Dar/Mikoani. Maandamano ya mawakili wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) yaliyopangwa kufanyika nchi nzima leo Septemba 22, 2025 kupinga kushambuliwa kwa wakili Deogratius Mahinyila, yameyeyuka huku Jeshi la Polisi likiweka kambi kati ofisi za chama hicho.
Maandamano hayo yalichochewa na tukio la Septemba 15, 2025 wakati kesi ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu ikisikilizwa, baada ya Mahinyila ambaye ni pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha) kushambuliwa na askari wakati wakimkamata.
Baada ya tukio hilo, Baraza la Uongozi la TLS liliazimia kufanya maandamano ya amani nchi nzima, kulaani kitendo cha kushambuliwa kwa Wakili Mahinyila na askari polisi akiwa mahakamani.
Hata hivyo, licha ya uamuzi huo wa TLS, Jeshi la Polisi lilionya kuhusu maandamano hayo likieleza wasingeweza kutoa ulinzi kwa kuwa, wamejielekeza kwenye ulinzi wa mikutano ya kampeni za uchaguzi, hivyo iliyazuia.
Wakati polisi wakipiga kambi Dar es Salaam, huko mikoani hali ni shwari kwa kuwa, maandamano hayo hayajafanyika huku viongozi wa chama hicho wakieleza, yameahirishwa baada ya mazungumzo ya viongozi wao na jaji Mkuu, George Masaju.
Katika Mkoa wa Dar es Salaam, Jeshi la Polisi limeweka kambi katika ofisi za TLS ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuwazuia viongozi wa chama hicho kwenda kuhamasisha na kuongoza maandamano hayo.
Mwananchi imefika katika ofisi za TLS saa 4 asubuhi na kushuhudia polisi wakiwa na kwenye magari matano, idadi yao ikiwa zaidi ya 20 na magari hayo yalikuwa yameegeshwa pembeni huku barabara hiyo ikiendelea kutumiwa na wapiti njia wengine.
Vilevile, Mwananchi imeshuhudi askari wengine wakiwa wamesimama kwenye lango kuu la kuingilia kwenye ofisi za TLS. Hadi gazeti hili linakwenda mtamboni, saa 10 jioni, Jeshi la Polisi lilikuwa bado linalinda doria katika eneo hilo.
Wakati ulinzi ukiimarishwa kwenye ofisi hizo, Rais wa TLS, Boniface Mwabukusi ametoa taarifa akieleza kwamba, makao makuu ya chama hicho yamezingirwa na askari tangu asubuhi ya leo Jumatatu, Septemba 22, 2025.
Hata hivyo, katika taarifa yake hiyo, Mwabukusi amesema badala ya kundi kubwa la askari kuzingira ofisi hiyo ni vema rasilimali hiyo ikaelekezwa katika kuwakoa ndugu waliopotea ili kuungana na familia zao.
“Tunawasihi mawakili wote wanaofika ofisini kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali kuchukua tahadhari na kutochokozeka kwa uchokozi huu wa makusudi,” amesema Mwabukusi kwenye taarifa hiyo.
Hata hivyo, TLS imewataka wanachama wake kuchukua tahadhari na kutokubali kuchokozeka pale wanapochokozwa.

“TLS itaendelea kutimiza wajibu wake bila woga, upendeleo, hofu wala husuda katika kuhakikisha utawala wa sheria na haki za binadamu zinasimamiwa na kuheshimiwa,” amesema Mwabukusi.
Amesema TLS, wanawasihi mawakili wote kubaki na tahadhari na kutii maelekezo ya baraza la uongozi.
“TLS itaendelea kutimiza wajibu wake bila uwoga, upendeleo, hofu wala husda katika kuhakikisha utawala wa sheria na haki za binadamu zinasimamiwa na kuheshimiwa,” amesema Mwabukusi.
Katika hatua nyingine, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimepinga vikali kitendo cha Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kuzingira ofisi za TLS bila kutoa sababu zozote za msingi.
LHRC inasisitiza kuwa, ni wajibu wa vyombo vyote vya dola kuheshimu misingi ya sheria, pamoja na kanuni na miongozo ya kimataifa na kikanda inayolinda uhuru wa vyama vya wanasheria katika kutekeleza majukumu yao kwa uhuru na bila hofu.
“Tunatoa wito kwa polisi kuchukua hatua za haraka kuwaondoa askari walioko katika ofisi za TLS ili kuruhusu mawakili na wateja wao kendelea na shughuli zao kwa amani na utulivu,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Wakati hayo yakitokea Dar es Salaam, huko mikoani hali ni shwari kwa kuwa, hakuna maandamano yoyote yaliyotokea. Mwananchi imebaini hali ya utulivu katika mikoa ya Dodoma, Arusha, Mwanza na Shinyanga.
Mwenyekiti wa mawakili Mkoa wa Dodoma Mary Munisi amesema: “Mawakili hatuandamani leo, ni kweli tulikuwa na mpango huo, lakini kwa sasa hebu zungumzeni na Rais wetu ama makamu wake watawapeni majibu.”
Mwenyekiti wa TLS Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, Shaban Mvungi amesema maandamano ya amani yaliyopangwa kufanyika leo Septemba 22, 2025 wilayani humo yameahirishwa.
Mvungi amesema wameahirisha kutokana na maelekezo kutoka ngazi ya juu ya TLS kufuatia mazungumzo yanayoendelea kati yao na vyombo vya dola.
“Ni kweli maandamano hayo yalipangwa kufanyika leo, lakini tumepewa maelekezo kwamba tusitishe kwanza, kwa sababu kulikuwa na mazungumzo kati ya TLS, jaji mkuu pamoja na vyombo vya dola, mpaka pale tutakapowatangazia tena,” amesema Mvungi.
Mwenyekiti wa TLS Mkoa wa Mwanza, Wakili Joseph Mugabe ameiambia Mwananchi kuwa, maandamano hayo yameahirishwa kutokana na mazungumzo yaliyofanyika leo kati ya Jaji Mkuu, George Masaju na viongozi wakuu wa TLS na wamekubaliana kupata mwafaka wa madai hayo ndani ya siku saba.
“Leo hakutakuwa na maandamano ya aina yoyote ile kama ilivyotangazwa mpaka pale jaji mkuu atakapotoa tamko kutokana na madai ya shauri hilo na kama tamko lake halitakidhi mambo yote tunayohitaji kutimiziwa, basi tutaangalia utaratibu mwingine mpaka pale mambo hayo yatakapotekelezwa,” amesema wakili huyo.
Imeandikwa na Mintanga Hunda na Pawa Lufunga (Dar), Eliezel Mgeta (Mwanza) na Amina Mbwambo (Kahama).