Mahakama yatupa mapingamizi ya Tundu Lissu, kesi kuendelea

Dar es Salaam. Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam imetupilia mbali hoja zote za pingamizi la Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu kuhusiana na ubatili wa hati ya mashtaka.

Lissu, ambaye anakabiliwa na mashtaka ya uhaini, alidai kuwa hati ya mashtaka ni batili kwa kuwa haioneshi maelezo ya kosa wala nia ya kutenda kosa la uhaini ambayo ni viini muhimu katika hati ya mashtaka.

Katika uamuzi wake uliotolewa leo Jumatatu, Septemba 22, 2025 uliosomwa na kiongozi wa jopo la majaji, Jaji Dunstan Ndunguru imesema kuwa baada ya kupitia hati hiyo imeridhika ipo sahihi kwani, inatoa maelezo ya kosa kama sheria inavyoelekeza. Pia, imeeleza kuhusu suala la nia ya kutenda kosa la uhaini hilo ni suala la ushahidi unaotarajiwa kuwasilishwa.

Kuhusu hoja kuwa maelezo ya mashahidi ni batili kutokana na kukiuka amri ya Mahakama Kuu ya kuwalinda mashahidi wa Jamhuri ambao ni raia, na maelezo ya askari Polisi kuchukuliwa kinyume na sheria, Mahakama imeeleza hoja hizo zinagusa mwenendo kabidhi (committal proceedings) suala ambalo ilishalitolea uamuzi.

Hivyo, Mahakama hiyo imehitimisha kuwa pingamizi la Lissu halina msingi na imelitupilia mbali.