Wachimbaji wadogo walivyozalisha dhahabu ya Sh3.4 trilioni

Geita. Serikali imesema sekta ya madini imechangia zaidi ya ajira 35,000 kwa vijana na wanawake huku kilo 22,000 za dhahabu yenye thamani ya zaidi ya Sh3.4 trilioni ikizalishwa na wachimbaji wadogo katika kipindi cha miaka minne iliyopita.

Uzalishaji huo umechochewa kupitia fursa za maonyesho ya teknolojia ya madini yanayofanyika kila mwaka mkoani Geita.

Katika kipindi hicho cha mwaka 2021 hadi 2025, Serikali, pia, imepata mapato ya zaidi ya Sh235.5 bilioni kupitia mrabaha na kodi huku migodi mikubwa ikizalisha kilo 76,500 za dhahabu zenye thamani ya ya Sh11.8 trilioni na kuiingizia Serikali mapato ya takribani Sh793 bilioni.

Akizungumza jana Septemba 22, 2025 wakati akifungua maonyesho ya nane ya teknolojia ya madini yanayofanyika Geita, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema maonyesho hayo yamekuwa chachu ya kuunganisha wadau wa sekta ya madini na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

“Maonyesho haya yamekuwa siyo tu jukwaa la kuonyesha teknolojia za uchimbaji, bali pia yameleta mshikamano kati ya wachimbaji wakubwa na wadogo na kupunguza migongano. Hii imeongeza fursa za uwekezaji, biashara na ajira kwa wananchi wetu,” amesema Majaliwa.

Amesema mbali na uzalishaji wa dhahabu kuongezeka, maonyesho hayo yameongeza fursa nyingi za biashara ikiwemo thamani ya mikataba inayosainiwa baina ya wachimbaji, wamiliki wa maeneo na wawekezaji.

Waziri Mkuu amesema mapato yatokanayo na fursa hiyo yameongezeka kutoka Sh50 bilioni mwkaa 2018 hadi kufikia Sh1 trilioni mwaka 2025, fedha hizi zinahusisha mikataba iliyopo, vifaa, huduma mbalimbali na ushirikiano wa uwekezaji unaofanywa,” amesema Majaliwa.


Ameongeza kuwa sekta ya madini imekuwa kwa asilimia 10.6 huku ikichangia pato la taifa kwa asilimia 10.1 na kuutaja Mkoa wa Geita kuwa ndio unaozalisha dhahabu kwa wingi nchini.

Amesema katika kuendelea kukuza sekta hiyo serikali imeendelea kuweka kipaumbele katika uimarishaji wa sekta ya madini ikiwa ni pamoja na kuondoa kero, kupunguza tozo ili kuongeza uzalishaji na kuvutia uwekezaji.

Kiongozi huyo amesema uwekezaji mkubwa umefanywa kwa wachimbaji wadogo kwa kuwapa maeneo ya kuchimba na kuwaunganisha na taasisi za fedha ambapo amewataka wachimbaji kutumia maonyesho hayo kukutana na wadau ili waweze kujifunza zaidi.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka wadau wa sekta ya uchimbaji kuwekeza kwenye teknolojia rafiki na kuongeza thamani ya madini, sanjari na kuhakikisha usalama wa wachimbaji wadogo pamoja na kuimarisha ushirikiano baina ya wachimbaji wakubwa na wadogo kwa lengo la kuongeza thamani.

Aidha, amezitaka taasisi za umma zikiwemo halmashauri zilizopo mkoani humo pamoja na taasisi binafsi kujenga miundombinu ya kudumu ndani ya eneo la maonyesho ili kuyapa hadhi ya kimataifa.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigela amesema sekta ya madini imekua kwa kasi kubwa katika miaka minne iliyopita ambapo wachimbaji wadogo pekee wamezalisha tani 22.5 za dhahabu na migodi mikubwa tani 74.


Aidha, ameainisha kuwa fedha zinazotokana na sekta hiyo zimechangia maendeleo makubwa ya kijamii mkoani humo ikiwemo ujenzi wa shule mpya, hospitali, vituo vya afya na miradi ya kimkakati

“Serikali imetekeleza mambo mengi tumeongeza vijiji vilivyo na umeme kutoka 376 hadi 486, na mradi mkubwa wa maji wenye thamani ya Sh128 bilioni kutoka Ziwa Victoria, unatarajiwa kukamilika Desemba. Haya yote ni kazi iliyofanywa na serikali,” amesema Shigela.

Ushirikiano wa Serikali, wadau

Makamu wa Rais wa AngloGold Ashanti (GGML), Simon Shayo amesema kampuni hiyo imekuwa sehemu ya maonyesho hayo kila mwaka na kwa sasa asilimia 95 ya manunuzi yake wanayafanya hapa nchini na kukuza uchumi wa mtu mmoja na Taifa kwa ujumla.

“Tunashiriki miradi ya kijamii ikiwemo elimu, afya na maji. Tunashukuru serikali kwa kutuunga mkono na tunaahidi kuendelea kuwa wadau wa maendeleo,” amesema Shayo.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Wadogo (GEREMA), Titus Kabuo amesema Serikali imewawezesha wachimbaji wadogo kwa kuwapa mitambo na maeneo ya uchimbaji ambapo wachimbaji wameongezeka kutoka milioni tano hadi kufikia milioni sita nchi nzima.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Yahaya Samamba amesema maonyesho hayo yamekuwa chachu ya mabadiliko makubwa ya kiteknolojia nchini.

“Tulikuwa tukichimba kwa mikono na kutumia zebaki ambayo ni hatari. Sasa tunatumia mitambo ya kisasa na cyanide ambayo ni salama zaidi. Hii imeongeza tija na kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi tano bora Afrika zinazozalisha dhahabu,” amesema Samamba.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dk Janeth Lekashingo amesema taasisi hiyo itaendelea kusimamia kwa uwazi na weledi sekta hiyo ili kuhakikisha manufaa ya rasilimali madini yanawafikia Watanzania wote.

Mkurugenzi wa matawi ya CRDB, Boneventura Paul amesema benki hiyo kupitia programu ya Imbeju ambayo ni maalumu kwa vijana, wanawake na wenye ulemavu, tayari imeingia mkataba na wanawake wachimbaji wadogo wa madini na kuwezesha vikundi 168.