Baada ya kusambaa kwa taarifa zinazomuhusu kocha wa Simba, Fadlu Davis kuondoka klabuni hapo pamoja na benchi lake la ufundi akisalia Kocha Msaidizi pekee, Selemani matola, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo Ahmed Ally amewataka mashabiki wa klabu hiyo kuwa na subira.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Ahmed Ally amechapisha ujumbe huo huku akisisitiza kuwa hakuna kitakachoharibika ndani ya klabu hiyo.
Ameandika “Good Morning Wana Simba
Tuendelee kuwa na subira tukisubiri taarifa sahihi na rasmi kutoka kwa viongozi wetu
Ninachoweza kuwahikikishia kwamba hakuna kitakachoharibika wala kurudi nyuma ndani ya klabu yetu, Tunasonga mbele tukiwa bora na imara zaidi
Kwa sasa tutasikia mengi kila mtu akijaribu kupenyeza agenda zake kwa lengo la kuzua taharuki ndani ya klabu yetu
Jahazi letu lipo sawa, halijayumba wala kutikisika, Tunaendelea na safari ya mafanikio”
Simba inakabiliwa na michezo miwili hivi karibuni, wa Ligi Kuu dhidi ya Fountain Gate utakaopigwa Septemba 25 kwenye uwanja wa KMC Complex na ule wa marudiano dhidi ya Gaborone United utakaopigwa Septemba 28 kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa.
Licha ya kusafiri na timu kwenda Botswana kwenye mchezo wa kimataifa dhidi ya Gaborone na kushinda kwa bao 1-0, Fadlu ambaye ni kocha mkuu wa Simba, Darian Wilken kocha msaidizi na Wayne Sandilands kocha wa magolikipa hawakurejea nchini na timu huku ikitajwa wamepata ofa kubwa zaidi katika klabu ya Raja Athletic.