Dk Mpango aeleza umuhimu wa mifumo kukabili dharura za afya

Dar es Salaam. Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amesema Tanzania inasisitiza umuhimu wa mifumo endelevu ya ufadhili ili kuhakikisha uthabiti wa kukabiliana na dharura za afya ya umma barani Afrika.

Amesema hayo kwenye mkutano wa Kamati ya Wakuu wa Nchi na Serikali wa Kituo cha Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa Afrika (CDC) uliofanyika nchini Marekani. Dk Mpango yupo jijini New York anakohudhuria kikao cha 80 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Amesema Tanzania imedhamiria kuongeza ukusanyaji wa rasilimali za ndani, kuimarisha masuluhisho ya kibunifu ya ufadhili na kuunga mkono mipango ya kikanda ambayo inapunguza utegemezi wa misaada kutoka nje, hivyo kuhakikisha vipaumbele vya afya vya Afrika vinashughulikiwa na serikali.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Philip Mpango akishiriki katika Mkutano wa Kamati ya Wakuu wa Nchi na Serikali wa Kituo cha Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa Afrika (CDC) uliyofanyika pembezoni mwa Kikao cha 80 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Jijini New York nchini Marekani.



Dk Mpango katika taarifa iliyotolewa na ofisi yake leo Septemba 23, 2025, amesema uzalishaji wa ndani wa vifaa vya uchunguzi, matibabu na bidhaa nyingine za tiba ni muhimu katika kujitegemea kwenye sekta ya afya.

Amesema Tanzania inahimiza uwekezaji katika viwanda vya ndani, mamlaka ya udhibiti ya pamoja barani Afrika na ubia wa uhawilishaji wa teknolojia, ili kuimarisha uwezo wa bara kukabiliana na changamoto za kiafya za sasa na zijazo.


Amesema kutokana na uzoefu wa hivi karibuni wa milipuko ya magonjwa ya kuambukiza, ukiwamo Marburg yametoa hitaji la kujiandaa kwa nguvu na mifumo ya kukabiliana na maradhi.

Dk Mpango amesema Tanzania inasaidia vitengo vya matibabu ya magonjwa ya kuambukiza, upelekaji wa haraka wa timu za dharura, na uwekezaji katika miundombinu ya wafanyakazi na afya.


Amesisitiza umuhimu wa kuimarisha nguzo zote za dharura za afya ya umma, ikiwa ni pamoja na ufuatiliaji wa magonjwa, maabara, udhibiti wa maambukizi, vifaa na uratibu kwa ajili ya kukabiliana na milipuko kwa wakati na kwa ufanisi.

Makamu wa Rais ametoa wito wa kuimarishwa ushirikiano kati ya nchi wanachama wa Umoja wa Afrika, jumuiya za kiuchumi za kikanda na Kituo cha Udhibiti wa Magonjwa cha Afrika ili kuwa na mbinu ya pamoja ya  kukabiliana dharura za afya.


Amesema ushirikiano katika uchunguzi, sera na mipango ya pamoja ya kujenga uwezo itaimarisha uwezo wa pamoja wa kuzuia, kugundua na kukabiliana na vitisho vya afya vinavyojitokeza.

Mkutano huo ulilenga kujadili masuala yanayohusu CDC Afrika, chini ya kaulimbiu isemayo: “Kuhakikisha uhuru wa afya Afrika: Uongozi wa kisiasa kwa ufadhili endelevu wa sekta ya afya, uzalishaji wa ndani na maandalizi dhidi ya milipuko ya maradhi.