Dproz yaja na jukwaa kuwasogezea vijana fursa za ajira

Dar es Salaam. Taasisi isiyo ya kiserikali ya Dproz imekuja na suluhisho la ajira kwa vijana kwa kuweka mfumo maalumu utakaowawezesha kupata taarifa kwenye soko la ajira nchini.

Akizungumza mkurugenzi wa jukwaa la kidigitali la Dproz linalounganisha vipaji na nafasi za kazi nchini, Iddy Magohe amesema kufuatia changamoto hiyo ya ajira, wao wamekuja na suluhu.

Magohe amesema watu hawafikiwi na matangazo ya nafasi za ajira zinapotangazwa, hivyo husababisha wengi kuomba nafasi za kazi zinazojulikana na zile ambazo hazijulikani hawazipati.

“Sisi kama taasisi ya Dproz tumeamua kuwa na mfumo maalumu na lengo letu ni kuwasaidia vijana wanaotafuta ajira ili wazifahamu na kujua zinazopatikana kila siku kupitia mfumo wetu,” amesema.

Pia, ametoa wito kwa Serikali kushirikiana na sekta binafsi kama Dproz ili Watanzania wajue nafasi za kazi zilizopo katika soko la ajira, ziko wapi kwani mfumo unasaidia kuwaweka kwenye utaratibu maalumu wa kujua na kumshika bega kijana wa Kitanzania kujua fani yenye mafanikio na kujua ujuzi wake unajulikana wapi.

“Kazi ziko nyingi sana lakini ajira imekuwa shida sana na pia walio vyuoni wameshauriwa kusomea kazi zilizoko sokoni ili iwe rahisi kufanikiwa kupata ajira,” amesema Magohe.

Pia, ameongeza kwamba kozi yoyote inayotangazwa kwenye mitandao, wao kwenye mfumo wao itakuwepo kwani zipo kampuni zaidi ya 4,000 kwenye mfumo wa Dproz na wengi wanafanikiwa.

“Tunatambua kwamba Serikali ina mfumo mzuri wa ajira portal, kwa hiyo sisi kama taasisi tunatafuta namna ya kushirikiana nao ili kuongeza ufanisi wa kupata ajira kwa vijana,” amesema na kuongeza:

“Nawasihi vijana wafuatilie jukwaa hili la kidigitali na kutembelea tovuti ya www.dproz.com kwa kufanya hivyo wataweza kuona namna mifumo inavyofanya kazi na baadhi ya makundi ya watu wanavyonufaika na mfumo huo wa Dproz.

Baadhi ya vijana wamesema mfumo huo utarahisisha zaidi wao kupata fursa mbalimbali, kwani mifumo iliyopo nchini bado haijaweza kuwa rafiki wao kufikiwa na taarifa.

“Kuna Ajira Portal ile ya Serikali lakini zaidi ni matangazo mbalimbali kwenye magazeti, tunategemea zaidi vyombo vya habari. Kama kutakua na mkusanyiko wa fursa eneo moja itasaidia zaidi,” amesema John Mwenda, mkazi wa Tegeta jijini Dar es Salaam.