Kocha wa Simba SC, Fadlu Davids, ameaga rasmi klabu hiyo akieleza hisia zake nzito baada ya muda wake kumalizika Msimbazi.
Katika ujumbe wake wa kuaga, Davids amesema tangu siku ya kwanza alipojiunga na Simba alihisi mapenzi makubwa ya klabu hiyo na mashabiki wake, ambao amewataja kama nguzo kubwa ya mafanikio ya timu.
“Kuanzia nilipofika, nilihisi upendo wa klabu hii kubwa na mashabiki wake wa kipekee. Pamoja tulipambana, tukasherehekea, na tukakua imara kupitia kila ushindi na changamoto,” aliandika Davids.
Kocha huyo pia amemshukuru Rais wa Simba, Mohammed Dewji (Mo Dewji), kwa uongozi wake wa kipekee, maono na msaada mkubwa wakati wote.
Kwa wachezaji wa Simba, Davids aliwausia kuendelea kupigania heshima ya nembo ya klabu hiyo na kuamini kila wakati, huku akiwashukuru benchi la ufundi na uongozi kwa imani na juhudi zao zisizo na kikomo.
Aidha, ametoa salamu za dhati kwa mashabiki wa Simba SC akiwataja kama moyo na damu ya klabu:
“Mashabiki wa Simba, ninyi ndio mnapuliza uhai wa klabu hii. Sauti zenu, nyimbo zenu na mapenzi yenu yasiyoyumba hayatoweka kamwe katika kumbukumbu zangu. Asanteni kwa kunikaribisha mimi na familia yangu kama wenu.”
Davids ameahidi kwamba Simba SC itaendelea kubaki sehemu ya maisha yake, huku akitakia klabu hiyo mafanikio makubwa na mataji zaidi siku zijazo.
“Simba daima itabaki sehemu yangu. Nawapeni heri ya mafanikio yasiyo na kikomo, ustawi na makombe mengi zaidi. Asanteni sana, milele Nguvu Moja ❤️🦁,” aliandika kwa hisia.