Dar es Salaam. Ni furaha! Hivyo ndivyo unavyoweza kusema kwa familia ya Ali Kimara (14), mtoto mwenye ugonjwa adimu baada ya kuhitimu elimu yake ya msingi.
Ali ambaye anaishi na ugonjwa huo kwa zaidi ya miaka 10, amefanikiwa kuhitimu elimu yake ya msingi Septemba 11, 2025 na mahafali yake kufanyika Septemba 20, 2025 katika Shule ya Msingi Diamond, iliyopo Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam.
Ugonjwa adimu alionao umeathiri mfumo wake wa upumuaji na hivyo kulazimika kutumia mashine ya umeme inayomsaidia kupumua kwa saa 24 ama kuwekewa mtungi wa gesi pale umeme unapokatika.
Safari ya matumaini ya Ally Kimara akihitimu darasa la saba
Pia umefanya ashindwe kutembea hivyo kumlazimu muda mwingi kuwa amelala kitandani huku akihitaji uangalizi wa karibu.
Hata hivyo, hii si sababu kwa Ali kushindwa kupata haki yake ya msingi ya kupata elimu kama ilivyokuwa kwa watoto wengine wasio na changamoto.
Safari yake ya kuhitimu elimu ya msingi ni kielelezo cha uthubutu, uimara na ujasiri wa Ali pamoja na familia yake kuhakikisha changamoto ya maradhi haiwi kikwazo cha kushindwa kutimiza ndoto zake.
Septemba 21, 2025, Mwananchi lilitembelea nyumbani kwa wazazi wake anakoishi mtoto huyo Mtaa wa Kalenga, Upanga jijini Dar es Salaam kuzungumza na familia yake.
Mama mzazi wa mtoto huyo, Sharifa Mbarak amesema anajisikia faraja na fahari kuona mtoto wake amehitimu elimu ya msingi licha ya changamoto za kiafya zinazomkabili.
“Kama mzazi nina mchanganyiko wa hisia, safari ya Ali ndani ya miaka saba haikuwa rahisi kuna muda anakuwa hospitali wakati wenziye wakiendelea na masomo,” anasema.

“Kwangu haikuwa ni sherehe ya kuhitimu tu kwa mtoto wangu, ilikuwa ni alama ya ushindi kwa watoto wote ambao wanapitia changamoto mbalimbali za kiafya kuwa wanaweza kutimiza ndoto zao,” anasema.
Sharifa anasema, Ali alianza rasmi safari yake ya masomo mwaka 2018 huku milima na mabonde ikiwa sehemu ya safari hiyo.
Anasema kwanza alianza kusoma kabla ya kuanza kutumika rasmi mwongozo wa Shule ya Nyumbani kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu wa mwaka 2023.

Mama mzazi wa mtoto Ali Kimara, Sharifa Mbarak akizungumza wakati wa mahojiano maalumu na Mwananchi ilipomtembelea nyumbani kwake Mtaa wa Kalenga, Upanga jijini Dar es Salaam
Anasema hiyo iliwatia hofu juu ya hatima yake ya kielimu licha ya kuwa tayari walikuwa wamemtafutia walimu waliokuwa wakimfundishia nyumbani.
“Japokuwa alikuwa akifundishwa nyumbani lakini tuliwaza nini hatima yake je, anatambuliwa, atawezaje kufanya mitihani ya kuhitimu ngazi mbalimbali za elimu, ni maswali ambayo tulikuwa tunajiuliza sana kama familia tutamuwezeshaje kupata haki yake ya msingi ya elimu,” anasimulia Sharifa.
Hata hivyo anasema haikuwakatisha tamaa bado walifanya jitihada kuhakikisha mtoto wao anapata elimu hadi pale alipofanikiwa kusajiliwa rasmi katika Shule ya Msingi Diamond Julai 2020 na kuanza kusoma kama mwanafunzi wa darasa la pili.
“Nakumbuka katika maadhimisho ya siku ya magonjwa adimu duniani 2020 Ali alishiriki na kutoa hotuba yake iliyoeleza magumu anayopitia na ndoto zake za elimu, viongozi mbalimbali wa Serikali waliniahidi watapambana kuhakikisha anasoma na kusajiliwa, ndani ya miezi mitatu Ali alisajiliwa na kuanza rasmi kusoma kama watoto wengine,” anasema.
Anasema alipofika darasa la tatu jaribio lake la kwanza Ali alifanikiwa kushika nafasi ya nne kati ya watoto 575 na aliendelea kuingia 10 bora mara kadhaa jambo lililowapa faraja.
“Kufanya vizuri katika masomo kwa Ali kulikuwa kunatupa faraja sana na matumaini kuwa ataweza kutimiza ndoto yake,”anasema.
Nyakati ngumu zenye maumivu
Sharifa anasema nyakati ngumu alizopitia ni kipindi ambacho walilazimika kuwa hospitali kwa siku nyingi kutokana na hali ya kiafya ya Ali kubadilika.
“Alipokuwa darasa la tatu nakumbuka alilazwa kwa takribani mwezi mmoja huku wenziye wakiendelea na masomo iliniumiza sana, hata hivyo baada ya afya yake kuimarika walimu walijitahidi kuhakikisha anasoma kile ambacho alikikosa,” anasema.
Anasema moja ya siku ambayo alikuwa na furaha na hataisahau katika maisha yake ni ile aliyoanza kufanya mitihani yake ya kuhitimu elimu ya msingi.

