CHUO cha Muziki (DCMA) kwa kushirikiana na Kituo cha OlimpAfrica, wamefanya tamasha la muziki lililopewa jina la Tutambue lililofanyika Dole, Wilaya ya Magharibi A, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Katika tamasha hilo, Mkurugenzi wa Sanaa kutoka DCMA, Tryphone Evarist ametoa wito kwa wananchi kuacha kuamini kuwa muziki ni kazi isiyokuwa na maadili, huku akisisitiza kwamba hiyo ni kama kazi nyingine kwani ni sehemu ya kujipatia kipato.
Ameeleza kuwa, muziki kwa upande wa Zanzibar, umekuwa na changamoto kubwa kwa sababu ya dhana potofu zinazorudisha nyuma vipaji vya baadhi ya vijana.
“Chuo hiki kipo kwa ajili ya kuendeleza muziki wa Taarab ambao ni asili ya Zanzibar kwa kutangaza nchi za nje,” amesema.
Mkurugenzi huyo amesema yeye ni miongoni mwa wanufaika wa chuo hicho na sasa amekuwa muimbaji mzuri ambaye anatuimbiza ndani na nje ya Tanzania.
Amefafanua kuwa sio rahisi jamii kukubali kazi hiyo, hasa wakati wa kujifunza, hivyo ametoa wito kwa wanaohitaji kujifunza muziki wasiache na waheshimu vipaji vyao kwa kuviendeleza kwani hizo ndio ajira zao.
Naye Ofisa Michezo kutoka kituo cha OlimpAfrica, Rashid Nassor Ali, amesema lengo la tamasha hilo ni kuzienzi nyimbo za taarab na kurithishana vipaji hivyo kwa vizazi vijavyo.
Vilevile, amesema ni wakati wa wazazi kuwaruhusu vijana wao ili kutafuta changamoto mpya za maisha katika nyanja ya muziki.
Kwa upande wake mwanafunzi wa DCMA, Mzee Omar Khamis amesema katika chuo hicho amepata nafasi ya kujifunza ala ya violin kwa miaka mitatu ingawaje alikutana na changamoto mbalimbali ikiwemo kuonekana kutokuwa na maadili.