KOCHA mkuu wa Mashujaa, Salum Mayanga amesema ana kazi kubwa ya kufanya kwenye safu yake ya ushambuliaji kuhakikisha wanatumia kila nafasi wanayotengeneza huku akiweka wazi kuwa ligi ya msimu huu ni pasua kichwa.
Mayanga amefunguka hayo baada ya kukusanya pointi nne kwenye mechi mbili walizocheza akianza na sare dhidi ya JKT Tanzania ya bao 1-1 na juzi kuibuka na ushindi mbele ya Mtibwa Sugar iliyopanda daraja msimu huu.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mayanga alisema sio mwanzo mbaya lakini ameona upungufu hasa kwenye safu yake ya ushambuliaji licha ya kutengeneza nafasi nyingi wanashindwa kuzitumia ila anaamini inatokana na presha kubwa ya ushindani wa ligi.
“Msimu huu ligi ni ngumu tunatakiwa kuchanga karata zetu vizuri ili kuwa bora ni kutumia nafasi tunazotengeneza hili ni eneo ambalo natakiwa kulifanyia kazi mapema zaidi maeneo mengine kama safu ya ulinzi ni makosa madogo madogo pia nitakaa na kuelekezana na wachezaji wangu,
‘’Ubora kwenye ligi yetu umeongezeka tunatakiwa kujipanga, makosa tuliyoyafanya katika mchezo uliopita dhidi ya JKT Tanzania yamefanyiwa kazi dhidi ya Mtibwa Sugar ndio maana umeona baada ya kushinda hatujaruhusu wapinzani kusawazisha kama ilivyotokea mchezo wa kwanza.”
Mayanga alisema baada ya ushindi ugenini sasa wanaangalia ni namna gani wanaenda kupata matokeo mchezo unaofuata kwa kuzingatia makosa waliyoyaonyesha na kuyafanyia kazi huku akiweka wazi kuwa utimamu wa wachezaji wake na utayari wa kuonyesha ushindani upo vizuri.
“Timu ipo vizuri, makosa madogo ndio yanatugharimu, lakini nawapongeza wachezaji wangu kwa kuzingatia yale ninayowaelekeza. Tunarudi kwenye uwanja wa mazoezi, tutaanza na tulipokosea na kujiandaa kwa mechi inayofuata, naamini kutakuwa na mabadiliko makubwa na tunaweza kuwa bora zaidi.”