Mkazi wa Nyakato ambaye ni Mfanyakazi wa ndani (Hauseboy), Fred Kelendo Marekioli (19), amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Nyamagana Mkoani Mwanza kwa tuhuma za kumfanyia shambulio la aibu mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 5 (jina limehifadhiwa kwa sababu za kisheria).
Akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ramla Shehagilo, Wakili wa Serikali, Tunu Msangi ameieleza mahakama hiyo kuwa tukio hilo lilitokea Septemba 9, 2025 katika eneo la Mwananchi jijini humo, ambapo mshtakiwa anadaiwa kutenda kitendo hicho cha ukatili dhidi ya mtoto huyo mdogo.
Katika kesi hiyo ya jinai yenye namba 22967/2025, mshtakiwa anakabiliwa na shtaka moja la shambulio la aibu, kinyume na Kifungu cha 138C (1)(d)(2)(b) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, marejeo ya mwaka 2023.
Hata hivyo, mshtakiwa amekana shtaka hilo, huku hakimu (Shehagilo) anayesikiliza kesi hiyo akieleza kuwa, kosa hilo linadhaminika kwa masharti, ikiwemo kuwa na wadhamini wawili wenye vitambulisho halali vya taifa, barua za utambulisho kutoka Serikali ya Mtaa na kila mdhamini kusaini hati ya dhamana ya Shilingi milioni moja.
Mshtakiwa ameshindwa kukidhi masharti ya dhamana jambo lililosababisha kurudishwa rumande hadi Septemba 23, 2025, kesi hiyo itakapoitwa kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa hoja za awali
Related