KATIKA kutoa hamasa kwa timu za Zanzibar zinazoshiriki mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi amesema atanunua kila bao litakalofungwa na timu hizo kwa Sh5 milioni.
Hayo yameelezwa jana Septemba 21, 2025 na Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Fatma Hamad Rajab wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumalizika kwa mchezo wa hatua ya awali ya Kombe la Shirikisho Afrika kati ya KMKM na AS Port ya nchini Djibouti.
Katika mchezo huo uliochezwa Uwanja wa New Amaan Complex kisiwani hapa, KMKM iliibuka na ushindi wa mabao 2-1, huku AS Port ikiuchagua uwanja huo kwa mechi ya nyumbani. Kwa upande wa Mlandege iliyocheza Septemba 20 mwaka huu dhidi ya Ethiopian Insurance katika Ligi ya Mabingwa Afrika, ilipoteza kwa mabao 2-0, mchezo uliopigwa Uwanja wa Abebe Bikila nchini Ethiopia.
Katibu huyo amesema kununuliwa kwa mabao hayo ni kuonesha hamasa kwa wachezaji kufanya vizuri zaidi ili kufika mbali katika mashindano hayo.
“Hii ni hamasa kwa wachezaji kuonesha uwezo wao kwa kila mchezo kwani jambo hilo litaipa sifa Zanzibar na kuipandisha hadhi katika viwango vinavyostahili,” amesema.
Ameeleza, fedha hizo zinaanza kutoka hivi sasa baada ya KMKM kufunga mabao mawili katika mchezo wake wa kwanza ambapo itakabidhiwa Sh10 milioni na zoezi hilo litaendelea hadi hatua watakayofikia timu hizo.
Katika taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF) Septemba 20 mwaka huu, wadau, mashabiki na taasisi za serikali wameombwa kuziunga mkono timu hizo katika ushiriki wa mashindano ya kimataifa ili ziweze kuvuka hatua ya awali na kufika mbali.
Baada ya kufanyika michezo ya kwanza, timu hizo zitashuka tena dimbani kwenye Uwanja wa New Amaan Complex ambapo Septemba 26, 2025 KMKM itaikaribisha AS Port, kisha Septemba 27, 2025 ni Mlandege dhidi ya Ethiopian Insurance.