Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, imeyakataa maombi ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, ya kesi yake kusikilizwa mubashara.
Mahakama hiyo imesema kuwa ingawa ni msingi muhimu wa haki huru, kwamba haki inatakiwa siyo tu itendeke, bali ionekane ikitendeka, lakini imesema kuwa hata hivyo hakuna kanuni zinazosimamia usikilizwaji wa kesi mubasahara.
Mahakama hiyo imesisitiza kuwa kwa mazingira ya kesi hiyo na hasa kutokana na kuwepo kwa amri ya ulinzi wa mashahidi na kwa kuzingatia matakwa ya utaratibu wa kikanuni kuwa shahidi mmoja anayetakiwa kutoa ushahidi hapaswi kusikiliza ushahidi wa shahidi mwingine, kesi hiyo haitasikilizwa mubashara.
Badala yake mahakama hiyo imesema kuwa kesi hiyo itaendelea kusikilizwa katika Mahakama ya wazi, kama sheria inavyoelekeza, ambapo kila mtu anaruhusiwa kuingia kusikiliza pamoja na vyombo vya habari.

Uamuzi huo umetolewa leo Jumatatu, Septemba 22, 2025 na jopo la Majaji watatu, Dunstan Ndunguru (kiongozi wa jopo) James Karayemaha na Ferdnand Kiwonde, kufuatia maombi yaliyowasilishwa na Lissu.
Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalotokana na maneno aliyoyatamka kuhusiana na kuzuia kufanyika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Anadaiwa kuwa Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania, kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyia kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, huku akitamka na kuandika maneno ya kumshinikiza kiongozi Mkuu wa Serikali ya Tanzania kuwa:
“Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli…, kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko…, kwa hiyo tunaenda kikinukisha…, sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli…, tunaenda kukinukisha vibaya sana…”
Septemba 8, 2025, kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya usikilizwaji wa awali Lissu aliibua pingamizi la awali na pia akawasilisha ombi la kuruhusu kesi hiyo isikilizwe mubashara kupitia vyombo vya habari na mitandao mbalimbali.
Hata hivyo mahakama hiyo katika uamuzi wake ilioutoa leo imelikataa ombi hilo.
Akisoma uamuzi huo Jaji Ndunguru ameanza kwa kusema kuwa ombi hilo limejikita katika kanuni za msingi za haki huru (open justice), kwamba haki si tu itendeke bali ionekane ikitendeka na haki hiyo imezungumzia katika mashauri mengi yaliyokwishaamuliwa na Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani.
Amesema kwa mujibu wa kifungu cha 192 CPA Mashauri ya Jinai husikilizwa Mahakama ya wazi kama inavyofanyika hata sasa katika kesi hiyo.
Hata hivyo amesema kuwa hakuna kanuni inayoratibu uendeshaji wa mashauri mubashara jambo ambalo inakuwa vigumu kuliratibu.
Jaji Ndunguru amesema, “kulingana na mazingira ya kesi hii kwamba kuna amri ya Mahakama Kuu kuwalinda mashahidi na kwa kuzingatia kanuni ya kawaida kwamba shahidi anapotoa ushahidi shahidi mwingine haitakiwi kujua alichokisema shahidi mmoja, hivyo itakuwa ni vigumu kuwa na udhibiti.”
“Mahakama inaona katika mazingira haya haitafaa kurushwa mubashara na kwa sababu tunatumia mahakama ya wazi, na haijakataza waandishi wa habari, hivyo itaendelea kutumia mahakama ya wazi,” amesema Jaji Ndunguru.