Fadlu atambulishwa Raja Club Athletic, Simba yamshukuru

Klabu ya Raja Club Athletic imetangaza kufanya mabadiliko katika benchi lake la ufundi.

Katika taarifa yake waliyoichapisha kwenye mtandao wa kijamii imesema

“Kulingana na mapendekezo ya Mkurugenzi wa Michezo na tathmini ya jumla iliyofanywa na Kamati ya Michezo kuhusu awamu ya maandalizi ya msimu huu, pamoja na mechi rasmi za kwanza, Raja Club Athletic inatangaza kusitisha mkataba na Lassad Chabbi na benchi lake la ufundi”.

“Bodi ya wakurugenzi ya klabu inatoa shukurani zake za dhati kwa Lassad Chabbi na wafanyakazi wake wa ufundi kwa kazi nzuri na ya kitaalamu katika kutekeleza majukumu yao, na kuwatakia kila la kheri katika juhudi zao za baadaye”.

“Raja Club Athletic inatangaza uteuzi wa Fadlu Davids kama kocha mkuu wa kikosi cha kwanza. Davids alikuwa mtu muhimu katika msimu wa kihistoria wa 2023-2024: Mashindano ya Kitaifa (Botola Pro), ambayo timu ilishinda bila kushindwa ambapo alicheza jukumu muhimu katika hili kama kocha msaidizi”.

“Uteuzi wa Fadlu Davids kukiongoza kikosi cha kwanza cha Raja ulitokana na ujuzi wake wa awali wa klabu, ambao unamfanya kuwa mtu sahihi wa kuimarisha mshikamano wa kikundi na kuiongoza Raja Club Athletic kufikia malengo yake ya kimichezo na kitaasisi”.

“Uamuzi huu unakuja ndani ya mfumo wa mwendelezo wa mradi mpya wa Raja Club Athletic, ambao unalenga kujenga muundo thabiti, unaofaa na maono yenye mwelekeo wa siku zijazo”.

“Klabu inathibitisha kuegemea kwake kwa usaidizi usio na masharti wa mashabiki wake waaminifu kuunga mkono timu katika awamu hii mpya”.

Wakati Raja ikimtangaza Fadlu kuwa kocha wao mpya, klabu ya Simba nayo imemuaga kocha huyo na kumtakia kheri hukon aendako huku ikimshukuru kwa mafanikio waliyoyapata akikiongoza kikosi hicho.

“Uongozi wa klabu ya Simba umefikia makubaliano ya kusitisha mkataba na kocha Mkuu Fadlu Davids baada ya kuhudumu na timu kwa kipindi cha mwaka mmoja”.

“Makubaliano haya ni matakwa binafsi ya kocha Fadlu kwa uongozi wa klabu”.

“Klabu ya Simba inamshukuru Kocha Fadlu kwa kuiongoza Simba kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita na kumalizia nafasi ya pili kwenye Ligi kuu ya NBC”.

“Uongozi wa klabu unamtakia kheri na baraka kocha Fadlu katika maisha yake ya soka nje Simba”.