NDIYO MILIONI 20 ZA HESLB ZITAKAVYOSAIDIA KUBORESHA MASOMO YA SAYANSI NCHINI

:::::::

Na: Dkt. Reubeni Lumbagala, Tanga

Juhudi zinazofanywa na serikali katika kuchochea maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla haziwezi kuzaa matunda kama hakutafanyika uwekezaji wa kutosha katika sekta ya elimu.

Hii inatokana na ukweli kuwa maarifa, ujuzi na stadi mbalimbali ni nyenzo muhimu zinazoharakisha kufikiwa kwa malengo na mipango ya maendeleo. Kwa kuzingatia ukweli huu, ndiyo maana mataifa yote yaliyopiga hatua kubwa za maendeleo ziliipa kipaumbele sekta ya elimu kwa kuhakikisha wanawaelimisha raia wao kikamilifu.

Kwa kuwa Tanzania si kisiwa, tumejifunza kwa wenzetu namna walivyowekeza katika sekta ya elimu na wakafanikiwa, serikali kwa upande wake imefaya kazi kubwa katika uboreshaji wa elimu kuanzia elimu ya awali, msingi, sekondari, vyuo vya kati na vyuo vikuu ili kuharakisha kasi ya maendeleo.

Kazi nzuri zimefanyika katika uboreshaji wa miundombinu ya kutolea elimu kama ujenzi wa madarasa, kumbi za mihadhara, maktaba, mabweni, vyoo, ofisi na nyumba za walimu, kutoa vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kama kompyuta, kuajiri walimu wapya, ununuzi wa vitabu, kutaja kwa uchache.

Serikali inawashirikisha kikamilifu sekta binafsi, wabia wa maendeleo, taasisi na mashirika yasiyo ya kiserikali, asasi za kiraia, watu binafsi na wananchi kwa ujumla katika kusaidia uboreshaji wa elimu.

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) ni moja ya taasisi muhimu chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia yenye jukumu la kutoa mikopo kwa waombaji wenye sifa na kukusanya fedha hizo ili zitumike katika kuwasaidia wengine kupata elimu ya juu.

Katika kuadhimisha miaka ishirini tangu kuanzishwa HESLB, wananchi na wadau mbalimbali walishirikishwa kuchangia fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya maabara katika shule mbili za sekondari, moja ya Tanzania Bara na nyingine ya Zanzibar ili kusaidia kukuza ufaulu wa masomo ya sayansi kama vile Baiolojia, Kemia, Fizikia na Uhandisi ambayo ni muhimu sana katika kuchagiza maendeleo.

Ni faraja kuona namna wadau walivyounga mkono mpango wa HESLB kusaidia kuboresha masomo ya sayansi ambapo HESLB imefanikiwa kutoa shilingi Milioni ishirini ambapo Shule ya Sekondari Temeke ya Jijini Dar es Salaam na Shule ya Sekondari Hasnuu Makame ya mkoa wa Kusini Unguja kila moja imepata shilingi Milioni kumi kwa aili ya ununuzi wa vifaa vya maabara.

Katika makabidhiano ya hundi ya Milioni kumi kwa Shule ya Sekondari Temeke, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia alisema “Pamoja na kuwa tunatimiza ahadi tuliyoitoa, msaada huu pia ni sehemu ya jitihada za HESLB katika kuunga maendeleo ya sekta ya elimu, hususani masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM). Tunatambua kuwa Taifa letu haiwezi kufikiwa uchumi wa kati wa viwanda bila kuwekeza elimu ya sayansi na teknolojia kuanzia ngazi za chini.”

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Dkt. Mwanakhamis Ameir alikuwa miongoni mwa waliohudhuria hafla ya makabidhiano ya hundi ya shilingi Milioni kumi kwa Shule ya Sekondari Hasnuu Makame ambapo aliwapongeza HESLB kutoa fedha hizo. “Nashukuru HESLB kwa msaada huu ambao utaenda kusaidia kupata vifaa vya maabara katika skuli hii ya Hasnuu Makame. Nasisitiza fedha hizo zitumike kwa uadilifu na umakini mkubwa ili kuhakikisha vifaa muhimu vinapatikana na wanafunzi wanapata fursa ya kujifunza kwa vitendo. Huu ni uwekezaji kwa wanafunzi na Taifa linawaangalia kama viongozi na wataalamu wa kesho,” amesisitiza Dkt. Ameir.

Kwa nyakati tofauti, Wakuu wa shule hizi mbili walionufaika na fedha hizo, Bakari Ali wa Hasnuu Makame Sekondari na Ingia Mtenga wa Temeke Sekondari kwa pamoja waliwashukuru HESLB kwa kusaidia upatikanaji wa fedha hizo ambazo zitawezesha ununuzi wa vifaa vya maabara, hivyo kusaidia kukuza na kuboresha ufaulu wa masomo ya sayansi.

Kimsingi, Milioni ishirini zilizotolewa na HESLB kufanikisha ununuzi wa vifaa vya maabara ni mwelekeo mzuri wa kusaidia juhudi za kuinua elimu nchini hasa masomo ya sayansi. Aidha, wanafunzi wanao wajibu wa kuthamini fedha hizo zilizotolewa kama chachu ya kuongeza bidii ya kujisomea ili waweze kutimiza ndoto zao za maisha kwa kupata elimu bora tena ya vitendo na si nadharia pekee.

Dkt. Reubeni Lumbagala ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Funguni ya wilayani Pangani mkoani Tanga.

Maoni: 0620 800 462.