Ushindi wa medali ya dhahabu katika marathoni kwa mwanariadha Alphonce Simbu kumeifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 20 bora katika mchezo wa riadha kati ya nchi 198.
Tanzania kwa sasa ni nchi ya 19 kwa mujibu wa orodha ya viwango vya dunia iliyotolewa jana na Shirikisho la riadha duniani (WA) na ya tatu katika bara la Afrika kwa nchi zilizoshinda medali katika mashindano ya dunia yaliyomaliza mjini Tokyo, Japan.
Simbu alibuka kinara katika marathon kwa muda wa dakika 2:09:48 na kuwapita wanariadha 89 kutoka nchi mbalimbali. Mbali ya kushinda medali ya dhahabu, Simbu alizawadiwa fedha taslimu ya dola 70,000 (takriban Sh173 milioni).
Kati ya wanariadha 89 walifuzu katika mbio hizo, 66 tu walioweza kumaliza ambapo miongoni mwao ni Josephat Gisemo aliyemaliza katika nafasi ya 53 kwa muda wa 2:22:47.
Kwa mujibu wa jumla ya wanariadha 2,202 kutoka nchi 198, wakishiriki katika michezo tofauti 49 katika mashindano hayo ya 20.
Kwa mujibu wa jedwali la mwisho, Tanzania imezibwaga nchi kama Uingereza & Ireland Kaskazini ambayo ilishiwasilishwa na wanariadha 67), China (wanariadha 88), Ethiopia (36), Afrika Kusini (49), Algeria (9), na Uganda (21).
Orodha hiyo ya WA imeonyesha kuwa, Uingereza ilimaliza nafasi ya 21 kwa jumla ya medali 5 (fedha 3 na shaba 2) bila dhahabu yoyote huku China, licha ya kutuma wanariadha 88, ilifanikiwa kupata medali mbili za fedha tu.
Ethiopia, ambayo ni taifa lenye nguvu katika marathon, iliwakilishwa na wanariadha 36, ilipata medali 2 za fedha na 2 za shaba, ikibaki nje ya nchi 20 bora.
Vivyo hivyo, Afrika Kusini, Algeria, na Uganda hazikuweza kupata dhahabu, jambo linaloonyesha ukubwa wa mafanikio ya Simbu.
Katika orodha hiyo, Marekani imeshika nafasi ya kwanza kwa jumla ya medali 26, zikiwemo dhahabu 16, fedha 5 na shaba 5. Kenya iliifuata kwa dhahabu 7 huku ikipata medali mbili za fedha na mbili za shaba na kufikisha jumla ya medali 11.
Nchi nyingine ambazo zimemaliza nafasi ya tano za juu ni Canada, Uholanzi, na Botswana.