Ali Kimara (14), mtoto mwenye ugonjwa adimu akitumia kompyuta mpakato akiwa nyumbani kwao Mtaa wa Kalenga, Upanga jijini Dar es Salaam.
Anasema Ali alifanya mitihani yake akiwa amelazwa Hospitali ya Aga Khan.
“Pia alipohudhuria shuleni kwa mara ya kwanza katika mahafali yake ya kuhitimu elimu ya msingi Septemba 20, 2021, namna walimu na wanafunzi wenzake walivyompokea na kufurahi naye, ilinipa faraja sana,” anasema.
Anasema anajisikia faraja kuona Ali amefanikiwa kuhitimu elimu ya msingi na anatamani kumuona anafikia ngazi nyingine.
Akizungumza na Mwananchi, walimu aliyekuwa akimfundisha na kusimamia masomo yake, Lucy Kayange anamuelezea Ali kama mtoto mwenye nidhamu, mdadisi, mpambanaji, asiyependa kukata tamaa.
Kayange ambaye ni mwalimu wa Shule ya Msingi Diamond anasema tangu alipoanza kumfundisha Agosti 2020, Ali amekuwa mtoto mwenye hamu ya kujifunza mambo mbalimbali mapya.
“Tabia hiyo imemfanya Ali kuwa moja ya wanafunzi wanaofanya vizuri masomo yao, mara nyingi amekuwa akishika nafasi ndani ya 10 bora na alipokuwa madarasa ya awali aliwahi hata kushika nafasi ya pili,” anasema.
Anasema safari ya kumfundisha Ali imempa somo la kutokata tamaa katika maisha licha ya changamoto zinazokukabili.
“Japokuwa mimi ni mwalimu wake, Ali amenifundisha kutokata tamaa, licha ya changamoto zake uso wa Ali muda wote ulikuwa na tabasamu,” anasema.
Anasema pia ameona namna ambavyo ushirikiano kati ya wazazi na walimu ni muhimu katika safari ya elimu kwa mwanafunzi
Akizungumzia ndoto zake, Ali anasema anatamani baada ya kuhitimu elimu ya msingi ajiunge na masomo ya amali akijikita katika teknolojia.

Ali Kimara (14), mtoto mwenye ugonjwa adimu akitumia kompyuta mpakato akiwa nyumbani kwao Mtaa wa Kalenga, Upanga jijini Dar es Salaam.
Anasema lengo ni kufikia ndoto ya kuwa mtaalamu wa teknolojia mashuhuri duniani.
“Awali nilitamani kuwa daktari, lakini baadaye nikavutiwa zaidi na teknolojia na namna inavyosaidia kutatua changamoto mbalimbali,” anasema mwanafunzi huyo.
Anasema tayari anafanya jitihada za kuhakikisha anafikia ndoto yake ikiwamo kusoma kozi mbalimbali kwa njia ya mtandao.
“Kupitia ujuzi nilioupata sasa ninaweza kutengeneza tovuti na programu mbalimbali, ninatamani kufanya zaidi ya hapa,” anasema.
Ali anatoa wito kwa wazazi ambao wana watoto wenye changamoto mbalimbali za kiafya wasiwafungie ndani.
“Ninawaomba wawasaidie kupata elimu, wawashike mkono nao watimize ndoto zao,” anasema.
Uwepo wa mwongozo wa shule ya nyumbani kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu wa mwaka 2023, umelenga kusaidia kupunguza vikwazo vya wanafunzi wenye mahitaji maalumu.
Mwongozo huo unaelekeza mazingira ya usomaji ya mwanafunzi mwenye mahitaji maalumu ambaye kwa sababu mbalimbali, hawezi kukaa darasani na kusoma.
Pia, unafafanua namna ya kuratibu, kusimamia, kutekeleza, kufuatilia na kutathmini lengo la kutoa maelekezo yatakayowezesha uboreshaji wa Shule ya Nyumbani.
Historia ya ugonjwa wa Ali
Sharifa, Mama wa Ali anasema mtoto wake alianza kuugua akiwa na miaka miwili, lakini mpaka sasa bado hawajatambua anasumbuliwa na nini licha ya kufanya vipimo vingi hapa nchini na nje ya nchi.
“Mwanangu anasumbuliwa na magonjwa adimu ambayo yanakisiwa kuwa kama 7,000 hadi 8,000 hapa duniani, kwa bahati mbaya mpaka sasa bado hatujatambua ni ugonjwa gani adimu unaomsumbua mtoto kati ya hayo,” anasema mama huyo.
Anasema moja ya changamoto anazokumbana nazo ni gharama kubwa za matibabu kwa mtoto huyo.
“Licha ya kutumia mitungi ya gesi na mashine, unakuta hata bima za afya zina kikomo, siyo kila mtu mwenye watoto kama hawa wanaweza kumudu gharama, tunaiomba sana Serikali kulifikiria hili,” anasema Sharifa.
Anasema licha ya gharama kubwa za matibabu ya Ali, lakini anamshukuru mwajiri wake ambaye anamsaidia kwa kiasi kikubwa kuhakikisha mtoto wake anakuwa na afya njema.
Anaeleza kuwa changamoto ya Ali ndiyo iliyowasukuma kuanzisha taasisi itakayosaidia kupaza sauti ya watoto wanaopitia hali hiyo inayojulikana kama ‘Ali Kimara Rare Disease Foundation’.
Anasema kuwa hadi sasa taasisi hiyo imekusanya Sh100 milioni kwa ajili ya kufanya tafiti kuhusu magonjwa hayo adimu na kusaidia watoto wenye changamoto hiyo.