Wanahabari watakiwa kutumia kalamu zao kuunganisha jamii

Dar es Salaam. Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imewataka waandishi wa habari nchini kujikita katika kuimarisha amani, utulivu na demokrasia kupitia kalamu zao ili taifa lipite kipindi hiki cha uchaguzi likiwa na amani.

Wito huo umetolewa jana Septemba 22, 2025 na Katibu Mtendaji wa THBUB, Patience Ntwina wakati wa mafunzo maalumu kwa waandishi wa habari kuhusu haki za binadamu katika kipindi hiki cha uchaguzi mkuu.

Ntwina amesema waandishi wa habari wana wajibu wa kuepuka kutumia lugha ya matusi, kashfa, kejeli, udhalilishaji au vitisho katika kuripoti matukio ya uchaguzi; kuepuka rushwa, takrima au zawadi zenye lengo la kushawishi maudhui yenye kuegemea upande wa chama au mgombea fulani.

Amewataka kuepuka kuchapisha au kutangaza habari zenye nia ya kuchochea vurugu, ubaguzi au chuki za kisiasa, kikabila, kidini au kijinsia. Pia, amesisitiza kwamba ifikapo kipindi cha kupiga kura, waepuke kufanya kampeni kwa namna yoyote ile katika siku husika.

“Ndugu washiriki; THBUB inatoa wito kwa waandishi wa habari kuchukua tahadhari dhidi ya matumizi mabaya ya majukwaa ya habari ikiwemo mitandao ya kijamii.

“Vyombo vya habari vijikite katika kuimarisha amani, utulivu na demokrasia nchini kwa kutotumika vibaya kalamu zenu,” amesema Katibu Mtendaji huyo.

Ameongeza kuwa mafunzo hayo yatasaidia kuweka misingi ya kitaaluma na kimaadili kwa vyombo vya habari, waandishi wa habari na wadau wote wa sekta ya habari, kwa madhumuni ya kuhakikisha haki, usawa, na weledi katika utoaji wa taarifa kwa umma ili kukuza demokrasia.

Vilevile, amesema mafunzo hayo yatasaidia kulinda amani na utulivu kwa Taifa na kuepusha kuchapisha maudhui yenye viashiria vya uchochezi, upotoshaji, kuegemea upande mmoja au yasiyo na uthibitisho.

“Mafunzo haya ni muhimu katika kuwezesha kutekeleza wajibu wetu kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizowekwa ili kuepuka migongano baina ya vyombo vya dola na waandishi wa habari wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.

“Aidha, yataongeza uelewa wa pamoja wa waandishi wa habari kuhusu haki na wajibu wao wakati wanapotekeleza majukumu yao katika kipindi cha uchaguzi, hii itasaidia kuwepo na uhuru wa habari na uhuru wa vyombo vya habari,” amesema.

Kwa upande wake, mwezeshaji wa mafunzo hayo ambaye pia ni ofisa wa THBUB, Kilua Mtae amesema haki za binadamu zina mawanda mapana na zinalindwa na Katiba, sheria na mikataba mbalimbali ya kimataifa ambayo Tanzania imeridhia.

Ametaja baadhi ya haki hizo ni kama vile, haki ya kuchagua na kuchaguliwa, haki ya kupata taarifa, haki ya kutoa maoni, uhuru wa kukusanyika, haki ya kuishi na haki ya kuwasilisha mahakamani uvunjifu wa haki nyingine.

“Ibara ya 130(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaeleza wazi majukumu ya Tume yakiwamo kupokea malalamiko ya ukiukwaji wa haki za binadamu, kufanya uchunguzi, kuelimisha umma na kutoa mapendekezo kwa Mamlaka husika,” amesema.

Philemon Thomas ambaye pia ni mwendeshaji wa mafunzo hayo, amesema kanuni za maadili ya uandishi wa habari za mwaka 2020 zimebainisha mambo muhimu ikiwamo kuripoti uchaguzi kwa usahihi, kuepuka mgongano wa maslahi na haki na usawa.

“Ni muhimu sana waandishi wa habari mkaepuka lugha zinazoweza kuchochea uvunjifu wa amani, chuki na vurugu wakati wa uchaguzi. Mna wajibu wa kuhimiza mshikamano wa kitaifa wakati wote,” amesema.