kiongozi na mwanachama wa Chadema, ambaye alishakuwa mbunge kwa vipindi viwili, mwaka 2010-2015 na 2015-2020.

Januari 27, 1960, ndiyo tarehe ambayo Samia alizaliwa katika Kijiji cha Kizimkazi, Makunduchi, Mkoa wa Kusini, Unguja, Zanzibar. Baba yake mzazi, Suluhu Hassan, alikuwa mwalimu, akawa anapewa uhamisho wa mara kwa mara. Ni kwa sababu hiyo, Samia alisoma elimu ya msingi katika shule tofauti za Unguja na Pemba,

Darasa la kwanza mpaka la tatu (mwaka 1966 mpaka 1968), alisoma Shule ya Msingi Chwaka, Unguja. Samia alijiunga na Shule ya Msingi Ziwani mwaka 1969, alipoanzia darasa la nne. Samia alihitimu elimu ya msingi mwaka 1972, Shule ya Msingi Mahonda, Unguja.

Kidato cha kwanza mpaka cha tatu, Rais Samia alisoma Shule ya Sekondari Ng’ambo mwaka 1973 mpaka 1975, kisha Shule ya Sekondari Lumumba, alikosoma na kuhitimu kidato cha nne, mwaka 1976. Mwaka 1980 alisoma na kuhitimu astashahada ya juu ya Takwimu, Taasisi ya Fedha na Utawala Zanzibar (Zifa). Mwaka 1981, alisoma astashahada ya juu ya Uongozi, Zifa.

Mwaka 1983 hadi 1986, Rais Samia alisoma stashahada ya juu ya Masomo ya Uongozi wa Umma, Taasisi ya Maendeleo ya Uongozi Mzumbe (IDM – Mzumbe), Morogoro. Siku hizi taasisi hiyo inaitwa Chuo Kikuu cha Mzumbe. Kati ya mwaka 1992 na 1994, Rais Samia alisoma stashahada ya umahiri wa uchumi, Chuo Kikuu cha Manchester, UK.

Mwaka 2004, alihitimu shahada ya uzamili ya maendeleo ya uchumi, katika programu ya pamoja, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (Out) na Chuo Kikuu cha Southern New Hampshire, Marekani.

Mgombea huyu ana vyeti mbalimbali vya mafunzo kama ifuatavyo; Astashahada ya utawala, Chuo cha Taifa cha Utawala wa Umma, Lahore, Pakistan, mwaka 1987. Astashahada ya utawala, Taasisi ya Uongozi ya Mashariki na Kusini ya Afrika (Esam).  Cheti cha masomo ya utawala kwa viongozi, Chuo cha Hyaerabad, India.

Baada ya kumaliza kidato cha nne aliajiriwa Ofisi Kuu ya Maendeleo Zanzibar, kama ofisa masijala. Baada ya kujiendeleza kielimu, mwaka 1987, akiwa na diploma ya juu ya uongozi wa umma, alipanda cheo kuwa ofisa mipango, kisha aliajiriwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Ulimwenguni (WFP), alikofanya kazi kwa miaka tisa.

Kutoka WFP, aligeukia harakati. Alijiunga na Asazi za Kiraia (Azaki), katika eneo hilo, Samia alipanda hadi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Zanzibar.

Mwaka 2000, aligombea ujumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, viti maalumu (CCM), akashinda, kisha akateuliwa kuwa Waziri wa Vijana, Ajira, Maendeleo ya Wanawake na Watoto Zanzibar. Mwaka 2005, alitetea nafasi yake Baraza la Wawakilishi, akahamishwa kuwa Waziri wa Utalii, Biashara na Uwekezaji.

Mwaka 2010, aligombea ubunge Makunduchi, Zanzibar. Aliposhinda, aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira. Mwaka 2014, Samia alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba. Mwaka 2015, chama chake, CCM, kilimteua kuwa mgombea mwenza wa urais katika Uchaguzi Mkuu 2015.

Novemba 5, 2015, Samia aliapishwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kisha, uchaguzi mkuu 2020, Samia alipitishwa tena kuwa mgombea mwenza wa urais. Novemba 5, 2020, aliapishwa kwa mara ya pili kuwa Makamu wa Rais wa Tanzania. Machi 19, 2021, alikula kiapo kuwa Rais wa Tanzania, kufuatia kifo cha mtangulizi wake, Magufuli.

Samia anapoendelea na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, akiomba muhula wa miaka mitano, 2025/2030, anakuwa na mtaji wa alichokifanya miaka minne na miezi saba ya urais wake.

Angalau Watanzania wameshamwona, wanamfahamu na wanajua aina yake ya uongozi.

Samia ana shahada tatu za udaktari wa heshima. Ya kwanza alitunukiwa Novemba 30, 2022 na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ikiwa ni shahada ya udaktari wa heshima ya Ubinadamu na Sayansi Jamii.

Ya pili, alitunukiwa Oktoba 2023 na Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru (JNU), India kwa kuimarisha uhusiano na India, kukuza diplomasia ya kiuchumi.

Samia ni mwanamke wa kwanza kutunukiwa shahada hiyo na JNU.

Shahada ya tatu ya udaktari wa heshima, Samia alitunukiwa na Chuo Kikuu cha Zanzibar (Suza), Desemba 2023, kwa uongozi wa utalii na masoko. Ni sababu sasa jina lake linapotajwa, linaanza na Dokta (Dk), kutokana na heshima aliyopewa na vyuo vikuu hivyo vitatu.