Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Wilson Elias Mulumbe, ana safari yenye hadithi ya aina yake kisiasa.
Inaleta maana kuisimulia kipindi hiki cha Uchaguzi Mkuu 2025, ukibisha hodi. Kila simulizi kuhusu Wilson inaanzia Uchaguzi Mkuu 2015.
Wilson alijipanga kuwania ubunge Jimbo la Tanga Mjini kwa tiketi ya ACT-Wazalendo. Siku zilivyokuwa zinasogea, alijitokeza rafiki wa Wilson, jina lake ni John Mapuri. Kitaaluma, Mapuri ni mhandisi aliyesomea shahada yake Marekani.
Kwa mujibu wa Wilson, Mapuri alikuwa na uwezo zaidi wa kushindania ubunge kuliko yeye.
Kwanza, Mapuri alikuwa na fedha, vilevile rasilimali nyingi ikiwemo magari, ambayo ni nyenzo muhimu wakati wa kufanya kampeni.
Kutokana na tathmini yake, Wilson aliona ni vizuri Mapuri asimame kama mgombea ubunge, halafu yeye arudi ngazi ya kata, aombe kuwania udiwani.
Wilson alianza kujipanga kuwania udiwani Kata ya Duga, iliyopo Wilaya ya Tanga Mjini. Wakati huohuo, alijitolea kumsaidia Mapuri ili apitishwe na ACT-Wazalendo kuwa mgombea ubunge.
Aliamini ingekuwa timu nzuri kwao Jimbo la Tanga Mjini, kama wangeamua kuingia kwenye ulingo wa ushindani wa uchaguzi kwa turufu ya Mapuri.
Haikuwezekana! ACT-Wazalendo walimsimamisha mtu mwingine kuwa mgombea ubunge Tanga Mjini. Mapuri aliachwa. Wilson alichukizwa na uamuzi huo, akaona haki haikutendeka.
Uamuzi wake wa haraka ukawa kuhama chama. Alijiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM).
Akiwa CCM hakusimama kama mgombea, lakini alijitahidi kwa kipimo kizuri kukisaidia chama chake kupata ushindi Tanga.
Baada ya Uchaguzi Mkuu 2015, Wilson anasema alipata mwaliko wa kibiashara China.
Alikaa kwenye nchi hiyo kwa mwaka mzima. Alipotoka China, Wilson alikwenda kuishi Lesotho, kisha maisha yake yakaegemea zaidi mataifa ya kusini mwa Afrika, hususan Zimbabwe na Botswana. Aliamua kujikita zaidi kibiashara kwenye mataifa hayo.
Kipindi chote akiwa nje ya nchi, Wilson alibaki kuishi na ndoto yake ya kufanya siasa Tanzania, akiamini kwamba unaweza kufika wakati Watanzania wenzake wakamwamini na kumpa nafasi ya kuwaongoza.
Wilson anasema kuwa hamasa kubwa ndani yake ni uelewa kuhusu Katiba, mahitaji ya nchi na yale ambayo Watanzania wanakosa.
Uzoefu alioupata wa kuishi kwenye nchi mbalimbali duniani ni hamasa nyingine kwa Wilson, kwamba akipata fursa ya kuongoza dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ataweza kuchagiza mapinduzi makubwa ya kiuchumi na taifa litapiga kasi katika maendeleo endelevu.
Ni hamasa hiyo iliyomfanya aombe kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu 2025. ADC wamempa tiketi. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (Inec) ikamteua. Kazi kwake.
Mwaka 2020, wakati Tanzania ilipokuwa kwenye Uchaguzi Mkuu, Wilson alikuwa amerejea nchini.
Alishiriki mchakato kama raia, alihuisha taarifa zake kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura, siku ya uchaguzi, Oktoba 28, 2020, alijitokeza kupiga kura. Baada ya hapo, alikula yamini kwamba uchaguzi ambao ungefuata, yaani Uchaguzi Mkuu 2025, lazima angeshiriki kama mgombea. Na imekuwa. Wilson ni mgombea urais.
Aprili 2024, alikwenda Makao Makuu ya Tanzania Labour Party (TLP). Katibu Mkuu wa TLP, Yustas Rwamugira, alimpokea Wilson. Akapewa kadi ya uanachama.
Kisha, alianza kujidhatiti ndani ya chama hicho akiwa na matumaini ya kuteuliwa kuwa mgombea urais.
Wilson anasema kuwa, ndani ya muda mfupi akiwa TLP, aliungwa mkono na vijana pamoja na viongozi waandamizi.
Wilson analalamikia mchakato wa kumpata mgombea urais kwa tiketi ya TLP ulivyoendeshwa. Analalamika kutotendewa haki na mazingira ya upendeleo kwa mtu fulani yalikuwa dhahiri. Zaidi, siku ya Mkutano Mkuu wa chama hicho, Juni 27, 2025, Wilson anasema wajumbe bandia walipandikizwa. Hakukubaliana na matokeo, kwa hiyo akaamua kuhama chama.
Baada ya kuachana na TLP, Wilson anasema aligundua kulikuwa na vyama vinne tu ambavyo havikuwa vimekamilisha mchakato wa kupata wagombea urais.
Kwa haraka, alibisha hodi ADC, alipokelewa. Na katika Mkutano Mkuu wa ADC, uliofanyika Julai 27, 2025, Ubungo Plaza, Dar es Salaam, Wilson alishinda uteuzi wa chama.
Agosti 31, 1984, kwenye Hospitali ya Wilaya ya Handeni, Tanga, familia ya Elias Mulumbe, aliyekuwa Ofisa Maliasili wa Wilaya ya Handeni, Tanga na mama Ruth Kimbute, walipata mtoto wa kiume. Jina lake wakamwita Wilson.
