WANANCHI WAPATA FURSA YA VIPIMO VYA MOYO KATIKA MAONESHO YA MADINI GEITA

Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Henry Mayala akimpima kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi  mkazi wa Geita aliyefika katika banda la  taasisi hiyo lililopo katika maonesho ya nane ya kitaifa ya teknolojia ya madini yanayofanyika katika Viwanja vya Maonesho vya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwaajili ya kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo.

……………..

Na Jeremia Ombelo – JKCI, Geita

22/09/2025 Wananchi wa mkoa wa Geita wameombwa kujitokeza kupata vipimo na matibabu ya magonjwa ya moyo katika Maonesho ya Nane ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika katika Viwanja vya Maonesho vya Dkt. Samia Suluhu Hassan vilivyopo  mjini Geita.

Wito huo umetolewa leo na daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Henry Mayala wakati akizungumza na waandishi wa habari waliofika katika banda la taasisi hiyo lililopo katika maonesho hayo yanayoendelea mkoani Geita.

Dkt. Mayala alisema lengo la kushiriki kwenye maonyesho hayo ni kuhakikisha wananchi wanapata nafasi ya kujua hali ya afya zao na kupata msaada wa kitaalamu kutoka kwa madaktari bingwa bobezi mapema.

“Tumekuja Geita katika maonyesho ya madini kwaajili ya kutoa huduma za upimaji wa magonjwa ya moyo, tutawapima wananchi shinikizo la juu la damu, kisukari, uzito na vilevile tunatoa elimu ya afya jinsi ya kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza”, alisema Dkt. Mayala.

Aliongeza kuwa mbali na elimu ya afya wataalamu hao wameenda na vifaa vya kisasa vya kuchunguza moyo vitakavyotumika kuwapima wananchi jinsi mioyo yao inavyofanya kazi na kuhakikisha matatizo ya moyo yanabainika mapema.

“Tumekuja na vifaa ambavyo vinaangalia uwezo wa moyo kufanya kazi na kama kuna shida yoyote kwenye moyo, tunatoa huduma hizi bila malipo kwa lengo la kuwasaidia wananchi kupata uelewa wa afya zao”.

“Tunatoa wito kwa wakazi wote walioko maeneo ya Geita na mikoa ya jirani waje kufanya vipimo vya moyo, ni vizuri kujua afya yako mapema na kuchukua hatua”, alisisitiza Dkt. Mayala.

Kwa upande wao wananchi waliojitokeza kupata huduma za vipimo na matibabu ya moyo walifurahishwa na huduma zinazotolewa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na kuomba serikali kuendeleza jitihada hizo katika maeneo mengine nchini.

“Ninashukuru nimepata huduma zote kuanzia vipimo vya awali mpaka vipimo vya moyo katika banda la JKCI, naiomba Serikali iendelee kufanya hivi katika maeneo mbalimbali kwani itakuwa ni fursa ya kuwafikia watu wengi bila gharama,” alisema Hassan Omar Mkazi wa Mwanza.

“Nimekuja Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ajili ya kupata huduma za vipimo na matibabu ya moyo, kiukweli huduma zao ni nzuri mpaka sasa hivi nasubiria kuelekea kwa daktari kwaajili ya tiba”,  alisema Melesiana Malima mkazi wa Tambuka Reli Geita.

Huduma zinazotolewa na wataalamu wa JKCI katika Maonyesho ya Nane ya Teknolojia ya Madini Geita ni sehemu ya juhudi za taasisi hiyo kuhamasisha jamii kujikinga na magonjwa ya moyo kwa kupima afya zao mapema, kupata elimu na ushauri wa magonjwa ya moyo.

Mwisho