MABINGWA wa zamani wa Tanzania, Mtibwa Sugar imeanza vibaya Ligi Kuu Bara kwa kufungwa bao 1-0 na Mashujaa mjini Kigoma, huku kocha wa kikosi hicho, Awadh Juma ‘Maniche’ ametaja sababu za kupoteza alama tatu, akiwataja washambuliaji.
Mtibwa iliyorejea katika ligi hiyo baada ya kupanda daraja msimu huu tangu iliposhuka msimu wa 2023-2024 kwa kucheza Ligi ya Championship, pambano la juzi lilikuwa la kwanza huku la Mashujaa likiwa la pili na kuifanya iongoze msimamo kwa pointi nne sawa na ilizonazo Namungo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Maniche alisema, kilichokwamisha kikosi hicho sio ubora wa mchezaji mmoja ila eneo la mbele kushindwa kutumia nafasi.
Alisema, kuna makosa madogo madogo yaliyofanyika ambayo yamemuonyesha mapema wapi panavuja, licha ya matamanio yake ya kushinda mchezo wa kwanza kutokukamilika.
“Yapo maeneo ya kuyaimarisha ikiwamo safu ya ulinzi ambayo ndio imeonekana kuwa na udhaifu uliosababisha bao moja kuingia na hilo ndilo nitaanza nalo mazoezini,” alisema Maniche nyota wa zamani wa klabu hiyo na Simba, akiyeongeza;
“Kingine ni washambuliaji wameniangusha sana, kwa sababu hawakuweza kutengeneza na kuzitumia nafasi nyingi, ambazo zingeweza kuleta matokeo zaidi ya waliyopata wapinzani.”
Mtibwa iliruhusu bao dakika ya 33 ya kipindi cha kwanza, lililofungwa na kiungo Idrisa Stambuli, ukiwa ni ushindi wa pekee kwenye mechi hiyo.
Mtibwa itakuwa nyumbani katika mchezo wa pili wa ligi kuvaana na Fountain Gate ambayo Alhamisi itatupa karata dhidi ya Simba, baada ya awali kupoteza nyumbani kwa mabao 1-0 mbele ya Mbeya City.