Uzao wa Elias Mulumbe na Ruth Kimbute ni watoto wanne. Wilson ni mtoto wa pili.
Mwaka 1992, Wilson aliandikishwa kuanza darasa la kwanza, Shule ya Msingi Mwakizaro, iliyopo Tanga Mjini.
Mwaka 1998, Wilson alihitimu elimu ya msingi. Alipata ufaulu mzuri na kuchaguliwa kujiunga na Shule ya Sekondari Maramba, Wilaya ya Mkinga, Tanga. Kwa mwongozo wa wazazi wake, alichagua kutokwenda shule hiyo ya Serikali.
Badala yake, Wilson alijiunga na Shule ya Sekondari Victory Seminary aliyosoma kwa mwaka mmoja, kisha alihamia Shule ya Sekondari Eckernforde, iliyopo Tanga Mjini, alikoendelea na kidato cha pili hadi cha nne. Wilson alihitimu elimu ya sekondari mwaka 2002.
Wakati anahitimu kidato cha nne, Wilson alishakuwa na mawazo ya biashara. Kwa mtaji alioupata kutoka kwa wazazi wake, alianza biashara ya kusafirisha samaki kutoka Tanga kwenda Arusha. Biashara ilimchanganya, ikamfanya apitishe miaka mitatu bila kurudi shule.
Hata hivyo, mwaka 2005, Wilson alijisajili Shule ya Juu ya Coastal kwa ajili ya masomo ya kidato cha tano na sita. Alijisajili kama mwanafunzi wa kujitegemea.
Alisoma akiwa anaendelea na biashara zake. Wilson alihitimu kidato cha sita mwaka 2007.
Baada ya kufanya mitihani ya kidato cha sita, Wilson alijipa muda kwanza kuendeleza biashara zake. Mwaka 2011, alijiunga na Chuo Kikuu cha Eckernforde, Tanga, alikosomea diploma ya Sheria. Pia amesoma Chuo Kikuu cha Gaborone, kilichopo Botswana, ingawa hajafanikiwa kumaliza programu yake ya shahada ya kwanza.
Wilson ni baba wa watoto wawili, Nicolaus na Elias. Wote wawili mama yao ni Grace Jackson, ambaye ndiye mke Wilson.
Katika mapambano yake ya kuusaka urais, bila shaka anawania pia mkewe awe mwanamke namba moja kwenye nchi (First Lady), pamoja na watoto wao wawe ndiyo familia namba moja Tanzania.
Wilson anasema kuwa, endapo atachaguliwa kuwa Rais wa Tanzania, kitu cha kwanza atafanya ni kuweka usawa wa tozo ya matumizi ya barabara.
Anasema, hivi sasa, mwenye lori na bajaji watozwa sawa, jambo ambalo siyo haki. Anaongeza kwamba mkulima na trekta yake shambani hatumii barabara, lakini anatozwa kodi ya barabara kwa kuwa imeunganishwa kwenye gharama za ununuzi wa mafuta.
Anaeleza kuwa, akichaguliwa kuwa Rais wa Tanzania, atahakikisha haki inatendeka kwa waendesha pikipiki, ili watozwe kidogo kulingana na aina ya vyombo vyao. Anaongeza kwamba mwenye chombo kinachotumia mafuta ya petroli au dizeli, kama hakitumii barabara, hatapewa tozo isiyomhusu.
Wilson anasema kuwa, Watanzania wakimchagua awe Rais, ataanzisha Mfuko wa Ajali za Barabarani kama ilivyo kwa Afrika Kusini.
Anasema, Afrika Kusini mtu akipata ajali analipwa Randi 270,000, ambazo anazilinganisha na Sh40 milioni za Tanzania.
Wilson anasema inawezekana pia Watanzania kulipwa kwa sababu ni raia wenye thamani kubwa.
Anaahidi kumaliza tatizo la maji nchi nzima. Kwanza, anasema atanunua magari ya kuchimba visima kila wilaya, ili Watanzania wote wapate huduma ya maji.
Anasema, hivi sasa kuna watu wengi hawana uwezo wa kulipia huduma ya maji ili waunganishiwe nyumbani kwao, na hawana fedha za kulipa ankara za maji kila mwezi.
Magari ya kuchimba visima kila wilaya yatatoa urahisi kwa watu wote kupata maji bure.
Tanzania chini ya Wilson, mitambo itanunuliwa kwa ajili ya kuchakata maji ya bahari, kuyaondolea chumvi na kuyasafisha ili yafae kwa matumizi ya nyumbani.
Anasema, haifai Dar es Salaam kuwa na uhaba wa maji kwa sababu ya kutegemea Mto Ruvu, ambao uwezo wake ni lita 300,000 kwa siku, wakati inawezekana kupata lita milioni moja kwa siku baharini, yakiwa hayana chumvi.
Wilson anaahidi kushughulika ipasavyo na wapenzi wa jinsia moja, vilevile wanaohamasisha vitendo hivyo.
Anasema, Serikali atakayoiongoza italeta matokeo makubwa ya kilimo; hakuna mchele utanunuliwa kutoka nje, badala yake, Tanzania itauza mchele kwa wingi hadi basmati.
Anaapa kutokomeza ugonjwa wa malaria. Anasema hafurahishwi sasa hivi jinsi elimu bora ilivyoachwa kwa sekta binafsi.
Wilson anaahidi kurejesha hadhi ya shule za Serikali, kama ilivyokuwa zamani. Walimu watalipwa vizuri, kiasi ambacho hata yule mwenye shahada ya Chuo Kikuu ataona fahari kufundisha shule ya msingi.