Lissu akwama tena kujinasua katika kesi ya uhaini

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, amekwama tena kwenye jaribio la kujinasua katika kesi ya uhaini inayomkabili, baada ya Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam kutupilia mbali sababu nyingine ya pingamizi lake.

Hii ni mara ya pili kwa Lissu jitihada zake za kumaliza kesi hiyo kwa mbinu za kiufundi, kupitia pingamizi la awali baada ya Septemba 15, 2025, Mahakama hiyo kutupilia mbali pingamizi lake hilo.

Uamuzi huo umetolewa leo Septemba 22, 2025 na jopo  ya  jopo la majaji watatu, Dunstan Ndunguru (kiongozi wa jopo) James Karayemaha na Ferdnand Kiwonde, kuhusiana na sababu ya pingamizi la Lissu kuwa hati ya mashtaka ina kasoro zisizorekebishika.

Kutokana na sababu hiyo na hoja alizozitoa mahakamani hapo Lissu aliiomba Mahakama hiyo iifute kesi hiyo na imwachilie huru, hoja ambazo zilipingwa vikali na Jamhuri iliyodai kuwa hati hiyo haina kasoro zozote na inakidhi matakwa ya kisheria.

Lissu  anakabiliwa na shtaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalotokana na maneno aliyoyatamka kuhusiana na kuzuia kufanyika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Anadaiwa kuwa Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania, kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyia kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, huku akitamka na kuandika maneno ya kumshinikiza kiongozi Mkuu wa Serikali ya Tanzania kuwa:

“Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli…, kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko…, kwa hiyo tunaenda kikinukisha…, sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli…, tunaenda kukinukisha vibaya sana…”

Septemba 8, 2025, kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya usikilizwaji wa awali,  Lissu aliibua pingamizi la awali.

Katika pingamizi hilo aliiomba Mahakama isiendelee na usikilizwaji badala yake akaiomba mahakama iitupilie mbali huku akibainisha sababu mbili, Mosi kwamba hati ya mashtaka ina kasoro za kisheria zisizorekebishika na ya pili kwamba Mahakama hiyo haina mamlaka kuisikiliza kutokana na kasoro za kisheria

Mahakama ilisikiliza kwanza sababu ya mamlaka ya Mahakama ambayo mahakama hiyo katika uamuzi wake  Septemba 15, 2025, iliitupilia mbali ndipo ikasikiliza hoja yake ya ubatili wa hati ya mashtaka, ambalo Mahakama imelitolea uamuzi leo.

Katika uamuzi huo Mahakama imetupilia mbali hoja zote za Lissu, badala yake imekubaliana na hoja za Jamhuri kuwa hati hiyo ya mashtaka haina kasoro za kisheria na ipo sahihi na imekidhi matakwa ya kisheria.

Mahakama hiyo imefikia uamuzi huo baada ya kupitia na kuchambua hoja za pande zote katika mizania ya kisheria na kesi rejea mbalimbali zilizowasilishwa na pande zote, zilizokwisha kuamuliwa na Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani zenye mazingira sawa na kesi hiyo.

Hoja za sababu ya pingamizi

Mosi, kwamba hati ya mashtaka kuwa  kasoro zisizorekebishika.

Akisoma uamuzi huo Jaji Ndunguru amesema kuwa hati lazima iwe na maelezo maalumu yanayoonesha asili ya shitaka linalomkabili mshtakiwa kwa mujibu wa kifungu cha 135 cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA)


Lissu akwama tena kujinasua katika kesi ya uhaini

Amesema kuwa kifungu cha 138 (1) (i-v) (CPA) ndicho kinachoeleza namna ambavyo hati ya mashtaka inapaswa kuwa.

Baada ya kurejea hati ya mashtaka iliyokuwa inabishaniwa, huku akisoma maeneo yanayodaiwa kutolewa na Lissu yaliyomo katika hati hiyo,  Jaji Ndunguru amesema kuwa Mahakama inaona kwamba  hati hiyo iko wazi na inakidhi matakwa ya kisheria.

Jaji Ndunguru amesema kuwa katika kesi alizozirejea Lissu hasa kesi ya Hatibu Gandhi, Mahakama ya Rufani ilisema kuwa, mahakama ya Tanzania haifungwi na mfumo na  misingi ya sheria za Uingereza kama ambavyo mshtakiwa Lissu alidai.

