Dar es Salaam. Mvutano baina ya Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), umeendelea kuchukua sura mpya na sasa askari wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania, wamezingira ofisi za chama hicho zilizopo Mikocheni, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyosainiwa na Rais wa TLS, Boniface Mwabukusi imeeleza makao makuu yake yamezingirwa na askari tangu asubuhi ya leo Jumatatu, Septemba 22, 2025.
Hata hivyo, katika taarifa yake hiyo Mwabukusi amesema kuwa badala ya kundi kubwa la askari kuzingira ofisi hiyo ni vyema rasilimali hiyo ikaelekezwa katika kuwakoa ndugu waliopotezwa, kuungana na familia zao.
“Tunawasihi mawakili wote wanaofika ofisini kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali kuchukua tahadhari na kutochokozeka kwa uchokozi huu wa makusudi,” amesema Mwabukusi kwenye taarifa hiyo.
Jeshi la Polisi limezingira ofisi hizo wakati kukiwa na vuguvugu la chama hicho kuitumia siku ya leo Jumatatu, Septemba 22, 2025 kufanya maandamano ya amani.
TLS ilitangaza kufanya maandamano hayo kama hatua ya kulaani tukio la vurugu zinazodaiwa kufanywa na askari Polisi katika viunga vya Mahakama Kuu Septemba 15, 2025 la wakili Deogratius Mahinyila kudhalilishwa wakati akifuatilia kesi ya Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu.
Waraka wa TLS uliotolewa Septemba 18, 2025, kwanza ulieleza kusikitishwa na tukio hilo ambalo limetajwa kuwa kinyume na misingi ya haki, utu na uhuru wa wanasheria kutekeleza majukumu yao bila kuingiliwa. Hivyo, kutangaza hatua kadhaa ikiwemo maandamano ya amani ikiwa ni sehemu ya kufikisha ujumbe wa kulaani tukio hilo.
Hadi kufikia asubuhi ya leo, askari Polisi walionekana wakiwa wamezingira ofisi za chama hicho kuimarisha ulinzi. Hata hivyo, TLS imewataka wanachama wake kuchukua tahadhari na kutokubali kuchokozeka pale wanapochokozwa.
“TLS itaendelea kutimiza wajibu wake bila woga, upendeleo, hofu wala husuda katika kuhakikisha utawala wa sheria na haki za binadamu zinasimamiwa na kuheshimiwa,” amesema Mwabukusi.