Jaji Ndunguru amesema kuwa  hati hiyo ya mashtaka kwa jinsi ilivyo imebainisha viini vyote viwili muhimu, yaani maelezo ya kosa na asili ya kosa.

“Kama upande wa mashtaka ulivyoeleza hati ya mashtaka imeeleza nia ya kuushawishi umma kuzuia uchaguzi Mkuu na imeeleza hilo lilifanywa kwa nia ya kutishia utawala (Serikali) na kwamba nia hiyo imedhihirishwa kwa matendo ya kutamka maneno hayo aliyoyasema”, amesema Jaji Ndunguru.

Amesema hoja ya msingi ni kwamba iwapo maneno hayo yanadhihirisha nia hilo suala la ushahidi utakaoletwa mahakamani ambalo Mahakama haiwezi kuliamua kwa sasa.

Hata hivyo amesema kuwa msingi wa kifungu cha 138 hati ya mashtaka inapaswa kuzingatia kesi Grey Likungu Mattaka na wenzake pamoja na kesi ya Hatibu Gandhi na wenzake, kama ambavyo mshtakiwa alidai kuwa ni lazima nia ya kutenda kosa ibainishwe kwenye hati ya mashtaka.

Jaji Ndunguru amesema kuwa katika mazingira hayo kifungu cha 135 na 138 ndivyo vinavyoongoza uandaaji maelezo ya shtaka na kwamba  Mahakama inaona kuwa vifungu hivyo vinajitosheleza na hakuna ulazima wa kutumia mfumo wa Uingereza.

“Hivyo Mahakama inaona kuwa hoja ya kwanza haina msingi”, amesema Jaji Ndunguru.

Mbili, kama hati ya mashtaka ilifanyiwa marekebisho isivyo halali.

Jaji Ndunguru katika hoja hiyo amesema kuwa inaona kuwa hati hiyo ya mashtaka iko sahihi na kwamba haijafanyiwa marekebisho.

Akiamua hoja hiyo Jaji Ndunguru amerejea kifungu cha 262(1), akisema kuwa kwa mujibu wa kifungu hicho Mahakama inakubaliana na hoja ya upande wa Jamhuri kuwa hati ya mashtaka katika kesi zinazosikilizwa na Mahakama Kuu hati ya mashtaka katika Mahakama ya Ukabidhi (committal court) yaani Mahakama ya chini (Wilaya au Mahakama ya Hakimu Mkazi) inayofanya uchunguzi wa awali  inakuwa ni pendekezwa tu.

Jaji Ndunguru amesema  kwamba kwa mujibu wa kifungu hicho baada ya upelelezi kukamilika na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) anaona kuna ushahidi anaweza chini ya kifungu 262 (2) kuandaa hati ya mashtaka rasmi.

Amesema kuwa DPP ataandaa hati ya mashtaka baada ya kusoma jalada la uchunguzi na kujiridhisha kuwa ana ushahidi na kuipeleka kwa Msajili wa Mahakama Kuu ambaye atawasilisha kwa Mahakama ya Ukabidhi, na hiyo ndio itakuwa hati rasmi ambayo mshtakiwa atasomewa Mahakama Kuu.

“Hivyo tunaona kwamba hati ya mashtaka aliyosomewa katika Mahakama ya Ukabidhi ndio hiyohiyo na hivyo tunakubaliana na upande wa Jamhuri kuwa hati ya mashtaka haijawahi kufanyiwa marekebisho yoyote” amesema Jaji Ndunguru.

Kuhusu hoja ya maelezo ya mashahidi raia kutokuzingatia amri ya Mahakama Kuu ya ulinzi wa mashahidi hao na kwamba yameandikwa kinyume na sheria, Jaji Ndunguru amesema kuwa kwa kuwa hoja hizo zinahusu suala la mwenendo kabidhi  ambalo ilishalijadili na kulitolea uamuzi, mahakama hiyo haiwezi kuliamua tena.

Kuhusu maelezo ya mashahidi ambao ni askari kuchukuliwa kinyume cha sheria pia kulizungumzia ni kufungua upya ukurasa kama mwenendo kabidhi ulikuwa sahihi au haukuwa sahihi.

“Hivyo kwa kauli moja Mahakama hii inaona kuwa pingamizi hili halina mashiko na inalitupilia mbali,” amehitimisha Jaji Ndunguru.